Diwani abanwa kwa kutotaja mali, madeni yake

Dodoma. Diwani wa Kata ya Cheyo mkoani Tabora, Yusuph Kitumbo amefikishwa Mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwa tuhuma za kushindwa kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni kwa miaka minne huku yeye akijitetea kuwa alikuwa anahudhuria kliniki kwa miaka mitatu mfululizo.

Kitumbo ametoa utetezo huo leo Juni 7, 2024 mbele ya Mwenyekiti wa baraza hilo la maadili, Jaji Mstaafu Rose Teemba.

Kabla ya utetezi huo, Ofisa Uchunguzi Mwandamizi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Magharibi, Tabora, Halima Mnenge amesema Kitumbo amekuwa na tabia ya kuchelewa kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni na kwa miaka minne hakuwasilisha kabisa.

Amesema Kitumbo alichaguliwa kuwa diwani mwaka 2015 kwa kipindi kile alitakiwa arejeshe ndani ya siku 30 lakini hakufanya hivyo, badala yake alirejesha fomu mwaka 2016 kwa kuchelewa.

Mnenge amesema mwaka 2016, ofisi ilimwaandikia barua ikimtaka kurejeshe fomu kwa wakati ikiwa imeambatishwa na fomu ya tamko la rasilimali na madeni, lengo likiwa ni kumkumbusha kuwasilisha tamko kwa mwaka husika.

Amesema pamoja na kukumbushwa huko, bado kiongozi huyo hakurejesha tamko lake kwa wakati na badala yake alilirejea mwaka 2017.

Mnenge amesema kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2019 kiongozi huyo alikuwa anarejesha tamko hilo kwa wakati isipokuwa kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2023 ambapo hakurejesha tamko hilo.

“Kuanzia mwaka 2020 ofisi haikupokea tamko lake na kwa 2021 ofisi pia haikupokea tamko lake,” amesema.

Mnenge amesema kutokana na kutowasilisha kwa miaka mwili, Mei 12, mwaka 22, ofisi yake iliandika barua kwenda kwa Kitumbo ikimtaka awe anawasilisha tamko kwa wakati kwa mwaka unaoishia Desemba 31 mwaka 2021.

“Kipengele cha nne cha barua hiyo kilisema kuwa katika kumbukumbu zetu zinaonyesha kwamba hujawasilisha tamko lako. Kupitia barua hii unatakiwa kuwasilisha utetezi kwa nini umeshindwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya Maadili,” amesema.

Amesema pamoja na barua hiyo kiongozi huyo hakuweza kuwasilisha hayo maelezo ya kwa nini alishindwa kuwasilisha tamko kwa miaka iliyopita.

Amesema walijaribu kumtafuta kwa njia ya simu lakini hakupatikana, pia ofisi ilikwenda Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kujua taarifa zake kama yupo na kuelezwa yupo.

Amesema hatua hiyo iliwafanya kuchukua jukumu la kumpeleka katika Baraza la Maadili.

Mnenge amesema pia Juni 6 mwaka 2023, Sekretarieti ya Maadili ya Umma iliandika barua kwenda kwa Kitumbo iliyohusu tamko la rasilimali na madeni kwa kipindi kilichoishia Desemba 31, 2022.

Mnenge amesema pamoja na barua hiyo, Kitumbo hakutoa utetezi wake wa kwa nini hakurejesha fomu hiyo ya tamko kwa kipindi hicho husika.

Baada ya ushahidi kutolewa, Jaji Mstaafu Teemba alimweleza Kitumbo kuwa ushahidi huo unaonyesha anazo tuhuma za kutowasilisha tamko la rasilimali na mali kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“Sasa tunakupa nafasi ya kujitetea kwa sababu ushahidi unaonyesha unazo tuhuma za kutowasilisha tamko la rasilimali na mali zake,” amesema.

Baada ya hatua hiyo, Kitumbo ameomba apewe muda wa kwenda kuandaa uthibitisho wa utetezi wake kabla ya kuanza kujitetea kwenye baraza hilo.

Kauli hiyo ilimfanya Jaji Mstaafu Teemba kuhoji alipata wapi taarifa ya kuitwa kwenye shauri hilo kama hajajiandaa kujitetea.

Akijibu swali hilo, Kitumbo amesema alipata taarifa kutoka kwa mkewe ambaye alimpigia simu akiwa Bujumbura, Burundi akimweleza kuna barua imekuja anaitwa shaurini Dodoma.

Hata hivyo, baada ya Jaji Mstaafu kumweleza kuwa yeye alikuwa ni mtu wa mwisho kuitwa kwenye mashauri kwa wakati huu, alikubali kujitetea.

Akijitetea, Kitumbo amesema hajawahi kuhudhuria darasa lolote la maadili ya utumishi wa umma na kwa bahati nzuri hiyo ni mara yake ya kwanza kuingia katika utumishi wa umma pindi alipochaguliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2015.

Amesema mara yake ya kwanza kujaza fomu hizo za tamko ilikuwa ni mwaka 2016 ambapo fomu nyingi za tamko kwa madiwani zilipelekwa katika Manispaa ya Tabora na kugawiwa madiwani wote.

Amesema alijaza fomu hizo, na kisha kuwasilisha katika ofisi za madiwani ambao walizichukua na kuzipeleka katika ofisi za sekretarieti Tabora.

Kitumbo amesema kuwa tamko la mwaka 2015 na 2016 aliwasilisha katika sekretarieti hiyo kwa kuchelewa huku mwaka 2017 na 2018 akiwasilisha kwa wakati kupitia ofisi za manispaa.

Hata hivyo, amesema mwaka 2020 hadi mwaka 2023 hakuweza kuwasilisha tamko lake kutokana na changamoto ya kuugua ambayo ilimfanya kulazwa kwa miezi minne na aliporuhusiwa alilazimika kushinda kliniki kila siku.

“Mwaka 2023 sikuwahi kupokea barua yoyote ya maagizo wala maelekezo yoyote kutoka sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma,” amesema.

Baada ya maelezo hayo, Wakili wa Serikali, Fikiri Ngakonda amemhoji kuwa alipata wapi barua ya kutakiwa kwenda katika ofisi ya sekretarieti  ya maadili ya umma kwa ajili kujieleza kwa nini hakutamka mali zake ikiwemo nyumba na kampuni ya ulinzi ya mwaka 2017 kwenye tamko la mali zake.

Akijibu swali hilo, Kitumbo amesema hakupokea barua yoyote bali alielezwa na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Mwaitebele kuwa anahitajika kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya uhakiki wa mali zake.

Hata hivyo, licha ya mawakili wa Serikali, kumbana kuhusu anwani zilizotumika katika mawasiliano yake na sekretarieti hiyo, Kitumbo amekataa akisema anwani zilizotumika hazikuwa za kwake.

Akihitimisha shauri hilo, Jaji Mstaafu Teemba amesema basda aya kusikiliza pande zote mbili, baraza litafanya tathmini na uchunguzi kabla ya kutoa uamuzi kuhusu shauri hilo.

Related Posts