Dar es Salaam. Wakati msukumo mkubwa wa kielimu uliowekwa kwa watoto wa kike ukitajwa kuwa sababu ya idadi ya wasichana wanaokacha masomo vyuoni kupungua, kutomudu masomo ya kozi walizochagua imetajwa kuwa moja ya sababu za anguko la wengi.
Hayo yamesemwa na wadau wa elimu wakati ambao takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ya mwaka 2023 (TCU) ikionyesha idadi ya wasichana walioacha vyuo imepungua kwa asilimia 42.07, huku wavulana ikiongezeka kwa asilimia 8.51
Kupungua kwa idadi hiyo ya wasichana ndiyo kulikochochea kushuka idadi ya waliokacha masomo mwaka 2022/2023 kwa asilimia 20.52 ikilinganishwa na idadi iliyokuwapo mwaka uliotangulia.
Ripoti ya TCU inaeleza jumla ya wanafunzi 2,839 walikacha masomo mwaka 2022/2023 ikilinganishwa na wanafunzi 3,640 walioacha mwaka uliotangulia.
Kati yao, wasichana walikuwa 1,272 ikiwa ni pungufu ikilinganishwa na 2,196 idadi ya mwaka 2021/22 huku wavulana wakiwa 1,567 kutoka 1,444, mtawaliwa.
Kufeli masomo ni sababu kubwa iliyotajwa na TCU inayowafanya wanafunzi wengi kuacha chuo kwa kuwa ilibeba asilimia 77.6 ya wanafunzi wote mwaka 2022/2023.
Hiyo ikiwa na maana kuwa katika wanafunzi 2,839 waliorekodiwa mwaka huo, 2,205 walifeli na waliofutiwa usajili walikuwa 445, waliofariki dunia 32, huku utoro ukiondoa wanafunzi 157.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumapili Juni 9, 2024, kuhusu idadi ya watoto wa kike wanaoacha vyuo kupungua, Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko, amesema kwa sasa jamii imeona umuhimu wa kuwaendeleza kimasomo na kuweka msukumo kwao kuhakikisha wanabaki shuleni.
Jitihada hizo pia zimewapa hamasa wao na kuwafanya waweze kumudu masomo tofauti na wanaume.
“Wanaume ni tofauti, akifanya biashara kidogo akiona anaweza kumudu maisha anaona bora asiendelee kusoma kwa sababu kunamchelewesha,” amesema Nkoronko.
Hata hivyo, amesema zipo sababu nyingi zinazofanya wanafunzi waache vyuo, ikiwemo za kimfumo na nyingine zikiwa juu yao.
Amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiacha vyuo kwa sababu ya kukosa mahitaji ya msingi, hasa wakiwa hawajapata mikopo na familia kushindwa kumudu gharama.
“Pia baadhi wanaacha chuo kwa sababu wamechagua kozi wasizomudu, anasoma mwaka wa kwanza, wa pili mwisho anashindwa kuendana na kasi ya masomo anaamua kuacha,” amesema Nkoronko.
Pia amesema baadhi ya wanafunzi wanashindwa kuelewa umuhimu wa wao kuwapo chuoni, jambo linawachochea kujiingiza katika shughuli mbalimbali, ikiwemo biashara zinazowafanya wakose muda wa kuhudhuria vipindi, kufanya mitihani ya majaribio na baadhi wanapoona biashara zinafanya vizuri, wanaona chuo hakina maana.
Shayo Massawe ambaye ni mzazi, amesema wakati mwingine kufeli kwa wanafunzi kunachochewa na wazazi kuwalazimisha kusoma kozi fulani kwa sababu ni matamanio yao.
“Unakuta baba anataka mwanaye awe daktari, mwanaye hawezi, lakini kwa sababu baba ametaka anakwenda, matokeo yake ndiyo hayo akisoma baada ya muda anarudi nyumbani kafeli. Umefika wakati sasa wazazi waache watoto wasome kitu anachotaka kwa sababu wanajua soko la ajira linataka nini,” amesema Massawe.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Kristomus amesema wakati mwingine matumizi ya lugha ya kiingereza huweza kuwa sababu ya wanafunzi kufeli masomo yao kutokana na kushindwa kuelewa kinachofundishwa wala yeye kuelewa alichokiandika.
“Kwa miaka mingi kumekuwa na uwezo mdogo wa wanafunzi kumudu lugha ya kiingereza, sasa wanapokuja vyuoni kinatumika kwa asilimia kubwa ikiwemo kujieleza, kufundishia inamfanya anakuwa anasoma haelewi vizuri na kuandika visivyoeleweka anaishia kupata alama za chini ambazo hazimuwezeshi kuendelea,” amesema Kritomus.
Mabadiliko ya ghafla ya mfumo wa maisha pia ni sababu ya wanafunzi wengi kuishia njia, kwa sababu wengi huwa wametoka kidato cha tano na sita na mara nyingi wanakuwa chini ya uangalizi, lakini vyuoni wanapewa uhuru.
Hali za kiuchumi nyumbani kwa wazazi wao, mifarakano katika familia nayo inatajwa na Dk Kristomus kama moja ya sababu inayowafanya baadhi kuacha vyuo.
Kwa mujibu wa Nkoronko, hali hii inaweza kupunguzwa ikiwa wazazi watawaacha wanafunzi wachague kozi wanazoweza kumudu na Serikali ikasimamia vyema uwezeshaji kiuchumi wanafunzi.
“Hili linaweza kuisha ikiwa wanafunzi wataweza kujifanyia tathmini kwa kuchagua kozi wanazoweza kusoma, hii itawafanya kusoma anachoweza kumudu,” amesema Nkoronko na kuongeza; “Pia ugharamiaji wa elimu, Bodi ya Mikopo ifanye juhudi za makusudi kwa watoto wenye mahitaji ambao familia zao haziwezi kumudu maisha.”
Katika hili, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) tayari imefungua dirisha la uombaji mikopo litakalokuwa wazi kwa siku 90 ambalo limeenda sambamba na kutenga Sh787 bilioni kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi 250,000.