LIGI Kuu ya Wanawake inaendelea leo baada ya kusimama tangu Mei 14, mwaka huu, huku Simba Queens ikihitaji ushindi ili kutwaa ubingwa huo ambao waliukosa msimu uliopita mbele ya JKT Queens.
Simba Queens itakuwa ugenini leo katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni ikiwakabili wenyeji wao, Alliance Girls ambao ushindi kwao ni wa lazima ili wajinusuru na hatari ya kushuka daraja.
Alliance Girls inakamata nafasi ya tisa ikiwa na pointi 10 baada ya michezo 15, ikishinda tatu, sare moja na kupoteza 11, huku Simba Queens ikiwa kileleni na alama 43 ikiwa haijapoteza mchezo, ikifuatiwa na JKT Queens yenye pointi 34.
Kocha wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka alisema mchezo huo ni mgumu kwao lakini hawaogopi kwani wamejiandaa kucheza kwa nidhamu kubwa, kuiheshimu Simba lakini wakihitaji alama tatu za kuwatoa chini.
Chobanka alisema katika mechi tatu walizobakiza ukiwemo dhidi ya Yanga Princess na Simba Queens wanahitaji kupata alama zote tisa ili ziwasaidie kuepuka hatari ya kushuka daraja, huku akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi leo kuwapa nguvu.
“Tunaendelea na maandalizi tumeanza mazoezi leo (Jumanne) baada ya wachezaji waliokuwa timu za taifa kurejea, tunaendelea kupambana tuone kama Mungu atatusaidia.
Tunaingia katika mchezo huu tukiwaheshimu wapinzani, kujua udhaifu na uimara wao,” alisema Chobanka
“Hivyo tutacheza kwa nidhamu, ni mechi inayotaka tucheze kwa mkakati na siyo kukurupuka, tunataka tupate pointi tisa katika mechi hizi tatu za mwisho zitusaidie. Mashabiki wa Mwanza waje watupe hamasa tunajiandaa tupate kitu kizuri cha kwenda nacho dhidi ya Simba Queens,” alisema.