Straika wa mabao yupo yupo tu

BAADA ya kupandisha timu Ligi Kuu na kuibuka mfungaji bora winga wa Ken Gold, William Edgar amesema bado hajajua hatma yake kubaki au kuondoka kikosini humo msimu ujao.

Nyota huyo aliandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza aliyefunga idadi kubwa ya mabao (21) lakini ikiwa mara ya pili kupandisha timu Ligi Kuu, akifanya hivyo 2021/22 kwa Mbeya Kwanza.

Hata hivyo, kwa misimu minne nyuma, nyota huyo amekuwa katika kiwango bora akifunga mabao mengi kuwa kwenye vita ya kuwania kiatu cha mfungaji bora japokuwa alizidiwa na wapinzani.

Katika msimu wa 2021/22, Edgar alitupia mabao 15 akizidiwa na straika wa JKT Tanzania, Edward Songo aliyemaliza msimu kwa mabao 18 na kuipandisha timu yake Ligi Kuu.

Edgar aliliambia Mwanaspoti kuwa mpira ndio kazi yake hivyo hawezi kuweka wazi wapi atakuwa msimu ujao, licha ya kwamba anaipa zaidi nafasi Ken Gold.

Alisema kilichompa ufanisi katika ligi hiyo ni kutokana na ushirikiano ndani na nje ya uwanja, lakini kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ndio ilikuwa silaha kwake.

“Hii ni kazi yangu, nitaangalia masilahi japokuwa naipa nafasi kubwa timu yangu niliyoipandisha, nilijituma na kushirikiana na wenzangu, lakini zaidi kufuata maelekezo ya kocha† alisema Edgar.

Nyota huyo aliongeza kuwa haikuwa kazi rahisi kuweza kufikia malengo kutokana na upinzani wa ligi ulivyokuwa kwa timu zilivyokuwa zimejipanga haswa kwenye nafasi nne za juu.

Alisema wanapoenda Ligi Kuu lazima wajipange vizuri kuweza kuhimili mikiki ya wapinzani ili kuweza kubaki kwa muda mrefu akiwaomba wenzake kujiandaa kiushindani.

“Haikuwa kazi rahisi, timu zilijipanga haswa zile za nafasi nne juu, kwa ujumla tunajipongeza na kuwashukuru wadau kwa sapoti yao na tutajipanga Ligi Kuu tuweze kufanya vizuri† alisema staa huyo.

Related Posts