Sugu aililia rasimu Katiba ya Warioba

Mbeya. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, ameshauri namna ya kuunasua mchakato wa Katiba, akitaka rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba irejeshwe ili ipigiwe kura na wananchi.

Sugu amesema hatua hiyo itasaidia kuokoa mabilioni ya fedha yaliyotumika katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambayo haikupatikana.

Mchakato huo ulianzishwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete mwaka 2012 alipounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya maoni ya wananchi na kuandika rasimu ya Katiba.

Rasimu hiyo ilipelekwa katika Bunge Maalum la Katiba na kujadiliwa, lakini baadhi ya vyama vya upinzani vilisusia bunge hilo na kujitoa. Kwa upande wa vyama na wadau wengine waliobaki ikiwemo CCM walitoka na rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Hata hivyo, hatua ya kupiga kura ya maoni haikutekelezwa na mchakato wa Katiba umekuwa ukipigwa danadana.

Mwaka 2023 Serikali ilisema mchakato huo utaanza baada ya miaka mitatu, ili kuwapa elimu wananchi kuhusu Katiba.

Akizungumza leo Jumamosi Juni 8, 2024 kwenye mdahalo wa wazi wa kujadili mchakato mabadiliko  ya katiba ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na kufanyika jijini Mbeya, Sugu aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa  miaka 10, amesema ni vyema mchakato huo ukarejea kwa wananchi ili wapitie na kupiga kura za ndio au hapana.

“Kwa sababu mchakato ulianzia kwa wananchi ni vyema ukarejeshwa tena waupitie kwa umakini na kupiga kura, ikiwa pamoja na kupunguza madaraka ya rais na kuacha vyombo vya maamuzi kama majaji  kutekeleza majukumu yao bila kuingiliwa na hata viongozi wanaoteuliwa wachaguliwe na wananchi,” amesema Sugu.

Amesisitiza: “Tuendelee kudai Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi ili haki itendeke, kwani majaji wanateuliwa na rais na ndio maana wanakwama katika kufanya maamuzi na kusubiri maelekezo.’’

Mbilinyi ametoa mfano yeye ni mwathirika aliyefungwa gerezani na alipokata rufaa kulikuwa na changamoto zilizoashiria kutokuwepo kwa uhuru wa Mahakama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Mbeya (Chawata), Jimmy Ambilikile,  ameomba mchakato wa tume huru na katiba mpya kuangalia kundi hilo  hususan katika mgawanyo wa majibu ili watimize wajibu wao wa kupiga kura.

Naye, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri (KKKT), Stephen Kimondo ameshauri mabadiliko ya  katiba mpya, akitaka wakuu wa wilaya na mikoa wasiteuliwe na rais bali wapigiwe kura na wananchi “Haya ni mapendekezo yangu maana Ma – RC, ma- DC wamekaa kwenye kivuli cha siasa. Ni wakati sasa wachaguliwe na wananchi kwa kupigiwa kura,’’ amesema.

Ameongeza: ‘’Rais awe jukumu la kuteua wakurugenzi wa halmashauri kushika nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya kwani uwezo wanao.’’

Kwa upande wake , mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Deus Kibamba amesema ni wakati sasa wananchi kudai Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi,  ili kuharakisha maendeleo hususan katika makundi mbalimbali.

Related Posts