Mtwara. Kitanzi kimemng’ang’ania, ndivyo unaweza kuelezea uamuzi wa Mahakama ya Rufani, kubariki adhabu ya kifo kwa dereva bodaboda, Lucas Wage, aliyemuua dereva bodaboda mwenzake, kuchimba shimo na kisha kumzika.
Tukio hilo la kikatili lililofanywa kwa usiri mkubwa na dereva bodoboda huyo dhidi ya dereva bodaboda mwenzake aitwaye, David Dominick, lilitokea Mei 24, 2019 eneo la Mkalapa Kijiji cha Bondeni katika Wilaya ya Masani, Mkoa wa Mtwara.
Hukumu ya kubariki adhabu ya kifo ilitolewa Juni 5, 2024 na jopo la majaji watatu wa mahakama ya Rufani Tanzania, Rehema Kerefu, Sam Rumanyika, Agnes Mgeyekwa, ambao wamesisitiza adhabu ya kifo aliyopewa ndio anayoistahili.
Ushahidi unaeleza kuwa shahidi wa 2 wa upande wa mashitaka, Augusta Mwambe alikuwa ni mjasiriamali aliyekuwa akimiliki pikipiki aina ya SanLG yenye usajili namba MC 226 BZJ ambayo alikuwa akiitumia kwa biashara ya kubeba abiria.
Mwambe alimkabidhi mshitakiwa pikipiki hiyo ambayo aliitumia kubeba abiria maarufu kama bodaboda kwa makubaliano kuwa atakuwa anamlipa Sh40,000 kwa wiki lakini mambo hayakwenda sawa kwani Wage hakuheshimu makubaliano.
Kwa hiyo, Augusta Mwambe akaamua kumnyang’anya Lucas Wage pikipiki hiyo na kumkabidhi marehemu (Dominick) kwa ajili ya kufanya biashara ile ile ya bodaboda ambapo ufanisi wake ulikuwa mzuri tofauti na ilivyokuwa kwa Lucas.
Dominick alivyotoweka ghafla
Mei 22, 2019 saa 4:00 usiku, Augusta ambaye ni mmiliki wa pikipiki hiyo, alimpigia simu Dominick lakini haikupatikana na siku iliyofuata, mume wa Agusta alimjulisha kuwa hapatikani na anatafutwa.
Siku hiyo Mei 23, 2019, msako ulianza na uliwahusisha madereva bodaboda wenzake lakini bado hakupatikana hadi Mei 24, 2019, mume wa Augusta alimjulisha kuwa mwili wa marehemu umepatikana ila umezikwa.
Wakati Dominick akiendelea kutafutwa, shahidi wa nane, Inspekta wa Polisi, David Mwangawa alijulishwa na shahidi wa tatu, Caspar Chilala kuwa Dominick alionekana kwa mara ya mwisho Mei 22,2019 Saa 2:00 usiku akiwa na mshitakiwa.
Kutokana na taarifa hiyo, mrufani wakati huo akiwa mtuhumiwa, alikamatwa na kuhojiwa na Inspekta Mwangawa na kukiri kuwa kweli alikuwa na Dominick usiku huo kwa kuwa alikuwa amemkodi ampeleke kwa mpenzi wake.
Hata hivyo alimweleza ofisa huyo kuwa waliachana na Dominick baada ya mpenzi wake huyo kukataa kutoka naye, maelezo ambayo aliyatilia shaka kwa kuwa hakuweza kumtaja kwa jina mpenzi wake huyo wala namba yake ya simu.
Kulingana na maelezo ya shahidi wa tatu, Caspar Chilala, usiku huo alipomuona Dominick na mrufani, walikuwa wamesimama pamoja huku mrufani akichezea simu yake na marehemu akiwa ameegemea pikipiki.
Mwili ulivyopatikana umezikwa
Shahidi wa saba, Fadhil Abdalla ambaye ni jirani na mshitakiwa, aliieleza mahakama kuwa usiku wa Mei 22, 2019, mshitakiwa alifika nyumbani kwake na kuomba beleshi ambalo alilirudisha siku inayofuata asubuhi likiwa na udongo mbichi.
Lakini shahidi wa nne, John Benedict yeye alieleza kuwa Mei 24, 2019 wakati wakiendelea kumtafuta Dominick, walifika hadi shemu ya shamba ambalo halijalimwa kwa muda mrefu lakini walishangaa kukuta lina tuta ambalo ni jipya.
Yeye pamoja na watu wengine waliokuwa katika shughuli ya kumtafuta marehemu walifukua eneo hilo ambapo walikuta mwili wa marehemu na uchunguzi wa daktari ulionyesha kiini cha kifo ni kunyongwa kwa waya uliokutwa eneo la tukio.
Pikipiki yakutwa imefukiwa kwa mshitakiwa
Juni 9, 2019 saa 5:00 asubuhi, shahidi wa sita wa Jamhuri alikuta kipande cha karatasi kikiwa kimeingizwa ofisini kwake kikiwa kimeandikwa na mtu aliyejitaja kuwa ni Xaver Mteu, ambaye alisema yeye alipewa kazi ya kupeleka pikipiki kwa mshitakiwa.
Katika karatasi hiyo, alifichua kuwa pikipiki hiyo ilikuwa imefukiwa ardhini ndani ya chumba cha mshitakiwa, aliamua kumjulisha mpelelezi wa kesi ambaye naye alikumbuka kutajiwa jina la Xaver Mteu alipokuwa anamhoji mshitakiwa.
Maofisa wa polisi walikwenda nyumbani na kukuta chumba kimefungwa kwa komeo, walifungua na chini ya kitanda kulikuwa na shimo limefukiwa, walilichimbua na kukuta pikipiki ya Dominick imefukiwa hapo.
Alivyojitetea kujinasua na kitanzi
Katika utetezi wake, ingawa mshitakiwa alikiri kumfahamu marehemu kama dereva bodaboda na mwanakijiji mwenzake na kwamba awali alishawahi kupewa pikipiki na shahidi wa pili ambayo baadaye alipewa marehemu, alikanusha kuua.
Alieleza mahakama kuwa alikamatwa Mei 23, 2019 akihusishwa na mauaji ya dereva bodaboda mwenzake na kwamba mara baada ya kukamatwa, chumba chake kilipekuliwa na polisi lakini hakuna kitu chochote kilipatikana kwake.
Kwa mujibu wa mrufani (mshitakiwa), Juni 9, 2019 hakuhusishwa katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwake nao pikipiki aliyokuwa akiendesha marehemu ilipatikana ila akakiri kuomba beleshi kutoka kwa Jirani yake usiku wa Mei 19.
Hata hivyo, alisema alitumia beleshi hilo kuzuia dimbwi la maji lililokuwepo katika msingi wa nyumba yake kwa kuwa mvua ilikuwa imenyesha siku hiyo na akakiri kuwa shahidi wa tatu ni mpenzi wake na mwanakijiji mwenzake tangu utoto wao.
Lakini alikanusha Ushahidi wa kuonwa naye usiku wa Mei 22, 2019 akiwa na marehemu na kueleza kuwa shahidi huyo alitoa hadithi ya uongo mahakamani kutokana na chuki zilizokuwepo baina yao baada ya yeye kuamua kumuacha.
Baada ya mahakama kusikiliza Ushahidi wa pande mbili, ulimtia hatiani kwa kosa la mauaji ya kukusudia kwa kuegemea kanuni kuwa yeye ndio mtu wa mwisho kuonekana na marehemu na pia maelezo yake ya onyo ya kukiri kutenda kosa.
Hakuridhika, akaamua kukata rufaa akiegemea na moja ya sababu ni kuwa Jaji alikosea kisheria pale alipotilia maanani maelezo yake ya onyo wakati hayakuwepo wakati wa mchakato wa kuihamishia kesi Mahakama Kuu.
Katika hukumu yao, jopo la majaji watatu walitupilia mbali rufaa ya mrufani huyo licha ya kukubaliana naye kuwa maelezo yake ya onyo ya kukiri kosa yalipokelewa kama kielelezo kinyume cha utaratibu kwani hayakuwepo kwenye ‘committal’.
Hata hivyo, majaji hao walisema kwa kuzingatia kuwa mshitakiwa ndio mtu pekee wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu usiku wa Mei 22, 2019 wanaona mahakama ilikuwa sahihi kumtia hatiani kwa kuzingatia kanuni hiyo ya kisheria.
Majaji hao walisema hata alipotakiwa kueleza basi mahali alipo marehemu kwa kuwa ndiye mtu wa mwisho kuwa naye, alishindwa kutoa maelezo na hivyo kushindwa kujitoa katika tuhuma hizo za mauaji ya dereva bodaboda mwenzake.
Kufuatia kanu hiyo, na kwa kuzingatia Ushahidi wa mdomo uliotolewa mahakamani na mashahidi namba 1,2,3,4,6,7 na 8, hitimisho pekee linaloweza kufikiwa na mahakama ni kuwa mshitakiwa ndiye aliyehusina na mauaji hayo.
“Kwa kuangalia ushahidi kwa ujumla wake, hatuna mashaka kabisa kwamba kwa mazingira yaliyopo, mahakama kuu ilikuwa sahihi ilipohitimisha kuwa kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa pasipo kuacha mashaka. Kwa hiyo rufaa inatupwa,”walisema.
Kwa sheria za Tanzania, Mahakama ya Rufani Tanzania ndicho chombo cha mwisho cha rufaa katika kesi za jinai hivyo kwa msimamo huo wa jopo la majaji hao, mshitakiwa huyo ataendelea kuwapo gerezani akisubiri siku ya kunyongwa.