Dar es Salaam. Jeshi la Magereza limeingia makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kwa ajili ya mauziano ya nishati safi ya kupikia ambayo ni mkaa mbadala unaozalishwa na shirika hilo.
Makubaliano hayo yamesainiwa mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Mzee Ramadhan Nyamka pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse.
Aidha, Stamico imeingia mkataba wa ushirikiano na jeshi hilo kwa ajili ya kuendeleza utafiti na uchimbaji wa maeneo yenye leseni ya uchimbaji madini.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Dk Mwasse mbali na kuwashukuru magereza kwa mwitikio wao wa kutumia nishati hiyo safi ya kupikia, amewaahidi kutekeleza makubaliano hayo kwa asilimia 100.
Amesema kutokana na uwekezaji uliopo, Stamico wanawahakikishia upatikanaji wa nishati hiyo mbadala kwa muda wote.
“Uzalishaji utakuwepo mkubwa, kwani mwisho wa mwezi huu tunakwenda kukamilisha ujenzi wa viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa. Kiwanda kimoja kipo Kisarawe mkoani Pwani na kingine kipo Kiwira mkoani Mbeya.
“Pia katika Bandari ya Dar es Salaam, yametua makontena 14 yenye urefu wa futi 40 ambapo ndani yake kuna mitambo ya uzalishaji wa mkaa huu ambayo itakwenda kufungwa mkoani Dodoma na Tabora. Pia mitambo hii itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa,” amesema.
Kuhusu mkataba wa uchimbaji madini, Dk Mwasse amesema Stamico ambayo ina uzoefu wa zaidi ya miaka 50 kwenye tasnia ya madini, wanakwenda kuunda kikosi kazi katika kutekeleza makubaliano ya mkataba huo ambao ni utafiti na uchimbaji wa madini, hasa ikizingatiwa shirika hilo lina wafanyakazi wa kutosha wenye uzoefu katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza amesema utiaji saini baina ya taasisi hizo ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia aliyoyatoa Mei 8, 2024 wakati akizindua mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, akitaka taasisi zote zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa siku, zianze kutumia nishati safi ya kupikia.
“Leo nimekabidhiwa mkaa rafiki unaotokana na masalia ya madini, mkaa huu utatufanya tuondokane na matumizi ya kuni na mkaa, hivyo na sisi Magereza tutakuwa tumechangia uhifadhi na utunzaji wa mazingira yetu, hasa ikizingatiwa tumeambiwa ipo akiba ya kutosha ya mkaa huu katika kutumika kulisha magereza yote nchini kwa miaka mingi ijayo,” amesema.
Amesema jeshi hilo lina magereza 129 yenye uwezo wa kuhifadhi wafungwa 29,902 kwa siku nchini na wafungwa hao huhitaji huduma za malazi, chakula na matibabu.
Amesema chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwenye magereza ni kuni na mkaa, hivyo kwa siku magereza hayo hutumia kuni zenye ujazo wa mita91,591.25 kwa ajili ya kupikia.
“Ukiangalia tasfiri yake ni miti mingi sana inabidi ikatwe kwa siku, ili kuwezesha kuwapikia wafungwa chakula. Sasa tunakwenda kuondokana na uharibifu wa mazingira kupitia makubaliano haya.
“Pia ndani ya Magereza tunakwenda kupata faida ya kulinda afya za wapishi ambao ni wafungwa na askari wanaosimamia kutokana na moshi uliokuwa unatokana na kuni na mkaa,” amesema.
Aidha, kuhusu utafiti na uchimbaji wa madini, amesema baadhi ya maeneo yamefanyiwa utafiti na kuonekana kuna madini mbalimbali, hivyo ushirikiano huo wa Stamico na Magereza utatumika kuimarisha uchimbaji endelevu kwa masilahi ya Watanzania.