Morogoro. Wakati Jeshi la Polisi mkoani Morogoro likiendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Signal, Christian Tungaraza, mdogo wa marehemu, Clavery Tungaraza amesema mara ya mwisho kaka yake alimtumia picha yake na kumwelekeza kwamba itumike kwenye mazishi yake atakapokuwa amekufa.
Clavery amebainisha kwamba hadi sasa hafahamu mauaji hayo yametokana na nini kwa kuwa marehemu kaka yake hakuwahi kumueleza kama alikuwa na mgogoro au ugomvi na mtu yeyote.
Wakati uchunguzi huo ukiendelea, mke wa mwalimu wake Jovina Mwakiyee (33), mkazi wa Kijiji cha Mang’ula A, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kula njama na kumuua mume wake.
Akizungumzia na Mwananchi Digital, mdogo wa marehemu amesema alipata taarifa za mauaji ya kaka yake Juni Mosi, 2024 usiku kutoka kwa shemeji yake (Jovina) ambapo alielezwa kuwa walivamiwa usiku huo na watu wasiojulikana na kuanza kumshambulia kaka yake.
“Baada ya kupata taarifa hizo nikiwa nyumbani Simiyu, nilianza kuwasiliana na ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa karibu na kaka huku Morogoro na ilipofika asubuhi tukapata taarifa kuwa kaka amefariki akiwa hospitali Ifakara, basi nikiwa na ndugu wengine tulikwenda Morogoro na kuchukua mwili wa mpendwa wetu,” amesema Clavery.
Ameongeza kuwa baada ya kufika Morogoro kwa ajili ya kuchukua mwili wa kaka yake, hakuweza kupata nguvu na muda wa kuuliza chanzo cha mauaji hayo na wala kujua nani amehusika, bali waliweza kuwasiliana na polisi na kukabidhiwa mwili na kuusafirisha hadi Simiyu kwa ajili mazishi.
“Hata hivyo, baada ya kufika Ifakara tulipata taarifa kutoka polisi kuwa yule shemeji amekamatwa na kushikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kaka na kula njama, sisi kama familia hatuwezi kuthibitisha kama kweli shemeji amefanya hivyo ama la, wenye uwezo wa kuthibitisha hilo ni polisi baada ya kukamilisha uchunguzi,” amesema Clavery.
Kuhusu maisha aliyokuwa akiishi kaka yake na mke wake, Clavery amesema hana uhakika kama yalikuwa ni maisha mazuri na furaha ama ya migogoro kwa kuwa katika kipindi chote walichoishi, hakuwahi kusikia kesi wala malalamiko kutoka kwa wanandoa hao.
“Enzi za uhai wake, kaka yangu alikuwa ni mtu mcheshi, hakuwa mgomvi, yawezekana alikuwa akipita kwenye migogoro ya ndoa lakini mimi kama mdogo wake na hata ndugu wengine hawajawahi kusikia alilalamika kufanyiwa vitendo vya ukatili na mke wake, hivyo kama alikuwa akipita kwenye magumu basi alichagua kuvumilia,” amesema Clavery.
Akieleza kauli ya mwisho aliyoongea na kaka yake, Clavery amesema wamekuwa na mazungumzo ya kawaida lakini mara ya mwisho alimtumia picha na kumuandikia ujumbe kuwa picha hiyo itumike kwenye jeneza endapo atafariki siku yoyote.
“Nakumbuka kuna picha moja alinitumia na kuniambia kama atakufa basi ndiyo itumike kwenye jeneza, sikujua alikuwa anamaanisha nini, mimi niliitunza ile picha na siku ya msiba tuliamua kuitumia ile picha kama alivyousia na hiki ndio kitu kinachoniuma zaidi,” amesema Clavery.
Amesema kaka yake ni mtoto wa tatu kati ya watoto sita waliozaliwa kwenye familia ya mzee Tungaraza ambapo naye ameacha watoto watatu aliozaa na mke wake huyo ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi.
Amesema tayari watoto wawili kati ya hao watatu wamechukuliwa na ndugu zao na mmoja mdogo mwenye umri chini ya miaka miwili alichukuliwa na akiwa na mama yake polisi walipokuja kukamata.
Mmoja wa walimu ambao ni marafiki wa karibu wa marehemu Tungaraza ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema taarifa alizopata ni kwamba wanandoa hao walikuwa kwenye mgogoro ambao unaelezwa kuwa ulitokea baada ya mke kutokuwa mwaminifu katika ndoa yake.
“Mwalimu Tungaraza enzi za uhai wake alisumbuana na mke wake hasa kwa kile kinachodaiwa kuwa mke wake hakuwa mwaminifu na zipo taarifa kuwa alikuwa na uhusiano na kijana mmoja ambaye tunasikia tayari ameshakamatwa,” amesema mwalimu huyo.
Jirani wa marehemu Tungaraza ambaye pia ni katibu wa Kitongoji cha Gendeni, Kijiji cha Mang’ula A, Fahamia Abdallah amesema Aprili 2024, Tungaraza alifika kwenye Serikali ya kitongoji hicho na kueleza mgogoro uliopo baina yake na mke wake, huku akitaja sababu kubwa ya mgogoro huo kuwa ni mke wake kutokuwa mwaminifu katika ndoa na kumtaja kijana mmoja kuwa alikuwa na mahusiano na mke wake.
Katibu huyo wa kitongoji amesema kuwa baada ya kupokea madai hayo mke wa Tungaraza aliitwa katika ofisi hizo na viongozi akiwemo yeye katibu na baada ya kuelezwa kile anachotuhumiwa mwanamke huyo alimuomba radhi mume wake (Tungaraza) na kumuahidi kujirekebisha hasa kitabia na hivyo wanandoa hao waliondoka na kwenda kuendelea na maisha kama kawaida.
“Wiki mbili kabla ya Mwalimu Tungaraza hajauawa, alinipigia na kunipa taarifa kuwa kijana aliyekuwa akimtuhumu kujihusisha kimapemzi na mke wake aliendelea kufika nyumbani kwake. Hivyo aliniomba nizungumze na mke wake na nimuonye kwa kuwa jambo hilo halipendi, sikuwahi kumuita huyu mwanamke kwa kuwa na mimi nilianguka na kuvunjika mguu. Nilitamani kabla ya kumuita nifanye uchunguzi wangu ili nijiridhishe lakini ndo hivyo kama sijakamilisha uchunguzi ndipo tukio hilo likatokea,” amesema Fahamia.
Akizungumzia marehemu Tungaraza, katibu huyo amesema tangu amemfahamu hajawahi kumuona akigombana na mtu yeyote na mara zote amekuwa akicheka na watu na pia hajawahi kupelekwa kwenye Serikali ya kijiji kwa tuhuma zozote, hivyo kifo chake kimeacha maswali mengi kwa wananchi wa Mang’ula na hata maeneo ya jirani.
Kufuatia tukio hilo, katibu huyo amesema Serikali ya kijiji imepanga kuitisha mkutano mkubwa wa wananchi kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya kuepukana na matukio kama hayo ambayo yanaweza kutokea, pia ameliomba Jeshi la Polisi kutenda haki ili wote waliohusika na mauaji hayo wakamatwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama akizungumza na waandishi wa habari, amesema mwalimu huyo akiwa amelala na mtuhumiwa (mke wake) na watoto wao wawili, alivamiwa ndani na kuuawa kwa kupigwa na kitu butu kichwani.
Kamanda Mkama amesema baada ya mauaji hayo, jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kuwapata watuhumiwa wengine ambao wanatuhumiwa kushirikiana na mwanamke huyo.