Simba Queens ipo katika mazungumzo na beki wa kati wa Yanga Princess, Noela Luhala anayemeliza mkataba wake na klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Simba inahitaji beki huyo kwa makubaliano maalumu ya kumuazima kwa ajili ya kuwasaidia kwenye michuano ya kimataifa ambayo kama Simba itachukua ubingwa wa Ligi Kuu ya wanawake awasaidie eneo la ulinzi.
MABOSI wa Ihefu wameanza hesabu mapema za kuhakikisha wanakisuka kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao na tayari wameanza kuifukuzia saini ya kiungo mkabaji raia wa Congo, Harvy Ossete ambaye anaichezea timu ya FC Saint Eloi Lupopo kwa sasa.
Harvy mwenye umri wa miaka 24, mkataba wake na FC Lupopo unafikia tamati mwakani japo viongozi wa Ihefu wameingilia kati dili hilo na wapo tayari kufanya mazungumzo ya kumsajili nyota huyo kwa ajili ya kuboresha eneo hilo muhimu msimu ujao. Kabla ya Lupopo, nyota huyo aliichezea Diables Noirs Brazzaville.
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Zambia, Red Arrows wameripotiwa kuwa katika mazungumzo ya kumsajili winga wa zamani wa Simba, Peter Banda ambaye kuna kipindi alikuwa pia akihushishwa na Singida Fountain Gate. Winga huyo anatajwa kupewa ofa ya kusaini mkataba wa miaka miwili na wababe hao, huku awali alihusishwa na KMC na Suingida Fountain Gate.
KLABU ya Ihefu iko mbioni kukamilisha usajili wa beki wa kushoto wa Al Hilal ya Sudan, Ibrahim Imoro kwa ajili ya msimu ujao.
Nyota huyo aliyewahi pia kucheza timu mbalimbali ikiwemo, Asante Kotoko, Bolga All Stars, Karela United FC zote za kwao Ghana, kwa sasa yupo huru jambo ambalo limewafanya mabosi wa Ihefu kumtolea macho huku mazungumzo kati yao yakiendelea.