Johannesburg. Bunge jipya la Afrika Kusini lililochaguliwa Mei 29, 2024 litakutana kwa mara ya kwanza Ijumaa ya Juni 14, 2024, wakati vyama vya siasa vikivutana kuhusu kuunda muungano baada ya uchaguzi mkuu uliopita kutotoa mshindi wa moja kwa moja.
Wabunge katika Bunge la Kitaifa lenye viti 400 wataitwa kuteua Spika na kuanza mchakato wa kumchagua Rais wa nchi hiyo, kazi inayoweza kuwa ngumu kuliko kawaida mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa demokrasia mwaka 1994, chama cha African National Congress (ANC) cha Rais Cyril Ramaphosa kimepoteza idadi kubwa ya wabunge katika uchaguzi uliofanyika Mei 29.
Chama hicho kinara wa kupinga ubaguzi wa rangi, kilipata asilimia 40 ya kura, kikiwa ni kiwango cha chini kuwahi kutokea na sasa kinahitaji kuungwa mkono na vyama vingine, ili kutawala.
“Kikao cha kwanza cha Bunge kitakuwa Ijumaa, Juni 14, 2024,” Jaji Mkuu, Raymond Zondo ameandika katika agizo lililotolewa leo Jumatatu Juni 10, 2024 kwenye vyombo vya habari na Wizara ya Sheria.
Chama cha ANC tayari kimedokeza kinataka kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kundi pana la vyama vya upinzani, kuanzia mrengo wa kulia hadi mrengo mkali wa kushoto.
Pendekezo hilo limepokelewa vizuri na baadhi ya watu wiki iliyopita ambapo chama chenye siasa kali za mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF) awali kilipuuza wazo la kuungana na wapinzani wenye mitazamo tofauti ya kisiasa, kama vile chama cha mrengo wa kati cha Democratic Alliance (DA).
Lakini mazungumzo yaliendelea mwishoni mwa wiki na viongozi wakuu wa baadhi ya vyama, ikiwa ni pamoja na DA, walifanya majadiliano ya ndani leo Jumatatu, ili kuamua njia ya kusonga mbele.
Wakati huohuo, chama cha Rais wa zamani, Jacob Zuma cha Umkhonto weSizwe (MK) ambacho kilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo, kikishinda asilimia 14.6 ya kura na viti 58, kimesema kinakusudia kuwasilisha rufaa mahakamani kuzuia Bunge jipya kuitishwa, ili kusubiri malalamiko tofauti kuhusu madai ya kasoro za uchaguzi kusikilizwa.
ANC itakuwa na wajumbe 159 katika Bunge la Kitaifa kutoka 230 mwaka 2019. DA ilishinda viti 87 kikiwa na ajenda ya soko huria.
EFF ilipata wabunge 39 na inaunga mkono ugawaji upya wa ardhi na kutaifishwa kwa sekta muhimu za kiuchumi.