Biteko aiagiza Tanesco kujenga laini mpya ya umeme Ushirombo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujenga laini mpya ya umeme kutoka Nyakanazi-Ushirombo na Kahama Bongwe hadi Bukombe ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa umeme katika  Wilaya ya Bukombe inaimarika. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Dk. Biteko ametoa agizo hilo alipozungumza na wananchi wa Jimbo la Bukombe, Mkoa wa Geita ambapo amesema kuwa sambamba na ujenzi wa laini hizo za umeme, kutajengwa kituo cha kupoza Umeme Bukombe ili kuhakikisha wananchi wakiwemo wa Ushirombo wilayani Bukombe wananufaika na umeme wa uhakika.

‘’ Umeme tunaopata Bukombe unatoka Bulyanhulu,  unapita Mbogwe na kuja  Bukombe ambapo  ukifika hapa unakuwa na nguvu hafifu na ikitokea hitilafu Bulyanhulu Bukombe pia inakosa umeme hivyo ni vema TANESCO ikajenga laini hizo mpya  ili wananchi wa Bukombe wapate umeme wa uhakika,” amesema Biteko.

Kuhusu uwepo wa umeme wa kutosha nchini, Dk. Biteko amesema  Serikali  imefanya kazi kubwa ya  kuhakikisha wanaondoa mgao wa umeme  kwa kuongeza vyanzo mbalimbali vya uzalishaji umeme na hivyo  kuondoa tatizo la kukatika mara kwa mara kwa nishati hiyo.

Related Posts