Waziri aelekeza wenye kipato duni wapate msaada wa kisheria

Mbeya. Waziri wa Sheria na Katiba, Pindi Chana ameagiza  wasaidizi wa kisheria ngazi za jamii kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi wasio na uwezo ili kutatua changamoto za mirathi, migogoro ya ardhi, ndoa na ukatili wa kijinsia.

Sambamba na hilo, ameagiza taasisi na mashirika ya kidini yanayotoa huduma yasajiliwe na kuingizwa kwenye mifumo ya kidijitali, hali ambayo itaimarisha mahusiano.

Chana amesema leo Ijumaa June 7, 2024 wakati akifungua mafunzo ya  wasajili wasaidia wa msaada kisheria, kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na alitumia jukwaa hilo kusisitiza usimamizi wa haki katika ngazi ya jamii.

“Shukeni chini kwa wananchi kuboresha huduma za misaada ya kisheria na kuweka orodha za taasisi mlizosajili na namba za simu kwenye mbao za matangazo ili ziweze kufikika na wananchi wenye uhitaji,” amesema.

Wakati huohuo amewataka katika kutekeleza majukumu yao kushirikiana na taasisi, mashirika ya dini, viongozi wa ngazi za kata, vitongoji na vijiji ili kupata ushirikiano kwani hao ndio wanaishi na jamii na kutambua changamoto zilizopo.

“Wizara itaendelea kuratibu mifumo ya kuhakikisha jamii inapata msaada wa kisheria kupitia sura na. 31 ya upatikanaji huduma bure, kupitia utaratibu wa ofisi za Tamisemi ngazi ya  wasajili wasaidizi ili kuondoa vikwazo,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi  kitengo cha huduma za msaada wa kisheria wizarani, Ester Msambazi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wasajili wasaidizi  wa kisheria kutekeleza majukumu katika kutoa huduma kwa jamii.

“Kupitia mafunzo ya  siku mbili,  wataangalia changamoto katika  kutekeleza majukumu yao na kuja na njia mbadala ya kutatua vizuizi na kuwasilisha mpango kazi kwa waziri mwenye dhamana  sheria na Katiba,” amesema.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma, Hyness Kajilu amesema lengo la kuelekeza nguvu kwa maofisa maendeleo ya jamii ni baada ya kubaini ni njia sahihi ya kutoa huduma ya msaada kisheria kwa wananchi.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya, Victor Kabuje amesema changamoto kubwa ni jamii kukosa fedha za kuendesha mashauri ya migogoro ya ardhi, mirathi na ukatili.

Amesema kutokana na changamoto hiyo, wamelazimika kubeba jukumu la kuisaidia jamii kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kutatua migogoro hiyo.

Naye mkazi wa Mabatini Jijini hapa, Atupakisye Nassoro amesema jamii inakosa haki kutokana na kutojua sheria, hivyo umefika wakati sasa Serikali ielekeze wasajili wasaidizi wa sheria kushuka kwa wananchi wa chini kutoa elimu hususan ya mirathi, ndoa na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Related Posts