Saini ya hakimu yasababisha kesi ya kulawiti kusikilizwa upya

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dodoma, imetengua hukumu na adhabu ya Mahakama ya Wilaya ya Singida iliyomuhukumu kifungo cha maisha jela aliyekuwa askari wa Jeshi la Polisi, Sajenti David Sangana kutokana na mapungufu ya kisheria.

 Uamuzi huo umefikiwa kutokana na hakimu aliyesikiliza shauri hilo awali, kutotia saini kumbukumbu za mwenendo wa kesi, hivyo imeamuru shauri kurejeshwa Mahakama ya Wilaya ya Singida kuanza kusikilizwa upya.

Sangana, aliyekuwa mkazi wa eneo la Kikosi cha Polisi cha Utemini, Kata ya Ipende mkoani Singida alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Singida, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka tisa.

Anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba 2021 na Machi 18, 2023 katika eneo la Kikosi cha Polisi cha Utemini.

Alikata rufaa iliyosikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma mbele ya Jaji Evaristo Longopa na hukumu kutolewa Juni 5, 2024.

Rufaa hiyo ya jinai namba 3853 ya mwaka 2023, inatokana na kesi ya jinai namba 35/2023 iliyosikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Singida.

Katika rufaa Sangana aliwasilisha hoja saba ambazo zilionekana hazina mashiko isipokuwa ya kushindwa kuzingatiwa matakwa ya kifungu cha 210 (1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinachohusiana na kurekodi ushahidi wa mashahidi mahakamani.

Alieleza kifungu hicho katika mashauri isipokuwa kifungu cha 213, kinaelekeza namna ushahidi wa kila shahidi utakavyotolewa mbele ya hakimu na kuwekwa saini.

“Sheria inatoa hitaji la lazima kwa hakimu wa mahakama kusaini ushahidi uliorekodiwa wa kila shahidi. Matumizi ya maneno ‘itatiwa saini naye’ inaashiria mahitaji ya lazima kwa saini inayoidhinisha juu ya ushuhuda wa mashahidi,” alisema Jaji.

Akirejea mashauri mbalimbali yaliyotolewa maamuzi na Mahakama za Rufani, Jaji ameeleza katika kesi hiyo iliyosikilizwa na mahakimu wawili, Hakimu Mkazi Mkuu U. Swallo alirekodi ushahidi wa shahidi wa kwanza hadi wanne.

Ameeleza iliposikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi E. Luvinga alisikiliza na kuandika ushahidi wa shahidi wa tano hadi wa nane pamoja na mshtakiwa.

Amesema wakati wa kusoma rekodi ushahidi wa shahidi wa kwanza hadi wa nne ulirekodiwa bila kuwa na saini ya hakimu aliyesikiliza.

“Ninafahamu kuwa siyo makosa yote katika shauri yanaathiri mwenendo wa shauri isipokuwa pale ambapo kosa au makosa hayo yamesababisha upotevu wa haki kwa kuzingatia kifungu cha 388 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambacho kinaeleza kunaweza kubatilishwa kwa uamuzi, kukosa kutia saini kwa ushahidi wa kila shahidi ni mojawapo ya makosa,” ameeleza

“Je, nini hatima ya kukata rufaa mbele ya Mahakama hii katika mazingira ya kesi. Nina hakika kuwa kusikizwa upya kwa kesi hiyo kunaonekana kuwa hatua inayokubalika zaidi sababu upande wa mashitaka ulithibitisha kesi yao kwa kiwango kinachohitajika isipokuwa makosa yaliyosababishwa na hakimu kutoweka saini kwenye shauri.”

“Ni rai ya Mahakama hii kwamba makosa hayo kutohusishwa na upande wa mashitaka, ni kwa manufaa ya haki shauri hilo kusikilizwa upya katika Mahakama ya Wilaya. Ninafuta mwenendo wa Mahakama ya Wilaya na kuweka kando hatia na hukumu dhidi ya mrufani. Kesi hiyo imepelekwa katika Mahakama ya Wilaya ya Singida kwa ajili ya kutajwa tena,” amehitimisha hukumu Jaji.

Mrufani aliwakilishwa na mawakili Isaya Nchini na Sarah Makonda, upande wa mashitaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Yusuph Mapesa.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili mahakama ilianza kupitia hoja hizo kabla ya kutolea uamuzi.

Baadhi ya hoja za mrufani ni kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitishwa kosa hilo.

Hata hivyo, mahakama ilisema lilithibitishwa na upande wa mashitaka ikiwa ni pamoja na ushahidi wa mtoto huyo aliyeeleza kunyanyaswa kingoni kwa kulawitiwa na mrufani.

Alieleza katika kesi za jinai Jamhuri wana wajibu wa kuthibitisha makosa pasipo kuacha shaka na kuwa ushahidi uliopo kwenye rekodi unatosha kuthibitisha hatia ya mrufani huyo ikiwemo ushahidi wa daktari aliyemchunguza mtoto.

Related Posts