Dodoma. Mbunge wa Masasi Mjini, Godfrey Mwambe amekosoa jina la Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, huku akitadharisha kuachwa mtoto wa kiume katika mipango ya malezi na uwezeshaji.
Amesema hayo leo Juni 8, 2024 katika mafunzo ya wabunge kuhusu uchambuzi wa bajeti kwa kuzingatia masuala ya kijinsia, yaliyoandaliwa na Bunge kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) na UN Women.
Amesema akiwa mtumishi katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kikanda na kimataifa aliwahi kushauri kuhusu urefu wa jina hilo.
“Nikiwa mtumishi Wizara ya Mambo ya Nje mwaka 2015 iliundwa na wizara yenye jina refu, tukakaa, tukasema hakuna haja ya kuwa na maneno mengi kwa kuwa yote ni mambo ya nje, Serikali ilikubali na wakabadilisha jina la wizara,” amesema.
Amesema kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu hata Sera ya Maendeleo ya Jamii imeitwa Sera ya Maendeleo ya Jamii na Wanawake.
“Sasa unajiuliza hao wanawake kwenye jinsia mle hawamo? Wamechomolewa humo ndani, wakatengenezewa maendeleo pekee yao, hao wengine jinsia haitaki maendeleo ni kina nani?”
“Lakini hata wewe waziri sijawahi kukusikia hata mara moja, unakuwa na mpango wa kuwa na vikao na wabunge wanaume kila siku wanawake. Sisi wabunge ndio watunga sera na kinachoonekana dunia inahangaika kuwatoa kina mama ndani kule kwenye familia,” amesema.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wenye dhamana na wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima amesema katika mifumo yote inayotekelezwa kwenye masuala ya jinsia na wanaume wapo.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kusema walienda mbele na wanawake na kuwasahau wanaume, hivyo hawana budi kuwachukua na kuwaingiza katika mipango.
“Hii ndiyo ahadi ya Serikali na imetimia kwenye sera wametambuliwa,” amesema.
Amesema katika kuwafanya watoto wa kiume kuwa baba wazuri kesho, wamewasilisha mara kadhaa na kujibu maswali ya mipango inayotekelezwa.
“Upo mpango wa makuzi ya awali ambao unachukua watoto wenye miaka 0 hadi minane ambao tuliuzindua mwaka 2021. Tumeanza utekelezaji wa programu hii kwenye vituo vya kijamii, vilianza 30 vikaendelea,” amesema.
Dk Gwajima amesema ndani ya vituo hivyo watoto wa jinsi zote wanatengenezwa kujitambua wao ni nani, kujengwa kimaadili, afya, elimu na lishe.
Amesema Serikali haijamsahau mtoto wa kiume kwa kuwa ina mpango mwingine kwa walio na miaka 10 hadi 17 wanaofundishwa kujitambua na kujielewa.
Amesema kuna mabaraza ya watoto yanawashirikisha wa jinsi zote.
Akifungua mafunzo hayo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu aliwataka wabunge watakaporudi majimboni kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwa bado jamii haina elimu kuhusu matumizi ya kuni, gesi na mkaa.
Amesema kilo sita za gesi ni sawa na matumizi ya kilo 30 za mkaa, huku kilo sita za gesi zikiwa ni sawa na kilo 60 za kuni.
“Utaona jinsi ambavyo miti inakatwa katika mapori yetu, nendeni mkaelimishe umma, tumsaidie na kumshika mkono Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha nishati safi inawafikia wananchi,” amesema.
Amewataka kuhakikisha bajeti inakuwa chombo cha kumkomboa mwanamke, akiipongeza Serikali kwa kuwa na miongozo ya bajeti inayozingatia masuala ya kijinsia.
Amesema miongozo ya mwaka 2023/24 na 2024/25 imetoa maelekezo kwa maofisa wanaoandaa bajeti kuzingatia masuala yanayohusu jinsia katika uwasilishaji, uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji, tathimini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa bajeti zao.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa wabunge katika utekelezaji wa majukumu ya msingi hususan katika kupitisha na kusimamia bajeti katika mtizamo wa kijinsia.
“Hivyo ili kwenda sambamba na utekelezaji wa dhana hii yenye mtazamo wa kijinsia, nadhani tutizame pia kanuni zetu kama zinakidhi ipasavyo utekelezaji wa dhana hiyo na kama zina kasoro ziboreshwe ili ziwezeshe wabunge kushauri kuhusu bajeti kwa minajili ya Taifa,” amesema.