BoT waja na kampeni dhidi ya mikopo umiza

Dodoma.  Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeidhinisha mpango maalumu wa elimu kwa umma kupitia kampeni ya ‘Zinduka usiumizwe kopa kwa maendeleo’ ukiwa na lengo la kutatua changamoto ya mikopo umiza nchini.

Mikopo hiyo ambayo imepachikwa majina mengi ikiwemo kausha damu, komandoo, pasua moyo, kichefuchefu, imekuwa ikitajwa kuwa chanzo cha kufilisika, kujiua, kuvunjika kwa ndoa na kupata magonjwa ya akili baada ya wakopaji kushindwa kuilipa kutokana na masharti magumu.

Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Huduma Ndogo za Fedha, Kurugenzi ya Usimamizi wa Fedha, ya BoT, Deogratiaus Mnyamani ameyasema hayo leo Juni 6, 2024 wakati wa semina ya waandishi wa habari.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo itaanza Julai mwaka huu kupitia makundi mbalimbali vikiwamo vyombo vya habari, wasanii, vibonzo, semina za walimu, washereheshaji, wabunge na viongozi wa dini.

Amesema kampeni hiyo itakayofanywa kwa makundi yote ya jamii itawaelimisha kusoma masharti ya mikataba ya ukopeshaji, haki zao kama wateja, masuala ya riba, tozo ada, marejesho ya mikopo, dhamana ya mikopo na iwapo mtoa huduma amesajiliwa na BoT kutoa huduma hiyo.

 “Imeonekana kuwa Watanzania wengi wanahitaji kuzinduliwa. Umma unatakiwa uamshwe utoke pale ambapo umesinzia. Watu wengi wanaonekana kuchukua mikopo lakini ukiwauliza hawajui kigezo na masharti ya mkopo aliochukua,” amesema. 

Amesema wamebaini wanaoumizwa na mikopo wengi wao hawajui riba wala muda gani na anachokijua ni kiasi cha rejesho analotakiwa kurejesha.

 “Kwa mfano mtu anapokwambia nakupa riba ya asilimia 10 lazima akwambie kuwa ni asilimia 10 kwa wiki, kwa mwezi ama kwa mwaka. Hizi zote kwa kifedha zina maana tofauti kabisa. 

Akikwambia kuwa anakupa mkopo kwa asilimia 10 lazima akueleze ni kwa muda gani,” amesema.

Amesema mtu anapokwambia kuwa mkopo ni asilimia 10 kwa mwezi ina maana ni asilimia 120 kwa mwaka.

 “Kwa sababu ya mahangaiko mengi BoT ililazimika kutoa mwongozo wa kutoa riba isiyozidi asilimia 3.5 kwa mwezi ambayo ni asilimia 42 kwa mwaka. Anayetoza zaidi ya hapo ina maana kuwa amelenga katika kuumiza wananchi,” amesema. 

Amesema mkopaji ahakikishe kuwa ana nakala ya mkataba wa ukopaji iliyosainiwa, ili siku anapokuwa na malalamiko akienda BoT aionyeshe.

Kuhusu mikopo kwa njia ya mtandao, Mnyamani amesema ukopeshaji kwa njia ya mtandao, ni eneo jingine ambalo BoT inahitaji kuja na miongozo rasmi kwa kuwa vinginevyo ni eneo jingine ambalo litakuwa jipu nchini. 

Akizungumza na Mwananchi Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara, Dk Nasibu Mramba amesema njia nzuri wangeangalia kwa watoa huduma badala ya kualia wahitaji.

“Mara nyingi ukitaka kuangalia kitu unaangalia walio wengi na wahitaji ni Watanzania wote, kila mtu anahitaji fedha. Huko ni wengi hiyo elimu itafikia lini?,” amesema.

Amesema yeye anafikiri kwa kuwa watoaji wa mikopo inayoumiza wananchi wanafahamika, ni vyema Serikali ikaenda kupambana nao mbali na kutoa elimu ya mikopo kwa wananchi.

 “Watu wanaochukua mikopo hiyo wameshajaribu njia nyingine wameshindwa, mtu ana mwanaye hospitali hana fedha anakwenda kukopa huko. Halafu zamani tulisema kuwa wanakwenda huko (mikopo umiza) kwa sababu hakuna vyombo vya fedha kama benki.

“Hivi sasa benki zipo kibao, unakopa hata kwa njia ya simu lakini wanakimbilia huko kwa sababu ni za haraka na zinapatikana kiurahisi na wakopeshaji ni waongo,” amesema. 

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Dk Lutengano Mwinuka amesema suala la kutoa elimu ni zuri kufanyika lakini ni vyema watu wakakumbushwa kuweka mpango wa urejeshaji wa mikopo kabla kuuchukua.

Pia amesema ni vizuri kukawa na fomu ambayo itawezesha wakopaji kushirikisha watu wa karibu kabla ya kukopa ili inapotokea changamoto basi suala la urejeshaji lisikwame. 

“Utaratibu unaweza kuboreshwa kwa kuhakikisha kunakuwa na fomu ambayo inahusisha wadau muhimu ili washauriane kabla ya kuchukua mkopo husika,” amesema.

Sakata la mikopo kausha damu limekuwa likijitokeza kila mara bungeni wabunge wakitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya mikopo hiyo.

Mei 18, 2023 Mbunge wa Viti Maalumu Angelina Malembeka alilieleza Bunge kuwa wanawake wamekuwa wakihangaika mitaani na mikopo inayowadhalilisha inayojulikana kama kichefu chefu, rusharoho, komandoo, pasua moyo na kausha damu.

Hata hivyo, Mei mwaka 2024, suala hilo liliibuka tena bungeni ambapo Mbunge wa Viti Maalumu, Felista Njau alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kwa kuwa wananchi mitaani wanaadhirika kwa kusombewa mali zao wanapochelewa kulipa.

Swali hilo lilisababisha mjadala huo kuwa mpana hadi Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuwaagiza mawaziri, Dk Mwigulu Nchemba (Fedha) na Nape Nnauye (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) kwenda kulifanyia kazi kwa kuwa riba zake zimekuwa kubwa na zinawaumiza wananchi.

Related Posts