Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Miundombinu katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila amewaagiza wahandisi washauri wanaosimamia miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara nchini kusimamia kwa ukaribu miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Mhandisi Mativila ameyasema hayo leo tarehe 10 Juni 2024 wakati akikagua ujenzi wa jengo la ofisi la wahandisi katika manispaa ya Tabora ambalo lipo chini ya mradi wa TACTIC unaosimamiwa na TARURA.
“Rais Samia Suluhu Hassan anahangaika kutafuta fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata barabara, wataalam lazima mbadilike na kusimamia kwa ukaribu ujenzi wa miradi hii. Mkandarasi huyu angekuwa anasimamiwa kwa ukaribu angeshakuwa amemaliza hapa,” amesema.
Hata hivyo, Mhandisi Mativila amewataka wataalam hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa ujenzi ili wakandarasi wakamilishe kazi kwa wakati.
Aidha, amemtaka Mhandisi Mshauri UNITEC Civil Consultants Ltd. kuhakikisha anasimamia kwa karibu ujenzi huo na ifikapo Agosti mwaka huu jengo hilo liwe limekamilika.
Ujenzi wa jengo la ofisi la wahandisi linalogharimu takribani Sh 800 milioni lilianza ujenzi wake Novemba 2023 na lilitarajiwa kukamilika 15 Juni 2024.
Hata hivyo, ameagiza ujenzi huo unaotekelezwa na mkandarasi CICO Contractor, ukamilika ifikapo Agosti 2024.