Polisi waendelea kumng’ang’ania Malisa | Mwananchi

Moshi. Wakati Jeshi la Polisi likiendelea kumshikilia Godlisten Malisa, mwanaharakati na mkurugenzi wa GH Foundation katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro, Msemaji wa Taasisi hiyo, James Mbowe amedai kuwa mwanaharakati huyo amepata changamoto za kiafya akiwa kituoni hapo.

 Malisa alikamatwa jana Juni 6, 2024 muda mfupi baada ya kesi inayowakabili yeye na meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Baada ya kukamatwa Malisa alisafirishwa kwenda Moshi na alipofika Saa 3:00 siku aliingizwa kituoni moja kwa moja na kuhojiwa hadi saa 7:00 usiku na mpaka jioni leo alikuwa hajapewa dhamana.

Mwananchi lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoani hapa kwa njia ya simu , Simon Maigwa kuzungumzia suala hilo, amejibu kwa kifupi kuwa yupo kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi na kukata simu.

“Dada yangu nipo kwenye msafara wa Katibu Mkuu wa CCM,” amesema.

Akizungumzia kukamatwa kwa mwanaharakati huyo,  Mbowe amedai Malisa akiwa kituoni hapo amepata changamoto ya kiafya, akipata shida ya kupumua na kulazimika kutumia dawa za kumsaidia kupumua.

“Jana usiku Malisa alipata changamoto ya kiafya akiwa polisi, alipata shida ya kupumua na ikalazimika kuanza kutumia dawa na mpaka leo asubuhi alikuwa akilalamika kupata maumivu ya kifua na hata mchana huu anatumia dawa ambayo inamsaidia kupumua”

Amesema licha ya Malisa kuumwa bado anaendelea kushikiliwa katika kituo hicho na hajapewa dhamana wala kupelekwa mahakamani, licha ya saa 24 kupita tangu akamatwe.

“Malisa alifikishwa Moshi jana saa 3 usiku na kufanyiwa  mahojiano hadi saa 7 usiku, wakimhoji kuhusiana na taarifa aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram Desemba mwaka 2023”

“Taarifa hiyo ilikuwa inahusu Beatrice ambaye alidaiwa kuuawa kwa kuchomwa visu 25 na aliyedaiwa kuwa mpenzi wake, hata baada ya kukamilika kwa hayo mahojiano, Malisa hakupewa dhamana na aliendelea kuwekwa ndani.”

“Tulitarajia leo asubuhi wenzetu wa Polisi, kwa sababu jambo hilo lina muda mrefu kidogo tangu Desemba hadi sasa walipokuja kufanya naye mahojiano, tunaamini upelelezi wa jambo hili ungekuwa umekamilika na hatua stahiki za kumpeleka mahakamani zingefanyika leo lakini mpaka sasa kumekuwa na kucheleweshwa”

Amesema katika uvutaji wa muda, walipata taarifa kuwa kuna askari wanatoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upepepelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya kumhoji.

“Lakini kwa sasa Malisa amefunguliwa jalada jipya likihusiana na kifo cha mwanafunzi aliyedaiwa kufariki kwa kuchapwa na mwalimu na sasa anaendelea kuhojiwa”

“Tumeona si busara kuendelea kukaa kimya maana tangu amekamatwa jana saa 24 zimeshapita lakini hajapelekwa mahakamani na hakuna dalili zozote za kupewa dhamana,” amesema Mbowe.

Akizungumzia kukamatwa kwa Malisa, Pamela Maasay, mbunge mstaafu wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na mwanachama wa taasisi hiyo, amesema suala la kuchelewesha kumpeleka Malisa mahakamani kuna kitu nyuma pazia kwa kuwa saa 24 zilishapita.

“Kama alifanya makosa, hatukatai basi apelekwe mahakamani kwa sababu tunajua kuna taratibu za kisheria, ni kwa nini inachukua saa 24 kumpeleka mahakamani na hapewi fursa ya dhamana?

“Tutaendelea kusimama na Malisa pamoja na wanaharakati wengine ambao watakuwa tayari kumsemea na hatutanyamaza bila kujali mtu anatokea chama gani, au ana imani ipi au mkoa gani, amani yetu tutailinda wenyewe,” amesema Maasay.

Related Posts