Kigali. Matumaini ya Diane Rwigara kugombea urais katika uchaguzi wa Julai 14, 2024 yameyeyuka baada ya Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Rwanda (NEC) kuliondoa jina lake kwenye orodha ya wagombea.
Ni wagombea watatu tu kutoka uchaguzi wa urais wa 2017 waliopatikana kwenye orodha ya muda ya wagombea iliyotolewa na NEC jana Alhamisi, Juni 6, 2024.
Miongoni mwa wagombea hao, yuko Rais Paul Kagame, anayeendelea kutetea nafasi hiyo tangu nchi hiyo ilipotoka kwenye mauaji ya kimbari mwaka 1994.
Wagombea wengine ni Frank Habineza wa Chama cha Kijani na mgombea huru Phillippe Mpayimana.
Uamuzi wa kumwengua Rwigara (42) utakuwa pigo kubwa kwa mwanaharakati huyo ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mfadhili wa zamani wa Chama cha Rwanda Patriotic Front (RPF), Assinapol Rwigara, aliyeuawa katika ajali ya gari iliyoacha utata Februari 2015.
“Natumaini kuwepo kwenye orodha hii wakati huu,” alisema Rwigara Jumanne baada ya kuwasilisha fomu za kuomba uteuzi zikiwa na saini zipatazo 930 zilizokusanywa kutoka wilaya 30 za nchi hiyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Oda Gasinzigwa amesema Rwigara ameshindwa kuwasilisha mahitaji kama vile rekodi ya uhalifu na kulikuwa na kasoro kadhaa kwenye saini zinazomuunga mkono.
Gasinzigwa amesema wagombea walioathiriwa bado wanaweza kuwasilisha nyaraka zinazokosekana ndani ya siku tano za kazi lakini Rwigara hawezi kufikia viwango, kwani mahitaji ya saini yalifungwa Mei 30.
Sio mara ya kwanza kwa Rwigara kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho, kwani hata mwaka 2017, alishindwa kabisa kuingia kwenye orodha baada ya kutuhumiwa kwa kughushi saini za watu waliokufa.
Pia alikumbana na ukatili wa siasa pale picha za utupu zinazodaiwa kuwa zake zilipochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Baadaye alikamatwa pamoja na mama yake, Adeline na dada yake Anne na kushtakiwa kwa kughushi na ukwepaji wa kodi.
Wagombea wengine watano walioondolewa kwenye kinyang’anyiro ni Jean Mbanda, mbunge wa zamani na Fred Barafinda Sekikubo, ambaye kama Rwigara, naye alitupwa nje mwaka 2017.
Wengine walioenguliwa ni walimu wawili Thomas Habimana na Innocent Hakizimana na Herman Manirareba, ambaye maono yake ni kuigeuza Rwanda kuwa ufalme chini ya utawala wake kamili.
Viongozi wawili wa upinzani, Victoire Ingabire na Bernard Ntaganda, ambao wote walikamatwa mwaka 2010 na kufungwa baada ya kujaribu kupinga utawala wa Kagame, walizuiwa mapema kwenye uchaguzi na maamuzi ya Mahakama yaliyopingwa.
Rais Kagame ameitawala Rwanda tangu 1994 baada ya kusimamisha Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi – ingawa kwa miaka tisa ya kwanza alikuwa makamu wa Rais na waziri wa ulinzi, kabla ya kuchukua madaraka kamili mwaka 2003.
Amesifiwa kwa kurejesha utulivu nchini na kuiinua kutoka kwenye majivu ya mauaji ya kikabila hadi kuwa mfano wa uchumi lakini pia anakosolewa kwa kupunguza nafasi ya demokrasia na ukiukwaji wa haki za binadamu.