Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema maafa yakitokea yanarudisha nyuma uwezo wa Serikali kuwahudumia wananchi, hivyo ushiriki wa taasisi za kijamii ni muhimu katika kuisaidia kulinda ustawi wa maisha ya raia na maendeleo kwa ujumla.
Amesema kwa kutambua hilo Serikali ina maono kupitia sheria namba sita (6) ya maafa ya mwaka 2012 inayolenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa vifaa vya kisasa vya uokoaji na mafunzo kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kukabiliana na majanga yanapojitokeza.
Waziri Mhagama amebainisha hayo leo Juni 9, 2024 Dar es Salaam kwenye hafla ya kuzindua mafunzo ya wiki mbili ya pamoja ya ukoaji kwenye maji kwa vikosi vya Jeshi la Polisi kitengo cha wanamaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na vikundi ngazi ya jamii na ugawaji wa vifaa vya uokoaji.
“Maafa ni mtambuka, yanagusa jamii moja kwa moja, ushiriki wa taasisi za kijamii ni jambo la msingi na serikali imetoa fursa taasisi zisizo za kiraia kushirikiana nasi kuleta maendeleo kupitia 4R za Rais Samia Suluhu Hassan na wadau wameanza kujitokeza,” amesema Mhagama.
Amesema maafa yanayojitokeza nchini yanasababishwa na majanga ya asili na mengine hutokana na shughuli za kibinadamu na yamekuwa yakiathiri maisha ya watu ikiwemo kupoteza maisha na mali zao.
“Majanga yapotokea inafikia hatua yanarudisha nyuma uwezo wa serikali kuwahudumia wananchi wake na uchumi wa mtu mmoja mmoja na Serikali umekuwa ukiathirika,” amesema waziri huyo.
Mhagama ametumia fursa hiyo kuipongeza taasisi ya Sukos Kova Faondation na Peaceland Foundation kwa kutoa kutoa mafunzo hayo na kutoa boti moja ya kisasa kwa serikali itakayosaidia shughuli za ukoaji majanga yanapojitokeza.
“Boti hii itasaidia hata kukabiliana na matukio ya uhalifu majini, mwaka 2023 Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya walikamata shehena dawa za kulevya zaidi ya mara tatu ya dawa zilizokamatwa kipindi cha miaka 11 iliyopita,” amesema.
Akizungumzia uwezo wa boti hiyo, Mkurugenzi wa taasisi ya Sukos, Suleiman Kova amesema ni boti ya kisasa, haiwezi kuzama hata kukiwa na maji kidogo inaelea juu.
“Ina uwezo wa kubeba abiria 13 wakati mmoja, ina uwezo wa kwenda sehemu yoyote baharini, ziwani, mtoni hata kwenye mafuriko na unaweza kuitoa upepo na kuipeleka unakotoka,” amesema.
Amesema ina uwezo wa kuwa na mwendeshaji mmoja na waokoaji wawili na zina nguvu na injini yake ni horse power 30, thamani yake moja ni Sh15 milioni.
“Kama taasisi tunazo boti kama hizi tatu na wataalamu wa kutosha, tupo tayari kushiriki uokoaji matukio ya majanga yakitokea, Serikali itualike,” amesema.
Mkuu wa polisi kitengo cha wanamaji Dar es Salaam, Daniel Mwakibete amesema boti hizo ni nzuri na itakuwa rahisi kwao katika shughuli za uokozi sehemu zenye maji madogo na mengi.
“Polisi kama walinzi wa rasilimali bahari tukiwa na boti kama hizi ni rahisi katika kukabiliana na wahalifu, kwa kuwa tumekuwa tukipata shida kuwakamata kwa kukimbilia sehemu zenye maji madogo hasa kwenye mikoko na kushindwa kuwakamata,” amesema Mwakibete.