PPRA yapewa mbinu udhibiti malipo ya wazabuni

Dodoma. Wabunge wametaka Mfumo Mpya wa Ununuzi wa Umma (NeST), kufungwa moduli inayoonyesha hatua zote za manunuzi hadi malipo.

Pia wameshauri taasisi zitakazoshindwa kuwalipa wakandarasi kufungiwa manunuzi.

Wabunge wameelezwa mfumo huo umeokoa Sh7 bilioni kwenye manunuzi ya umma, ukitarajiwa kuokoa zaidi Sh40 bilioni hadi Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) itakapokabidhi ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwaka huu.

Wakizungumza Juni 8, 2024 wakati wa mafunzo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2023 yaliyoandaliwa na PPRA, wabunge wametaka mfumo huo kuhakikisha unaangalia hadi kwenye malipo ya wazabuni na kuwachukulia hatua wanaochelewesha.

Mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya ameshauri mfumo uzingatie mchakato mzima wa manunuzi hadi mzabuni anapolipwa kwa sababu watu wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya kutolipwa kwa wakati.

Amesema changamoto hiyo inawafanya Watanzania hao kuendelea kuwa masikini.

“Huku ukiwa umembana katika bei kwamba hii ni bei ya soko lakini kwenye kumlipa unamlipa baada ya mwaka,” amesema.

Mbunge wa Masasi Mjini, Godfrey Mwambe amesema mzunguko wa manunuzi wa PPRA haukamiliki kwa kuwa haufuatilii hadi kwenye malipo ya mzabuni.

“Kuna shida. Serikali haiwalipi wakandarasi, serikali hailipi wazabuni na manunuzi yanaonekana yameshafanyika na kwako wewe (PPRA) inaonekana sawa. Nilikuwa natamani mfumo uwe kwenye malipo hadi ya mwisho,” amesema.

Ameshauri taasisi ambayo inaonekana haiwalipi wazabuni ifungiwe hadi ilipe watu wake wa nyuma.

Mwambe amesema kuna hali mbaya mtaani kukiwa na dhana kuwa Serikali ina bei zake tofauti na watu binafsi, hivyo ni vyema PPRA ikaweka bei elekezi ya bidhaa kwenye mfumo ili wazabuni waweze kujipima.

Amesema kuna haja ya Serikali kuweka ukomo katika manunuzi ya bila ushindani  kama ilivyoweka kwenye utaratibu wa manunuzi wa Force account ili kuziba mianya ya matumizi mabaya.

Amesema asilimia 70 ya bajeti ya Serikali inaenda kwenye manunuzi ya umma, hivyo ni vyema Bunge likafikiria kuunda kamati maalumu itayoshughulikia masuala ya manunuzi ya umma.

Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni ametaka Serikali kuacha kuwakopa wakandarasi na kuhakikisha mzabuni anapomaliza zabuni na malipo yake yanakuwa tayari.

Amesema wakandarasi wengine wamekuwa wakimaliza hadi miaka miwili bila kulipwa fedha zao, jambo ambalo siyo zuri kwao.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Eliackim Maswi amesema watakapokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti watashauriana nini cha kufanya kuhusu suala la utaratibu wa single source kwa sababu hata yeye halipendi.

Amesema sababu ya kutolipenda ni kuwa linaweza kuruhusu mwanya wa matumizi mabaya ya fedha za umma kwa watu wanaofahamiana kula njama.

Kuhusu bei elekezi, Maswi amesema mfumo wa manunuzi utakapokamilika wataweka bei elekezi ya bidhaa kwa kila mkoa.

Mchakato wa manunuzi amesema hauishii katika kununua tu bali unakwenda hadi kwenye malipo kama walivyosema wabunge.

“Mfumo huu tutaunganisha hadi kwenye MUSE (Mfumo wa Ulipaji wa Serikali) ili ukishamwambia (mzabuni) kuwa unampa zabuni na fedha uwe umeshaweka, tutaunganisha huko ili tusiendelee kuwatesa,” amesema.

Akizungumzia fedha zilizookolewa kwa mfumo wa NeST, Maswi amesema kwa zabuni mbili tofauti waliokoa Sh7 bilioni na kwamba kwa mwendelezo huo wataokoa zaidi ya Sh40 bilioni hadi wakati watakapowasilisha ripoti kwa Rais Samia.

Akiwasilisha mada kuhusu NeST, Maswi amesema mpaka Juni 8, taasisi 1,147 zimesajiliwa kwenye mfumo huo.

“Kwa taasisi zilizojisajili hakuna zahanati, kituo cha afya, hospitali au shule ya sekondari za umma ambazo ilikuwa tuanze nazo ambazo zimejisajili,” amesema.

Alisema moduli ya mikataba inakwenda kukamilika Julai 30, mwaka huu.

Related Posts