SIMBA Queens imekata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) kwa wanawake baada ya leo kuifunga Alliance Girls mabao 3-0, kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu uliokuwa ukishikiliwa na JKT Queens msimu uliopita.
Mabao ya straika Jentrix Shikangwa aliyeweka kambani mara mbili na akifikisha mabao 10 na lile la Ritticia Nabbosa yaliua matumaini ya Alliance kujinasua mkiani ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi na pointi 10.
Simba imechukua ubingwa huo ikisaliwa na mechi mbili kabla ya ligi kumalizika ikiwa raundi ya 16 baada ya kukusanya pointi 46 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote ikiiacha JKT kwa pointi tisa.
Ukiachana na matokeo ya mchezo wa Simba, leo pia ilipigwa michezo minne kwenye viwanja tofauti Yanga Princess ikiifunga bao 1-0 Bunda Queens, JKT ikiitandika mabao 4-0 Fountain Gate Princess na Ceasiaa ikitoka sare ya mabao 2-2 na Baobab Queens, huku Amani Queens ikiififisha matuamaini ya kubaki Ligi Kuu Geita Queens kwa kuitandika bao 1-0.
Simba ambayo imekataa kutoka nafasi ya kwanza imeifanya JKT iendelee kusalia nafasi ya pili na pointi 37, huku Ceasiaa ikibaki nafasi ya tatu na pointi 31 na Yanga ikibaki ‘Top 4’ na pointi 30.
Wekundu wa Msimbazi imechukua ubingwa wa WPL bila ya kufungwa mchezo wowote ikiwa ni timu pekee ambayo haijafungwa na kwenye mechi 16 imeshinda 15 na sare moja ikifunga mabao 50 na kuruhusu saba.
Hili ni kombe la pili kwa Simba kuchukua msimu huu baada ya Desemba 12 mwaka jana kuitoa JKT Queens kwenye fainali ya ngao ya jamii kwa wanawake kwa jumla ya mikwaju ya penati 5-4 dakika 90 zikiisha kwa sare ya 1-1.
Matokeo hayo yanaifanya Simba msimu huu kukata tiketi moja kwa moja ya kushiriki michuano hiyo ambayo msimu wa 2022 ilifuzu baada ya kuchukua Kombe la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na kuishia hatua ya nusu fainali CAF.