Dodoma. Kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania kwa kushirikiana na wabunge wanawake, wamemtunuku tuzo maalumu, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Tuzo hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 9 mjini Dodoma katika siku ya gesi ya kimiminika ya petroli duniani na Spika wa Bunge.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Tulia Ackson aliyekuwa mgeni rasmi amesema kuna kila sababu ya Rais Samia kupatiwa tuzo hiyo.
“Hakuna ubishi, Rais Samia ni kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na juhudi zake zinashuhudiwa na Watanzania, Afrika na dunia kote kwa ujumla,” amesema Dk Tulia.
Amesema hivi sasa katika Bara la Afrika kunachangamoto ya nishati ya kupikia na takwimu zinaonesha asilimia 80 barani humo watu wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia.
Amesema hivi karibuni Rais Samia alipokuwa Dubai kwenye mikutano yake na ule uliofanyika Paris nchini Ufaransa, ametambuliwa na dunia nzima kama kinara wa uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia.
“Hivyo juhudi zake za kuhamasisha hilo zimeanzia hapa nchini, kwa sababu takwimu zinaonesha asilimia 90 ya wananchi mpaka sasa wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia,” amesema.
Spika huyo wa Bunge amesema hakuna asiyefahamu kuwa nishati chafu ya kupikia ina madhara kwa binadamu na kwa hapa nchini, inaonesha vifo takribani 3,3000 hutokea kila mwaka kutokana na athari za kutumia nishati isiyofaa na hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa kwa sababu tu za kutumia nishati chafu.
Amesema mbali ya vifo, lakini kutumia nishati chafu kumekuwa kukisababisha athari mbalimbali za kimazingira na kijamii huku akitumia nafasi hiyo kueleza namna wanawake na mabinti hutumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa badala ya kufanya shughuli za maendeleo.
“Hivyo Rais Samia amedhamiria kuwaondoa wananchi katika changamoto zinazotokana na nishati chafu ya kupikia,” amesema Dk Tulia.
Hivyo, amesema juhudi hizo za Rais Samia zinakwenda kumaliza athari zinazotokea kwa binadamu, lakini pamoja na mazingira kwan sababu hekta zaidi ya 500,000 zinaharibiwa kila mwaka kwa sababu ya kukata kuni na mkaa.
“Katika kufanikisha kampeni ya nishati safi ya kupikia Rais Samia ametafuta wadau mbalimbali. Nimefurahi kuona Oryx wanaungana na wabunge wanawake katika kumuunga mkono Rais katika hatua alizochukua kwenye maeneo mbalimbali ya kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa salama. Leo anapopewa tuzo hii, kwa kweli anastahili kwani unapotazama juhudi anazochukua kuhakikisha wananchi wa Tanzania tunakuwa salama ni kubwa mno,” amesema Spika huyo.
Akitaja baadhi ya mambo yaliyomo katika mkakati huo wa Serikali wa kipindi cha miaka 10 ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya gesi kila mwananchi aweze kumudu gharama sambamba na utolewaji wa ruzuku kwa ajili ya kununua vifaa vya nishati safi pamoja na kupunguza baadhi ya tozo kwa vifaa vya gesi.
“Nawapongeza wabunge kwa hatua wanazochukua za kuishauri Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha juhudi hizi zinazofanywa na taasisi binafsi kama Oryx basi Serikali nayo inaenda huko. Tumesikia Oryx wametoa mitungi zaidi ya 35,000 lakini ni dhahiri kaya tunazo nyingi zaidi ya hizo walizotoa na tungetamani wafike mbali zaidi,” amesema Spika Dk Tulia.
Naye Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman amesema katika kutambua mchango wa Rais Samia katika nishati safi wameamua kutoa tuzo kwa Rais kama sehemu ya kumuunga mkono kwa juhudi anazofanya kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
Amesema mpaka sasa kampuni yake imeshatoa mitungi ya gesi na majiko yake 35,000 kwa makundi mbalimbali nchini na wataendelea na mkakati huo na lengo ni kutaka kuona asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2032 kama Rais anavyosisitiza.
Awali, Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake nchini, Shally Raymond amepongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.