Dar es Salaam. Licha ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupiga marufuku uuzaji wa ardhi kupitia kampuni za madalali zenye mabango katika maeneo mbalimbali nchini, wadau wamesema hatua hiyo haitakuwa muarobaini wa utapeli na migogoro katika sekta ya ardhi.
Marufuku ya uuzaji wa ardhi kupitia kampuni hizo za udalali, imetolewa jana Juni 8, 2024 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa alipokuwa akisikiliza kero za wananchi ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.
Katika marufuku hiyo, Silaa ametaka badala ya kuwepo kwa utitiri wa mabango ya kampuni hizo, yeyote anayetaka kuuza ardhi apeleke taarifa katika Ofisi ya Ardhi ya Halmashauri husika.
“Na wananchi wajue kwamba viwanja katika nchi hii vya watu binafsi na kampuni binafsi vinauzwa ofisi ya ardhi ya wilaya,” amesisitiza huku akitoa siku saba mabango yote yaondolewe.
Msingi wa maelekezo hayo ya Silaa, unatokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi inayosababishwa na uholela katika biashara hiyo.
Ingawa Serikali imependekeza hivyo, wadau wa ardhi wana mtazamo kinzani wakisema marufuku ya mabango hayo haitakuwa muarobaini wa migogoro ya ardhi.
Kwa mujibu wa wadau hao, kukoma kwa migogoro hiyo kutatokana na wananchi kuwa na elimu ya kutosha kuhusu biashara ya ardhi, Serikali idhibiti uholela katika biashara hiyo na ardhi iliyopo irasimishwe.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Haki Ardhi, Cathbert Tomitho amesema badala ya marufuku iliyotolewa na Silaa, alipaswa aje na mfumo bora wa udhibiti wa biashara ya ardhi.
Hoja yake hiyo inatokana na kile alichoeleza, biashara ya rasilimali hiyo kwa sasa inafanyika kiholela na ndiyo sababu ya mianya ya migogoro na utapeli.
“Katazo hilo lingekuwa na mantiki kama lingesimamisha biashara ya ardhi na kusubiri kuwekwa utaratibu wa usimamizi wa biashara hiyo,” amesema.
Katika msisitizo wa hoja yake hiyo, Tomitho amesema haoni katazo hilo likifua dafu, akidokeza kuna uwezekano kampuni hizo zikaacha mabango na kuhamia kufanya biashara hiyo kupitia mitandao ya kijamii.
“Soko la ardhi halijadhibitiwa, kila kampuni inayopima viwanja inauza bei yake, manispaa inanunua bei yake, watu binafsi wananunua kwa bei yao. Kuondoa vibao hakuondoi migogoro,” amesisitiza.
Kilichozungumzwa na waziri huyo kwa mujibu wa Tomitho, ni utashi wake binafsi kwa sababu hata sheria ya ardhi ya mwaka 1999 inaruhusu kupima na kuuza viwanja, akisema nayo iko holela.
“Natamani matamko ya waziri yakabadilishe sera na sheria, kwa kuwa pamoja na nia njema aliyonayo, lakini sheria haimpi nguvu ya kutekeleza anachokitaka,” amesema.
Hata hivyo, amesema kinachowafanya wananchi waendelee kuziamini kampuni hizo za udalali ni hatua yake ya kusikika katika vyombo vinavyoaminika vya habari.
Mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Emmanuel Mchome amesema ili kukabili migogoro ya ardhi inayosababishwa na biashara katika sekta hiyo, ni muhimu kutambua umiliki.
Utambuzi wa umiliki wa ardhi, amesema ufanyike wakati wa upimaji na ramani itakayopatikana inapaswa kubandikwa kwenye ofisi ya kijiji au kitongoji kwa miezi mitatu.
Kwa mujibu wa Dk Mchome, ramani hiyo inapaswa kuwa na majina ya wamiliki wa kila ardhi na ukubwa wa eneo wanalolimiliki.
“Kwa kipindi cha miezi hiyo mitatu, kila mmoja atakwenda kuangalia jina lake na ardhi yake, kama atatokea mwananchi mwenye pingamizi atasema na utawekwa utaratibu wa kusikiliza na kutatua,” amesema.
Ameeleza kuwa hiyo itasaidia kujua wamiliki halali wa maeneo na hivyo kuepusha utapeli na uuzaji holela wa ardhi.
Mbali na mapendekezo yake hayo, amesema kumekuwa na utapeli kwenye biashara ya ardhi na hasa unafanyika kwa watu kuuza maeneo wakati hawayamiliki.
Ameenda mbali zaidi na kueleza wapo waliowahi kulipwa fidia wakati wa utekelezwaji wa miradi ya Serikali, ilhali si wamiliki halali wa maeneo husika.
“Hii iliwahi kutokea Bagamoyo kwenye mradi mmoja hivi, hatimaye wakati Serikali inataka kuanza kutekeleza mradi, mmiliki halali anajitokeza kwa hiyo imechelewesha kazi kuendelea,” amesema.
Kampuni za udalali zinasemaje
Madalali nao wanasisitiza umuhimu wa elimu kuhusu biashara ya ardhi kwa wananchi, kuwa itapunguza migogoro inayojitokeza, badala ya kupiga marufuku mabango pekee kama anavyoeleza Albert Sanane kutoka Kampuni ya EPL property.
Sanane amesema kwa mtazamo wake wananchi wengi wamekosa taarifa sahihi za wapi wauze au wanunue viwanja ndiyo maana migogoro na utapeli hutokea.
“Biashara ya uuzaji viwanja kupitia kampuni inaonekana ngeni miongoni mwa watu wengi, ukiangalia watu walikuwa wamezoea kuuza na kununua kiholela mitaani, sasa hatua ya waziri kupiga marufuku itawashtua watu ni wapi wakanunue viwanja na zile kampuni zenye nia mbaya zitashindwa kutekeleza janjajanja zao,” amesema.
Kwa mtazamo wa Sanane, marufuku ya Silaa itachukua muda mrefu jambo hilo kufanikiwa, lakini litasaidia kupunguza migogoro, huku akipendekeza elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuhusu biashara hiyo.
“Kwa kuwa itapaswa kuuzia halmashauri kuna baadhi ya kampuni ambazo hazijakidhi vigezo hazitakwenda, hivyo ni hatua nzuri, kinachotakiwa kampuni zifuate utaratibu ili mambo yawe yamenyooka,” amesema Sanane.
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa jijini Dar es Salaam, Juma Mwingamno amesema kitendo hicho kitaepusha migogoro ya wawekezaji kwenye ardhi.
“Busara za waziri ni sahihi kwa kuwa kampuni husika inayouza viwanja kwa watu ikienda kufanya jambo hilo chini ya usimamizi wa halmashauri ina maana mwekezaji katika ardhi hiyo atapata sehemu sahihi na ni rahisi kukwepa watu wasio waaminifu,” amesema.
Sambamba na kuunga mkono katazo la Silaa, mwenyekiti huyo amegusia uhalali wa mamlaka ya viongozi wa Serikali za mitaa katika biashara ya ardhi, akisema sheria haiwatambui.
Badala yake, amesema wajibu wa viongozi hao ni kuwatambua wakazi wa maeneo husika.
“Wanachopaswa kujua ni nyumba namba fulani ni ya mtu fulani wanaoishi ni kina nani. Mtu anapokuja kubadilisha umiliki sisi wajibu wetu ni kutoa taarifa kwa anayetakiwa kusimamia taratibu za mauziano.
“Wanasheria au Mahakama kwa sababu hawajui jengo wala wenyewe, hivyo sisi hatuna dhamana ya kusimamia mauzo,” amebainisha.
Ma-RC waeleza sababu za migogoro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema katika eneo analoliongoza migogoro ya ardhi aghalabu husababishwa na uvamizi wa maeneo yaliyotengwa.
“Unakuta mtu amevamia eneo la Serikali ambalo lilitengwa kwa ajili ya shughuli fulani, hapa ndipo migogoro hutokea,” amesema.
Sababu nyingine, amesema ni mtu na mtu kuvuka mpaka uliowekwa na mamlaka wakati inamilikisha ardhi, pia ipo migogoro ya ukoo au familia.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Abas Ahmed Abas amesema kukosekana kwa umilikishwaji ni sababu mojawapo.
“Mtu anaamini anamiliki sehemu lakini kisheria haionekani kama yeye ndiye anayemiliki. Kitendo hiki kinarahisisha tapeli kujitokeza akishajua hilo,” amesema.
Lakini kukosekana kwa elimu, amesema kunasababisha watu wasijue haki zao kwenye ardhi zao na hilo linalosababisha watu wanunue maeneo yasiyostahili.