Dar es Salaam. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), wamezindua kampeni ya kutoa elimu ya lishe kwa njia ya daladala lengo kufikia watu milioni 32.
Kampeni hiyo itawanufaisha wakazi wa Dar es Salaam, Mbeya na Zanzibar ambapo kila mwananchi atapewa tiketi bure ya daladala maalum zilizotengwa kwenye vituo vya mabasi na ndani ya usafiri huo kutakuwa na wataalamu wa kutoa elimu ya lishe.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa katika kituo cha daladala makumbusho Dar es Salaam Juni 4, 2024 imeanza kutekelezwa leo katika mkoa wa Dar es Salaam, Mbeya na Zanzibar kwa upande wa Unguja pekee.
Hatua hii ni kukabiliana na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano ambapo takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 (TDHS-MIS) zinaonyesha,asilimia 30 ya watoto nchini wamedumaa.
Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule, amesema elimu ya lishe kwa wananchi ni muhimu.
Amesema licha ya wananchi kuzalisha chakula kwa kiwango kikubwa bado tatizo la lishe kwao ni kubwa.
“Ukienda baadhi ya maeneo utawakuta watoto wenye ukondefu, wengine wanene kupitiliza na kudumaa hakuna sababu ya Watanzania kuwa na shida ya lishe.Nishukuru kwa ubunifu huu wa kutoa elimu, naamini lengo la kufikia watu milioni 32 litavukwa,”amesema.
Naye Mwakilishi Mkaazi wa FAO Tanzania Nyabenyi Tito Tipo, amesema kampeni hiyo itafanyika kwa mwezi mmoja.
Amesema wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine ambayo mradi huo utatekelezwa, kutakuwa na tiketi za daladala maalumu zitakazotumika kuwasafirisha abiria.
“Abiria watakaofuzu mafunzo hayo watapewa kuponi ya kwenda kuchukua mbogamboga na vyakula vya makundi mbalimbali sokoni,”amesema na kuongeza kuwa,
“Tutatoa elimu ya lishe kupitia daladala na tunategemea kufikia watu 900 moja kwa moja na milioni 10 kwa njia ya vyombo vya habari, lengo letu kufikia Agosti 2024 tuwe tumewaelimisha watu milioni 32,”amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dk Germana Leyna amesema, kampeni hiyo ni mbinu ya kutoa elimu ya mtindo bora wa maisha.
“Elimu itakayotolewa ndani ya daladala itazingatia ushauri wa kitaalamu kutoka kwenye Mwongozo wa kitaifa wa Chakula na Ulaji wa Tanzania Bara kwa kuzingatia mapendekezo ya makundi sita ya chakula pamoja na utayarishaji na uhifadhi usalama wa chakula, kushughulisha mwili na kuepuka tabia hatarishi,
Akizungumzia hatua hiyo, Ofisa Mfawithi Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) Rahim Kundo amesema mamlaka hiyo itatoa ishirikiano kufanikisha kampeni hiyo kwani lishe lishe ni jambo la msingi.
“Ili kufanikisha kampeni hii ni muhimu abiria elimu itolewe kwa makundi yote ndani ya jamii, wapo abaria wengi wanasafiri jioni na asubuhi na wapo wengine mchana hivyo ni muhimu wote waguswe ma elimu hii,”amesema.
Mpango huo wa elimu ya lishe kwa wananchi kupitia usafiri wa daladala unafadiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa AGRICONNEC.