Musoma. Jeshi la Polisi mkoani Mara limewafikisha mahakamani watuhumiwa 36 wa makosa mbalimbali ya ukatili wa kijinsia, akiwemo Nyaikorongo Mwita aliyedaiwa kumlisha kinyesi mke wake, baada ya kumpiga na kumjeruhi.
Akisimulia tukio hilo leo Ijumaa Juni 7, 2024 wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa jeshi hilo kwa mwezi Mei 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase amesema, Mwita alitenda kosa hilo Novemba, 2023 katika Kijiji cha Nyamburi Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Hata hivyo, Mwita alihukumiwa kifungo cha miezi 12 jela na kulipa faini ya Sh2 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumpiga mke wake kisha kumlisha kinyesi chake, hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Serengeti Mei 30, 2024.
“Hili tukio lilitokea Novemba 22, 2023 na limechukua muda mrefu kidogo mtuhumiwa kufikishwa mahakamani kwani baada ya kufanya tukio alitoroka lakini tulifanikiwa kumkamata akiwa amejificha mkoa jirani na kumrejesha mkoani kwetu, kisha kumfikisha mahakamani na tayari sheria imechukua mkondo wake,” amesema.
Akieleza namna tukio lilivyotokea, Morcase amesema siku ya tukio saa 2 usiku mwanaume huyo alirudi nyumbani akiwa amelewa na kuanza kumpiga mtoto aliyekuwa akilia muda huo.
Amesema kutokana na kipigo hicho, mke wake alihoji kwa nini mtoto anaadhibiwa, ndipo mwanaume huyo alipoacha kumpiga mtoto na kuanza kumshambulia mke wake kwa makofi na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake, kabla ya kumlisha kinyesi chake.
“Huu ni ukatili uliopitiliza yaani unampiga mke wako na kama haitoshi unamlisha na kinyesi, kwa kweli hili tukio mbali na kuwa ni ukatili lakini pia lilivuta hisia za watu wengi na kuhuzunisha pia.
“Hivyo na sisi tulisema lazima mtuhumiwa afikishwe mahakamani na sheria ichukue mkondo wake, niwaombe watu wa Mara kwa pamoja tukatae ukatili kwa wanawake na watoto, hebu tuseme sasa basi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo amesema kati ya kesi 36 zilizofikishwa mahakamani, 13 zimetolewa hukumu na watuhumiwa wamehukumiwa kutumikia adhabu mbalimbali ikiwemo vifungo vya muda tofauti gerezani.
“Zaidi ya watu watano wamefungwa kifungo cha miaka 30 kila mmoja jela na wengine kufungwa maisha kwa makosa ya ubakaji na ulawiti wa watoto na wengine kupewa vifungo tofauti katika mahakama zetu,” amesema.
Amesema kesi zingine 13 zinaendelea zikiwa katika hatua mbalimbali na kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya jeshi hilo na wananchi.
Jeshi hilo pia limewakamata watuhumiwa 346 wa makosa mbalimbali katika operesheni maalum ya kuzuia na kutokomeza uhalifu iliyofanywa mkoani humo mwezi mmoja uliopita.
Wakizungumza kuhusiana na matukio hayo, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamelipongeza jeshi hilo kwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wameomba utaratibu huo uwe endelevu.
Asha Mohamed amesema vitendo vya ubakaji na ulawiti vinazidi kuongezeka hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika kupambana navyo.
“Kizazi cha sasa hakiko salama, hivyo kasi hii ya polisi inaweza kurejesha usalama kwani hawa wabakaji wanatakiwa kupata funzo kwa wenzao, waliofungwa wajue kuwa wakiendelea na vitendo hivyo basi jela inawahusu,” amesema Nyagiro Thobias
Neema Agostino amesema jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili wahusika wengi waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.