Dodoma. Uwasilishaji wa bajeti za kisekta na uchangiaji wa wabunge wa mijadala ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2024 /25 umekuwa na mbwembwe na ubunifu huku baadhi wakitumia teknolojia kuwabana mawaziri kwa kauli walizotoa bungeni na nje ya Bunge.
Wizara mbalimbali ziliamua kufanya maonyesho katika viwanja vya Bunge kwa ajili ya kuwawezesha kupata baadhi ya majibu ya changamoto katika maeneo yao kabla ili pindi wanapochangia bungeni baadhi ya hoja zao zinakuwa zimeshapatiwa majibu na jinsi ya kuzitatua.
Baadhi ya wabunge wakaamua kuja kivingine na safari hii walitumia teknolojia kuwabana mawaziri kuhusu ahadi walizokuwa wakipewa bungeni hapo na utofauti wa kauli wanazotoa nje ya Bunge.
Mbunge wa Mbulu (CCM) Flatei Massay ni mmoja wa wabunge ambaye amekuwa akitumia mtindo wa aina yake kuwasilisha hoja zake bungeni.
Mei 23, 2022, wakati akichangia bajeti iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sasa Wizara ya Ujenzi, aliruka sarakasi akisisitiza ujenzi wa Barabara ya Hydom, Mbulu hadi Karatu mkoani Manyara.
“Spika hapa ananiangalia kwa jicho la tahadhari, niambie mwenzangu nafanyaje sasa wewe unamdanganya spika wetu, maana wewe, sasa hivi unamdanganya Rais wetu, mimi kuliko Rais aonekane mwongo, ninahakikisha wewe utaonekana mwongo humu ndani,” alisema Massay.
Baada ya maneno hayo Massay alichukua kishikwambi (tablet) yake na kusogeza katika kipaza sauti kabla ya kuwasha ‘clip’ ya sauti ya mwaka jana wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya matumizi kupitisha bajeti ya wizara hiyo.
Katika ‘clip’ hiyo anasikika Massay akitaka ufafanuzi kuhusu fedha chache zilizotengwa katika ujenzi wa barabara hiyo zitatumika kufanya nini huku Profesa Makame Mbarawa akimjibu kuwa zitajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kwamba itachukua miaka miwili kukamilika.
Mbunge wa Mbozi (CCM), George Mwanisongole alisema sikilizisha ‘clip’ ya Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba ambayo aliiweka katika mtandao wa Instagram akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika ‘clip’ hiyo, Dk Mwigulu alikuwa akisisitiza kuwa kuwatoza masikini na kuwapa ahueni matajiri ya kodi ni jambo ambalo halikubaliki.
“Inakuaje tunatoza ushuru wa mazao kwa mkulima kwa kukutana na mageti na mageti halafu tuna fedha nyingi ambazo hatukumbuki kama tulishawahi kukusanya ama la. Hiyo ni kufanya watu wetu walioko vijijini kuwa masikini huku tukiwafanya matajiri wafurahie kama wako mbinguni,”alisikika Dk Mwigulu akisema katika sehemu ya ‘clip’ hiyo.
Alimtaka Dk Mwigulu kuiondoa ‘clip’ hiyo katika mtandao kwa kuwa kinachofanyika hakiakisi maneno hayo na kwamba ushuru wa bidhaa (withholding tax) ulioondolewa katika mazao na Bunge umerudi kwa namna nyingine kwa kuwatoza wakulima wanapoenda kuuza mazao yao katika vyama vya ushirika.
Kati ya bajeti bajeti zito za kisekta Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Wizara ya Ujenzi wao walikuja na mbwembwe zao wakati wanawasilisha bajeti zao za kisekta.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inayoongozwa na Nape Nnauye alikuja na roboti ambalo lilipewa jina la Eunice ambalo asubuhi Mei 16, 2024 saa chache kabla ya kusomwa kwa bajeti ya wizara yake liliwakaribisha wabunge kwenye bajeti hiyo.
“Ninafuraha kukukaribisha mheshimiwa mbunge kwenye bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Asante nakutakia kikao chema cha bajeti,”ndivyo roboti hilo lilivyokuwa likisema huku likipeana mikono na wabunge katika lango kuu la kuingilia ukumbi wa Bunge.
Mei 29, mwaka 2024, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ambaye naye siku ya bajeti yake mbwembwe hazikuachwa nyuma katika viwanja vya Bunge asubuhi kabla ya kusomwa kwa bajeti yake.
Kabla ya kuingia ndani ya ukumbini, anasimama katika viwanja vya Bunge ili kuzungumza na Mzee Kimbwembwe akiwa na mkwewe kutokea Kilwa mkoani Lindi, waliomletea zawadi ya jogoo bungeni.
“Sasa mheshimiwa waziri kwa mila na desturi zetu za watu wa Kilwa, tukupe zawadi waziri wetu, mkombozi wetu baada ya kutoka Dar es Salaam kufika katika eneo letu wakati tulipopata matatizo ya mafuriko, ulikaa kwa siku tano…Yale uliyafanya kwa mapenzi yetu,”alisema Mzee.
“Kwa uwajibikaji wako, kwa huruma yako. Kwa niaba ya wananchi wa Kilwa pokea zawadi hii kama shukrani yetu, mfikishie pia salamu zetu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutatua tatizo la barabara kwa saa 72.”
Bashungwa anakuwa kiongozi wa pili kupewa jogoo na Mzee Kimbwembwe baada ya kumpatia Hayati Rais John Magufuli Julai 2020, Mzee Kimbwembwe alipokuwa safarini kuelekea Mtwara akitokea jijini Dar es Salaam.
Mzee huyo alimweleza Rais Magufuli kuwa jogoo huyo ni shukrani yao wananchi wa Somanga mkoani Lindi kwa kujengewa kituo cha afya katika eneo hilo.
Hata hivyo, akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi, kwa mwaka 2024/25, Massay alisema licha ya kila mwaka kutengwa kwa bajeti hiyo bado haijajengwa kwa kiwango cha lami.
Mbwembwe hizo za wakati wa uwasilishaji wa bajeti hazikuishia kwa mawaziri hao, bali hata katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyowasilishwa Juni 2, 2024.
Wizara hiyo ikiongozwa na Angellah Karuki, walikuja kinamna yake kwa kuweka banda la wanyama pori mbalimbali wakiwamo tembo, simba, duma na kobe kwenye viwanja vya Bunge na hivyo kuwapa fursa wabunge kujionea wanyama hao.
Aidha, katika siku mbili za bajeti yake, wabunge walipata nafasi ya kula nyama pori ilioandaliwa katika viwanja vya Bunge, lengo ni kuhamasisha utalii wa vyakula.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Leonce Mujwahuzi alisema hapo inawafundisha wananchi wanapofanya uchaguzi wa viongozi wanatakiwa kuwapima katika kufahamu kuwa wanaongea na wanachokiandika wanachokimaanisha.
“Miaka 2024 huwezi mtu ukafanya uchaguzi kwa kudanganywa na mtu uliyemuona leo kwa sababu ameleta kofia,chakula ama amekuletea Sh20,000, tunapaswa kumpima mtu katika utu wake kwa maana anachokiongea na kwa kuandika anakimaanisha.
“Kwa sababu hayo mambo tumekuwa hatuyazingatii, tumekuwa tukiweka wafanya maagizo. Kwa miaka hii ya 2024 tuende katika mambo ya kiuhalisia na tuchague mtu kwa ajili ya utu wake na sio kwa maigizo na maagizo yanajulikana,”alisema Dk Mujwahuzi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema anaona bado matumizi ya teknolojia kwa wabunge ni madogo kwa kuwa hawajaitumia vya kutosha.
“Kwa sababu kati ya vitu ambavyo vinasaidia sana kuumbua watu hawako inconstancy (wanyoofu) ni teknolojia. Tutunataka wanasiasa wawe constancy anachokisema leo kiwe sawa na atakachokisema kesho na kesho kutwa. Sio leo anasema hiki halafu kesho anasema kile,” alisema.
Dk Mbunda alisema teknolojia inatakiwa kusaidia kuwaumbua wabababishaji na wabunge wanatakiwa kuwa wabunifu kwa sababu taarifa zote ziko kwenye mtandao (online) tofauti na zamani ilivyokuwa ikiwapasa kwenda kutafuta kumbukumbu rasmi za Bunge (kwa njia ya karatasi).
“Wahakikishe wanafuatilia na kuona leo wamesema nini na kesho wamesema nini ili wakiona ubabaishaji wamlipue mtu hadharani. Hii itasaidia kujienga tabia ya wanasiasa kuwa wanyoofu. Kama unasimamia msimamo huu basi usimamie huo huo,” alisema.