Mama wa mtoto mwenye ualbino aliyeibiwa aliangukia Jeshi la Polisi

Muleba. Judith Richard (20), Mama mzazi wa mtoto mwenye ualbino,  Asimwe Novath (2) aliyeibiwa na watu wasiojulikana akiwa sebuleni kwao Kitongoji cha Mbale Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, ameliomba Jeshi la Polisi kuwabana watuhumiwa linaowashikilia ili waseme mtoto wake alipo.

Mama huyo amedai kuwa miongoni mwa wanaoshikiliwa yupo aliyemchukua mtoto wake siku 10 zilizopita ndani ya nyumba yake.

Katika tukio hilo lililotokea Mei 30, 2024, inadaiwa Asimwe alinyakuliwa na watu wawili saa 1:30 usiku kisha kumpeleka kusikojulikana.

Mpaka sasa tayari watu wanne wanashukiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kumuiba mtoto huyo akiwemo baba yake mzazi, Novath Venant (24)  anayetuhumiwa kuhusika na mpango wa mtoto huyo kuibiwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa maumivu, uchungu na machozi  leo Jumamosi Juni 8, 2024 mama huyo amesema anashindwa afanye nini kwa kuwa haelewi kinachoendelea kwenye uchunguzi wa alipo mtoto wake.

“Sijapatiwa majibu kuhusu kumpata mwanangu inaniuma sana nahisi kufa  hii ni siku ya 10 sipo karibu na Asimwe, waganga wapiga ramli wanaojiita watu wa tiba asili huenda wanahusika naomba Jeshi la Polisi hata kama ni mume wangu amehusika wampe adhabu kali huko alipo  na wote waliohusika na kushikiliwa na polisi mimi ninachohitaji ni kumuona mwanangu inaniuma sana,” amesema Judith.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Yusuph Daniel, amesema wanaendeleza msako na uchunguzi wa kumtafuta mtoto huyo ambaye bado hajapatikana akidai idadi ya watu wanaoshikiliwa na jeshi hilo imeongezeka kutoka watatu kufikia wanne tangu msako uanze Mei 30, mwaka huu.

“Tunaendelea na msako pamoja na  kufanya uchunguzi kwa kila hatua na mbinu zake kuwabaini wahusika waliotekeleza kumpora  mtoto Asimwe na mpaka sasa idadi imeongezeka kutoka watu watatu hadi watu wanne wanaohusishwa na tuhuma za tukio hilo, tutaendelea kutafuta ili kuwabaini  waliohusika hata kama wapo chini ya jiwe,” amesema Kamanda Daniel na kuongeza: “Kwenye mahojiano tunaenda kwa mujibu wa taratibu lakini siyo kwa mifumo ambayo mtu atakuwa anaisema yeye na kauli ya mama inasisitiza kuwa anataka kupata haki yake.’’

Diwani wa kata ya Kamachumu, Lodigard Chonde ambaye pia ni kiongozi wa vikundi vinne vya ulinzi shirikishi kikiwemo cha wawindaji na mbwa vilivyoundwa kuongeza nguvu ya kufanya msako kumtafuta mtoto huyo,  amesema wiki imepita wakimtafuta ila hakuna kilichobainika na leo vikundi hivyo vimefanya kikao ili kuweka mikakati mipya ya kuendelea na msako huo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga amesisitiza kamati ya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Polisi kuhakikisha Asimwe anapatikana akiwa hai au amekufa  ili akabidhiwe mikononi mwa mama yake.

“Tutaendelea kumtafuta huyo mtoto kama yuko hai tutamshukuru Mungu na kama tayari amekufa tunatamani tupate mwili wake na kumkabidhi mama yake amzike na kwa sauti za kulia tutalia na kwa sauti za kuomboleza lazima tuomboleze ila hatuwezi kukubaliana nalo hili,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Nyamahanga amepiga marufuku vibao vinavyoelekeza waganga wa kienyeji (wapiga ramli chonganishi) wanapopatikana akiitaka idara ya Ustawi wa  Jamii kuhakikisha hawatoi vibali kwa watu wanaojihusisha na shughuli hizo za tiba asili kwenye wilaya hiyo mpaka atakapo fanya kikao nao.

Related Posts