SIMBA Queens imebeba ubingwa huku msimu wa 2023/24 ukiwa haujamalizika baada ya kuifunga Alliance Girls mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza, jana Ijumaa.
Kwa ubingwa huo wa Ligi Kuu ya Wanawake, Simba imejikatia pia tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake ikiwa ni mara ya pili kwao.
Timu hiyo ilibeba ubingwa raundi ya 16, ikiwa imesalia michezo miwili ikifikisha pointi 46 zisizoweza kufikiwa na JKT Queens yenye 37 na Yanga Princess yenye 30.
Mwanaspoti limekuchambulia baadhi ya mambo yaliyosababisha Simba kurejesha taji ililolipoteza msimu uliopita mbele ya JKT.
Kitendo cha Simba kushinda kila mechi tangu msimu unaanza ilijipa matumaini ya kuchukua ubingwa huo ambao kwa msimu huu iliweka malengo ya kuchukua kutoka kwa wanajeshi wa JKT.
Duru la kwanza ambao kila timu inacheza michezo tisa, Simba ilishinda nane na kutoa sare moja dhidi ya Bunda Queens ya mabao 2-2 ugenini, ikiwamo ushindi wa mezani iliyopewa dhidi ya JKT iliyonyang’anywa pointi tano na kuing’oa kileleni ilipokuwa imejisimika kwa muda mrefyu tangu kuanza kwa msimu huu.
Tangu raundi ya sita mabingwa hao hawajapoteza mchezo wowote hadi sasa. Pia ni ya pili kwa kufunga mabao mengi, 50, bnyuma ya JKT iliyofunga 55 ikichangiwa zaidi na kuzipiga JKT na Yanga Princess.
Msimu uliopita Simba ilimfukuza Kocha Mkuu, Charles Lukula aliyepoteza ubingwa mbele ya JKT na kumua kumleta Juma Mgunda na Mussa Hassan ‘Mgosi’ ambao kwa asilimia kubwa wanalifahamu soka hilo na faida kubwa wote wazawa.
Makocha wote wawili walicheza Simba kwa miaka tofauti lakini pia waliwahi kufundisha timu hizo hivyo kukaa muda mrefu kwenye timu hiyo kuliisaidia kuchukua ubingwa.
Mabingwa hao mara nne wa WPL, msimu huu wamesajili wachezaji wanne pekee wawili wa kigeni na wengine wazawa ili kukiongezea nguvu kikosi hicho.
Ni timu iliyosajili wachezaji wachache tofauti na JKT na Yanga Princess zilizoleta maingizo makubwa.
Kwenye wachezaji wanne wapya, watatu tu ndio wameingia kikosi cha kwanza, Riticia Nabbosa eneo la kiungo, Elizabeth Wambui na Joanitha Ainembabazi winga.
Ukitaja mafanikio ya Simba msimu huu huwezi acha kutaja juhudi za wachezaji wazawa ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho.
Eneo la ulinzi Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na Violeth Nickolaus wamekuwa na mchango mkubwa wa kuzuia mashambulizi eneo lao kwani kwenye mechi 16 imeruhusu mabao saba pekee ikiwa sawa na JKT.
Eneo la washambuliaji pia limekuwa chachu na straika wao, Aisha Mnunka anayeongoza kwenye vita ya wafungaji bora akiweka kambani mabao 18.
Mapema mwanzoni mwa msimu timu hiyo iliweka wazi mipango yao ni kukomba kila kombe litakalokuwa mbele yao ikiwemo la Ngao ya Jamii.
Baada ya kuchukua ngao mbele ya JKT kwa mikwaju ya penati kiu yao kubwa ilikuwa kurudisha ubingwa na uliwafanya kujiamini na kuurudisha wa WPL.
Kadri Ligi inavyozidi kuendelea ndivyo inakuwa na mvuto wa aina yake lakini wanaonegesha hayo ni mashabiki.
Uwepo wa mashabiki uwanjani kujaa uwanjani imekuwa sapoti kubwa na mafanikio kwa timu hiyo kuchukua ubingwa.
Ukiachana na wale waliokuja kuisapoti timu hiyo hapa Dar es Salaam wapo pia waliosafiri kutoka Dar hadi Mwanza kuwashuhudia Simba hao wa kike.
Straika wa timu hiyo, Aisha Mnunka alisema suala la kuchukua ubingwa kumewaongezea kujiamini zaidi baada ya msimu uliopita kupoteza.
“Kama tungepoteza msimu huu tungeumia sana kwa sababu msimu uliopita tulipoteza mechi za mwisho hivyo tumefurahi kuchukua na ligi ya wanaume imeisha tungewaomba mashabiki waendelee kutusapoti.”
Kipa wa Simba, Carolyne Rufa amewapongeza mashabiki wa timu hiyo kutoka Dar hadi Mwanza kuwasapoti jambo lililowapa motisha ya kupambana kwenye mchezo huo.
“Nafurahia kuchukua ubingwa japo msimu uliopita niliumia kutokana na kupoteza kwa pointi moja, kitendo cha mashabiki kuja kuisapoti timu ya kike ni jambo kubwa na ubingwa sio wetu pekee ni wao pia.”