Wawili mbaroni kwa kubaka, kumuua mtoto wa miaka miwili

Songwe. Wanaume wawili wakazi wa wilaya ya Songwe Mkoani Songwe wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo Kwa tuhuma za kumbaka na kumuua mtoto mdogo wa kike (2) mkazi wa Kaloleni wilayani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo Augustino Senga  amethibitisha hayo leo Juni 5,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio ya jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa jeshi hilo katika kipindi husika linawashikilia watuhumiwa 680 kwa tuhuma ya kujihusisha na matukio ya ukatili wa kijinsia, uvunjaji, wizi, mauaji, utapeli.

Kamanda Senga amesema watuhumiwa hao walifanya tukio hilo Mei 9 mwaka huu kwa kumchukua mtoto huyo na kwenda kumbaka kwenye shamba la mahindi umbali wa mita 130 kutoka nyumbani kwao na siku moja baadaye mwili wa mtoto huyo ulipatikana kwenye shamba la mahindi akiwa amefariki.

“Watuhumiwa hao ambao wanajihusisha na uchimbaji wa madini walitekeleza tukio hilo, baada ya mama mzazi wa mtoto huyo kumwacha mwanawe amelala ndani na yeye kwenda kuchota maji kisimani,” amesema kamanda Senga.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina kutokana na shughuli za watuhumiwa za uchimbaji wa madini.

Kamanda Senga amesema upelelezi wa shauri hili bado unaendelea na pindi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Katika hatua nyingine kamanda Senga amezungumzia kukamatwa kwa watuhumiwa wengine akiwemo Osea David Clement Simwanza (32) kufanya ngono na  ndugu wa damu (maharimu).

Pia Simon Salati Mwakasula (30) alifikishwa mahakamani kwa kosa la kubaka kesi namba 70/2023 na 3985/2024 na kuhukumiwa miaka 30 jela katika mahakama ya Wilaya ya Momba na Songwe kila mmoja.

Mtuhumiwa Yohana Loti Mwashala (36) yeye  alifikishwa mahakamani kwa kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi kesi namba 04627/2024 na kuhukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kubaka na miaka 20 jela kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi.

Mtuhumiwa Baraka Watson Kameme (28) alifikishwa mahakamani kwa kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi kwa kesi namba 61/2023 na kuhukumiwa miaka 30 jela kwa kesi ya kubaka na miaka 30 jela kwa kesi ya kumpa mimba mwanafunzi katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi.

‘’Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe ambao wanajihusisha na uhalifu na vitendo vya ukatili wa kijinsia kuacha mara moja kwani hawatoweza kukwepa mkono wa sheria,’’ amesema.

Related Posts