Taifa Gas yapewa tuzo kwa utunzaji mazingira

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amekabidhi tuzo maalum kwa kampuni ya nishati ya gesi ya kupikia ya Taifa Gas Limited ikiwa ni ishara ya serikali kutambua juhudi za kampuni hiyo katika utunzaji wa mazingira sambamba na kuunga mkono kampeni ya kumtua mama kuni kichwani inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Kampeni hiyo inalenga kuwasaidia na kuwawezesha wananchi  kuifikia nishati hiyo kwa urahisi.

Dk. Mpango amekabidhi tuzo hiyo kwa Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius leo Jumatano jijjini Dodoma kwenye kilele cha Maadhimisho wiki ya Mazingira iliyofanyika jijini humo na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa kitaifa akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk.Seleman Jafo; Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Zungu pamoja na wadau wengine wa mazingira.

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango  (wa pili kulia) akikabidhi tuzo maalum kwa Meneja Mkuu wa Kampuni ya kuzalisha na kusambaza nishati ya gesi ya nyumbani ya Taifa Gas Limited, Devis Deogratius (kushoto).

Akizungumzia tuzo hiyo kwa niaba ya Kampuni ya Taifa Gas, Deogratius aliishukuru serikali kwa kutambua jitihada za kampuni hiyo katika uwajibikaji wake kwa jamii ikiwemo kuiunga mkono serikali na viongozi wake waandamizi katika kufanikisha adhma ya kuandaa taifa linalotegemea nishati safi ya kupikia kwa kuendelea kutoa mitungi ya gesi na elimu ya matumizi ya gesi lengo likiwa ni kupunguza matumizi ya kuni na mkaa miongoni mwa wananchi mijini na vijijini.

“Kuanzia mwaka jana hadi sasa, Taifa Gas tumegawa bure mitungi 20,000 yenye thamani ya Sh. 1.52 bilioni  kwa watanzania wenye mahitaji kwa ajili ya kuendeleza kampeni hii ya nishati safi nchini. Serikali ina malengo ya kuhakikisha tunafikia nchi yenye nishati safi ifikapo 2034, hivyo  kampuni ya Taifa Gas tutaendelea  kuunga mkono juhudi hizi ili tuweze kufikia malengo ya pamoja” Alisema Deogratius.

Alisema kampuni hiyo mbali na  kutoa mitungi ya gesi bure kwa Watanzania, inaendelea na mpango wake wa kutoa elimu kuhusu nishati safi sambamba na kutoa fursa za kiuchumi kwa watanzania ambao wangependa kuwa mawakala wa kampuni hiyo kote nchini.

Katika muendelezo wa kampeini ya utunzaji wa mazingira, Deogratius alisema kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha kwamba  kila Mtanzania mwenye nia ya kutumia nishati safi ya gesi anapata fursa hiyo kupitia vituo vya usambazaji ya taifa gas ambayo vinapatikana kila mkoa  kote nchini.

“Tanzania inapoteza takriban ekari 400,000  za misitu kila mwaka kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa na Taifa Gas ni miongoni mwa kampuni ambazo zimejitolea kusaidia serikali katika jitihada hizi.’’ alisisitiza

Related Posts