Rita yabaini ubadhirifu Sh1 bilioni Msikiti wa Ijumaa Mwanza

Mwanza. Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (Rita), imebaini ubadhirifu wa kiasi cha Sh1 bilioni katika Msikiti wa Ijumaa uliopo jijini Mwanza na hatua za kisheria zimeshaaza kuchukuliwa.

Hayo yamesemwa na leo Jumapili Juni 9, 2024 na Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Frank Kanyusi.

Amewaambia waumini wa msikiti huo kuwa ziara yake imelenga kuwasilisha ripoti ya ubadhirifu wa fedha kwa waumini sambamba na kusimamia uchaguzi wa wasimamizi watakaosimamia kwa muda mali za waumini wa msikiti huo.

“Rai yangu kwa wajumbe wa Bodi  ya Udhamini muhakikishe mnatekeleza majukumu yenu kama sheria inavyowaelekeza au kuwataka na waelewe kuwa wao siyo wamiliki wa mali, bali ni wasimamizi kwa niaba ya wanachama,  hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuzuia vitendo visivyofaa,” amesema Kanyusi.

Kwa mujibu wa Kabidhi Wasii Mkuu huyo, Februari 2, mwaka huu, aliunda kamati ya uchunguzi ambayo ilifanya kazi kwa mwezi mmoja na ikaja na ripoti iliyoonyesha ubadhirifu wa fedha takribani Sh1 bilioni za msikiti huo.

Hata hivyo, amesema tayari hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa na wale wote watakaobainika watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

“Rita inawatoa hofu waumini wote wa msikiti huu, mali zenu zipo kwenye mikono salama,” amesema Kanyusi.

Kufuatia ubadhirifu na mivutano miongoni mwa baadhi ya waumini, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma ilielekeza iundwe kamati ya wasimamizi kabla ya Juni 20 mwaka huu, itakayosimamia mali zote za waumini wa Msikiti wa Ijumaa Mwanza.

Ofisa Sheria wa Rita, Emmanuela Mwingira amesema Rita imeshafanyia kazi marekebisho ya Katiba na imewachagua waumini kadhaa wa msikiti huo watakaofanya uchaguzi ili kupata bodi ya wadhamini.

“Kazi tuliyokuwa nayo ni pamoja na kupitia sheria yao na kufanya maboresho ili kuzuia makosa kutojirudia siku za mbeleni,” amesemai Mwingira.

Hata hivyo amepongeza utulivu na ushirikiano uliotolewa wakati wote wa kikao na waumini wa msikiti.

Muumini wa msikiti huo, Sherally Sherally amesema sheria isipofuatwa haki haitopatikana, ameiomba Rita kuhakikisha wale wote waliohusika na ubadhirifu huo wanachukuliwa hatua stahihiki ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

“Tukiendelea kuwachekea watu wanaojilimbikizia mali za waumini hatutafika mbali, kwa sababu hata hawa tutakaowachagua kama watabaini hatua hazikuchukuliwa kuna hatari baadhi yao pia wakafanya kama hiki tunachokilalamikia,” amesema Sherally. 

Muumini mwingine, Abdallah Tawafique mbali na kuipongeza Rita kwa hatua iliyochukua, ameishukukuru kwa kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa taasisi zote za dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini.

Bodi ya kwanza ya udhamini ya msikiti huo ilivunjwa na serikali mwaka 2020 na baadaye kuundwa kwa kamati ya mpito ya wajumbe 13 ambayo nayo imevunjwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma kufuatia mvutano wa baadhi ya waumini uliokuwa unaendelea.

Related Posts