Gaza. Ikiwa leo ni siku ya 247 tangu kuanza kwa mapigano kati ya Jeshi la Israel na wapiganaji wa kundi la Hamas kutoka Palestina, taarifa kutoka eneo la mapigano zinasema hadi sasa vifo vimefikia 37,084.
Shirika la Habari la AFP limeinukuu Wizara ya Afya ya Gaza ikisema leo Jumapili Juni 9, 2024 kwamba vifo hivyo vimetokea katika eneo hilo ikiwa ni zaidi ya miezi nane ya vita kati ya Israel na Hamas.
Hata hivyo, wizara imesema watu wengine 84,494 wamejeruhiwa katika vita hivyo tangu vilipozuka Oktoba 7, 2023 baada ya uvamizi wa Hamas.
Idadi hiyo imepaa kutokana na vifo 274 vilivyotokana na uvamizi wa Israel wa Jumamosi iliyopita kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat ambapo mateka wanne waliokolewa wakiwa hai.
Operesheni ya Israel kuokoa mateka
Katika operesheni ya kuwaokoa mateka hao, wizara hiyo ya afya inayoendeshwa na Hamas, imesema watu 274 waliuawa katika kile ilichokiita ‘mauaji ya Nuseirat’, ikisahihisha idadi ya awali ya 210 kutoka ofisi ya serikali ya vyombo vya habari ambayo ilisema vifo hivyo ni pamoja na wanawake na watoto wengi.

Katika operesheni ya kuwaokoa mateka wanne ambao ni Noa Argamani (26), Almog Meir Jan (22), Andrey Kozlov (27) na Shlomi Ziv (41) wameokolewa wakiwa wazima.
Wanne hao walikuwa wametekwa nyara kutoka kwenye tamasha la muziki la Nova wakati wa shambulizi la Hamas, Oktoba 7, 2023.
Rais wa Marekani, Joe Biden, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ni miongoni mwa viongozi waliotoa salamu za kuachiliwa kwao huku wakitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano.
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell alikaribisha kuachiliwa kwa mateka na kusema “Ripoti za mauaji mengine ya raia ni ya kutisha…umwagaji damu lazima ukome mara moja”.
Wakati hayo yakiendelea, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amenukuliwa na Vatcan News akitoa wito wa msaada wa haraka kwa Gaza na kuhimiza juhudi za amani.
Papa Francis ametoa wito kwa mataifa kuchukua hatua za haraka kusaidia watu wa Gaza na misaada ya kibinadamu ambayo inahitajika kwa kiwango kikubwa.
Amehimiza juhudi za amani katika mkutano wa kilele ulioandaliwa na Jordan utakaofanyika wiki ijayo ambapo Jordan itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa unaoangazia dharura ya kibinadamu huko Gaza.
Katika sala ya Malaika ya Jumapili, Papa Francis ametoa wito kwa mkutano huo ulioitishwa na Mfalme wa Jordan, Rais wa Misri na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huku akiwashukuru kwa mpango huo muhimu.
Papa amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kutumia njia zote zinazowezekana kuwasaidia watu wa Gaza waliopo katikati ya vita huku akitaka misaada ya kibinadamu iwafikie haraka wale wanaohitaji na kwamba hakuna mtu anayepaswa kuizuia kufika.
Vilevile, Papa amehimiza mazungumzo yanayoendelea kati ya wale wanaohusika ingawa si rahisi huku akielezea matumaini kwamba mapendekezo ya amani, usitishaji wa mapigano katika nyanja zote na kuachiliwa kwa mateka, itakubaliwa mara moja kwa manufaa ya Wapalestina na Waisraeli.
Papa anatoa wito kwa Israel na Hamas kukubali mara moja makubaliano ya kusitisha mapigano mateka.