Kiteto. Wafugaji wa Kijiji cha Irkishibor wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati mgogoro wao wa ardhi baina yao na pori la akiba la Mkungunero ili shughuli za ufugaji na uhifadhi ziendelee.
Wafugaji hao wamewatuhumu baadhi ya askari wa pori hilo kuwanyanyasa, kukamata mifugo yao, kuvunja maboma yao yenye kaya 2,856 zenye watu 5,000.
Hata hivyo, Mhifadhi Mkuu wa Pori la Akiba la Mkungunero, Flora Kalambo akizungumza na Mwananchi amesema kwa sasa hakuna mgogoro baina yao na wafugaji wa kijiji hicho.
Bali amekiri kwamba mwaka 1995 kulikuwa na mgogoro uliosababishwa na muingiliano wa mipaka ya vijiji vya Irkishibor, Kimotorok na Loiborsiret vya wilayani Simanjiro.
“Vijiji hivi vilipimwa na kuingizwa mkoani Dodoma katika pori hilo na mwaka 2019 mgogoro huu ulitolewa maelekezo na Serikali na mwaka 2022 wakafuata maagizo ya Baraza la Mawaziri yalipotolewa, kwa hiyo hakuna mgogoro tena kama wanavyodai,” amesema Kalambo.
Amesema Serikali iliwataka kufanya uthamini kwa vijiji vya Mkoa wa Dodoma na kuwalipa fidia wananchi 158 waliokuwa na maboma kwenye pori hilo.
Amesema mpaka sasa tayari wananchi 125 tayari walishalipwa fedha na 33 pekee bado hawajalipwa kwa sababu walikuwa hawana akaunti za benki, vitambulisho vya Taifa na matatizo ya mirathi.
“Kwenye Mkoa wa Manyara, tulibaini Kijiji cha Kimotorok maboma 39 yapo wilayani Kondoa mkoani Dodoma na tulipaswa kumega ekari 558 ili kuwahamishia Mkungunero,” amesema.
Na kwa upande wa Kijiji cha Irkishibor, Kalambo amesema baada ya kufanya tathmini Mkungunero ilipaswa kumega ekari 11,891 ili izirejeshe kwa wananchi wa kijiji hicho.
Amesema vitongoji vya Lombenek, Imbopom na Elichura baada ya kumegwa, viwili vilibaki Kiteto ila Elchura kipo ndani ya pori la akiba la Mkungunero upande wa Wilaya ya Kondoa.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 5, 2024, wafugaji hao wamemuomba Rais Samia aingilie kati mgogoro wao huku wakisema wamechoka kuonewa.
Mmoja wa wafugaji hao, Jackson Ole Kau amedai wafugaji wa eneo hawana mahali pa kwenda, hivyo wanamuomba Rais asikilize kilio chao.
“Sisi wafugaji tunateseka mno, hatuna mahali pa kwenda tunanyanyaswa na askari wa Mkungunero,” amesema Ole Kau.
Amesema pori la Mkungunero ni tishio kwao na kuna kipindi iliwahi kuundwa timu ya mawaziri saba ila wakashidwa kuutatua mgogoro wao.
Mfugaji mwingine wa eneo hilo, Julius Simon amesema askari wa pori la Mkungunero, wanawaondoa kwenye makazi yao ya kudumu ambayo mababu zao walizaliwa.
“Wametuharibia visima vyetu 22 vya maji vya asili vilivyokuwa vinanywesha mifugo kwenye vitongoji vyetu vitano vilivyopo katika kijiji chetu,” amesema Simon.
Amesema tatizo lililopo ni mwingiliano wa mipaka baina yao na pori hilo la akiba la Mkungunero ambalo makao makuu yake yapo wilayani Kondoa.
“Hili tatizo liliwahi kufikishwa hadi bungeni, Waziri wa Maliasili na Utalii, wakati huo alikuwa Ezekiel Maige ila hadi sasa bado changamoto ya wafugaji kunyanyasika haijapatiwa ufumbuzi,” amedai mfugaji huyo.
Amesema ifike wakati sasa Serikali itazame mgogoro huo kwa jicho la kipekee na iumalize.