Taifa Stars ipo tayari kuivaa Zambia

TAIFA Stars jana ilijifua kwa mara ya mwisho katika kujiandaa na mchezo wa tatu wa kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Zambia utakaopigwa Jumanne, huku mastaa karibu wote wakionyesha wanaitaka mechi hiyo itakayopigwa ugenini.

Jana asubuhi kikosi hicho chini ya makocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ na Juma Mgunda kilipiga tizi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya jioni kuhamia kwenye viwanja vya Gymkhana kabla ya asubuhi ya leo kusepa kuifuata Chipolopolo ili kumalizana nayo kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa huko Ndola.

Stars ipo nafasi ya nne katika msimamo wa kundi hilo linaloongozwa na Morocco yenye pointi tatu kama ilizonazo Zambia, Niger na Tanzania zikitofautiana idadi ya mechi ilizocheza na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku Congo Brazzaville ikiburuza mkia baada ya Eritrea kujiondoa mapema.

Hiyo ni mechi ya tatu kwa timu hizo mbili, kwani awali Stars ilianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Niger ikiwa ugenini na kufungwa mabao 2-0 na Morocco Kwa Mkapa, wakati Zambia ilianza na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Congo na kulala 2-1 mbele ya Niger.

Katika mazoezi ya asubuhi ya jana wachezaji wote walioitwa na timu hiyo na waliokosekana kwenye ziara ya Indonesia ilipoenda kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na kumalizika kwa suluhu, walikuwapo ukiondoa nahodha Mbwana Samatta na Novatus Dismas anayetumikia kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mechi dhidi ya Morocco. Wengine ambao hawakuonekana jana asubuhi ni Kibu Denis ambaye awali ilielezwa angeungana na timu ikirudi Dar, Israel Mwenda, Haji Mnoga na Crispian Kachwele waliotajwa kikosini mapema.

Timu hizo zitakutana ikiwa ni miezi kadhaa imepita tangu zilipovaana katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 zilizofanyikia mwaka huu huko Ivory Coast zikiwa kundi F na kutoka 1-1 Januari 21. 

Related Posts