ACT Wazalendo: CCM wamepoteza misingi wajiandae kutupisha, wenyewe wajibu

Unguja. Chama Cha ACT Wazalendo kimesema kimejipanga kushika dola mwaka 2025 kwani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza misingi ya ilani ya ASP iliyoasisiwa na  Hayati Abeid Aman Karume. 

Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa jana Juni 9, 2024 katika mwendelezo wa mikutano ya chama hicho maarufu ‘bandika bandua’ katika viwanja vya Kilimahewa Unguja. 

Alisema ilani ya uchaguzi ya mwaka 1961 ya ASP, Karume alisema: “Uhuru ndio msingi wa chama chetu unachanganya bila shaka kumalizika kwa Serikali ya kikoloni na mwisho wa utawala wa nje.” 

Huku akinukuu katiba ya Zanzibar, alisema bado yaliyopingwa katika ilani hiyo yanaendelea kushuhudiwa katika utawala ulipo sasa.

“Katiba ya Zanzibar ibara ya 10 (h) inasema vyeo vyote na madaraka ni dhamana na vipo kwa manufaa ya umma na wale wote walio na madaraka watawajibika ama moja kwa moja kwa umma au kwa vyombo vya uwakilishi,” alisema.

 Hata hivyo alisema watawala hawawajibiki kwa hiyo kinachofanywa na ACT ni kusimamia Katiba ya Zanzibar.

Akiendelea kunukuu Katiba alisema, ‘katiba ya Zanzibar ibara ya 23 (2), (3) na (4) inaeleza kuwa kila mtu ana wajibu wa kulinda mali ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi na pia kuheshimu mali ya mtu mwingine, pia watu wote watatakiwa kulinda mali ya Zanzibar na kwa pamoja kupiga vita aina zote za uharibifu na kuendesha uchumi wa Zanzibar kwa umakini’.

“Hayo yote hayasimamiwi na ndio maana chama chetu kinataka mamlaka kamili ili kusimamia haki za wananchi wa Zanzibar.”

“Kwa hiyo sisi tunaposimama hapa tunatekeleza wajibu wetu wa kikatiba, na tunasema haya kuiwajibisha Serikali, jambo jema ni kwamba viongozi wenu tumejipanga safari ambayo tuliianza na  mzee wetu hayati Maalim tukauawa, tukaumizwa na  wengine wamepata vilema vya maisha tunakwenda kuhitimisha Oktoba 2025,” alisema Jussa. 

Alisema kwa sasa wazanzibari wanajitambua na hawadanganyiki tena na hawawezi kukubali kupoteza haki zao. 

Alisema kama kuna mtu wa kukumbukwa katika Taifa la Zanzibar ni Karume kwani alijenga majengo makubwa kila kona tena kwa muda mfupi bila mikopo, lakini kwa sasa nchi imeingia kwenye madeni makubwa kwa ajili ya masilahi binafsi. 

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma alisema deni la Taifa limefikia Sh1 trilioni. 

Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Mansour Yussuf Himid alisema nchi haiwezi kufikia malengo yake ikiwa kuna matabaka jambo ambalo alilipinga hayati Maalim Seif. 

“Maalim alisema na alitaka kuwa na usawa kwa kila mwananchi, hatuwezi kufika popote iwapo tukiendelea kuwa na matabaka na watu kugawanywa, aliamini  kuwa nchi hii lazima iwe na usawa na haiwezi  kufikia maendeleo ikiwa  watu wake wamegawanyika.” 

“Hatuamini kwamba mzee Karume alipindua nchi hii kwa ajili ya kuwatenga Wazanzibari na kunyimwa mambo wanayotaka, lakini alipindua kuleta usawa na kuondoa ubaguzi,” alisema Himid. 

Alisema kwa sababu ya kukosa misingi imara ya uongozi kwenye chama hicho CCM wameamua kuwawekea chuki wale wote wasiokiunga mkono  kwa kuwakosesha haki za msingi zikiwemo za kupata vitambulisho pamoja na nafasi za ajira.

“Hii ni dalili mbaya sana ukiona kiongozi anaogopwa kusemwa maana yake hana uadilifu na lazima wajue wazee wetu wamepindua ili tuishi kwa upendo na mshikamano sio wanayotufanya wao,”alisema Himid.
Akizungumzia madai ya ACT Wazalendo, Katibu wa Kamati Maalumu, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto alisema hawatishwi na maneno hayo aliyoyaita ya wakosaji.

“Kama kuna wakati CCM imetekeleza ilani yake kwa kiasi kikubwa ni katika utawala wa awamu ya nane, hayo maneno ni ya wakosaji na hayatutishi,”alisema Mbeto.
 

Related Posts