Mkuu wa Mkoa adaiwa kumlawiti mwanafunzi

Mwanza/Dar. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea na uchunguzi juu ya tukio la kigogo mmoja wa juu ngazi ya mkoa wa kanda ya ziwa, kutuhumiwa kumlawiti mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Mwanza ndani ya gari.

Uchunguzi umebaini jina la usajili wa namba ya simu iliyotajwa na mwanafunzi huyo, linafanana na la mmoja wa wakuu wa mikoa nchini.

Mbali na usajili huo ambao hufanywa kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa kuonyesha jina linalofanana na la mteule huyo, lakini jina hilohilo pia ndilo linaonekana katika tovuti ya ofisi ya mkuu wa mkoa huo na akaunti ya Instagram.

Lakini jina hilo pia limetokea katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mwaka 2022 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ingawa jina linaloonekana kwenye usajili wa simu na lile linaloonekana katika akaunti ya mkuu wa mkoa huyo kwenye mtandao wa  Instagram, linatofautiana kwa  jina la katikati.

Tukio hilo linalodaiwa kutokea Juni 2, 2024 katika eneo la maegesho la moja ya baa mashuhuri jijini Mwanza, tayari limeanza kusambaa katika mitandao ya kijamii hususan X (zamani Twitter) ingawa aliyetoa taarifa hiyo, hakumtaja mhusika kwa jina.

Uchunguzi wa gazeti hili kutoka vyanzo mbalimbali jijini Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam, vimedokeza uchunguzi wa suala hilo unafanywa kwa usiri mkubwa,  kwani  mtuhumiwa ni mtu mzito serikalini ambaye mpaka jana jioni alikuwa hajatiwa mbaroni.

Kulingana na taarifa kutoka vyanzo hivyo, tayari polisi walichukua sampuli kwa ajili ya kupima vinasaba (DNA) kutoka katika nguo alizokuwa amevaa mwanafunzi huyo kama zitaoana na mtuhumiwa na kuzituma kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Taarifa zimeeleza tukio hilo linaendelea kuchunguzwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza na tayari taarifa za awali zimetumwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai ambaye alipotafutwa hakupatikana.

Gazeti hili limemtafuta mmoja wa maofisa Ofisi ya Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema:“Taarifa za tukio hilo aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.”

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Wilbrod Mtafungwa alipotafutwa amesema: “Nipo msibani kwa sasa hivi.’’ (ilikua saa 10 jioni)

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya alipotafutwa ikiwa ni saa 12:40 jioni kuhusu suala hilo, hakukubali wala kukanusha juu ya uwepo wa tukio hilo zaidi amesema: “Yapo mambo anayoongea kamanda kama kamanda.”

Alipoulizwa na gazeti hili kuwa yeye ndiye ameachiwa ofisi, Kamanda Msuya alisisitiza atafutwe kamanda Mutafungwa kwani ndiye hutoa taarifa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alipotafutwa kuzungumzia suala hilo kutokana na yeye kuwa mwenyekiti wa usalama mkoani humo amesema: “Mimi sijaletewa kwenye dawati langu hilo tukio la mwanafunzi na huyo mwanafunzi hajaniletea hilo suala labda niwasiliane na polisi.”

Hivi ndivyo uhusiano ulivyoanza

Uchunguzi wa gazeti hili kwa kuegemea vyanzo mbalimbali jijini Mwanza, Dar es Salaam na Dodoma, zinaeleza mtuhumiwa huyo alianza uhusiano na mwanafunzi huyo mwenye miaka 21 Januari 2024 jijini Mwanza.

Siku hiyo walikutana katika tafrija ya siku ya kuzaliwa ambayo mtuhumiwa anatajwa ndiye alikuwa mgeni rasmi na hapo ndipo walipobadilishana simu na kuanzisha uhusiano na kuendelea kuwasiliana kwa simu mara kwa mara.

“Unajua huyu bosi ili kumu win (kumpata) huyu dada alianza kumtumia fedha za matumizi ya hapa na pale. Sasa ile mwezi Februari 2024 kama utakumbuka kulikuwa na ziara ya Rais hapa Mwanza,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo hicho kimedai siku hiyo kigogo huyo alikutana na dada huyo katika moja ya hoteli jijini Mwanza, ambapo katika hali ya kustaajabisha, alimuomba wafanye mapenzi kinyume cha maumbile, ombi ambalo dada huyo alilikataa.

Kigogo huyo inadaiwa aliendelea kumshawishi akubali kufanya naye mapenzi kinyume cha maumbile kwa ahadi kuwa angempa maisha mazuri na kumuahidi angekuwa anampa kiasi kisichopungua Sh500,000 kila mwezi.

Tukio lenyewe lilivyokuwa

Chanzo kimoja kutoka ofisi ya kigogo huyo, kimedai siku ya tukio, mtuhumiwa alitumia kila mbinu kumshawishi mwanafunzi huyo wakutane jijini Mwanza, ambapo walikutana katika baa hiyo mashuhuri na kupata vinywaji.

“Sasa baada ya muda huyu jamaa akamuambia wakazungumze kwenye gari maana kuna mambo ya muhimu anataka kumweleza. Huko sasa jamaa ndio akashinikiza wafanye kinyume cha maumbile,” kimedokeza chanzo hicho.

Chanzo kingine kutoka moja ya ofisi nyeti za Serikali jijini Dodoma, kimedai baada ya kwenda kwenye gari lililokuwa limeegeshwa eneo la maegesho ya klabu hiyo, ndipo kigogo huyo alipotimiza haja zake.

“Tunavyoambiwa sio kwamba huyo mwanafunzi aliridhia, hapana. Huyu jamaa alimtisha sana na kwa vile huyu dada alikuwa anamjua kama mheshimiwa, alijua ni watu wanatembea na silaha na walinzi hivyo akafanya aliyoyafanya”.

“Inaonekana huyu  ni mchezo wake baada ya kumshawishi sana huyu dada wa watu akamgomea. Ndio naona akaja na hiyo plan B (mpango wa pili) wa kumwita kwenye gari akamvua nguo kwa nguvu na kumlawiti,” kimesema chanzo kingine.

Chanzo kingine kilidai kigogo huyo na gari alilolitumia vilinaswa na kamera za usalama zilizofungwa katika klabu hiyo tangu gari hiyo inaingia, kuegeshwa na kutoka usiku wa saa sita na namba za usajili zilisomeka vizuri.

Kamera zinaonesha ilipofika saa 2:48 usiku, binti huyo alionekana akiingia katika gari hilo na saa 3:21 usiku, takribani dakika 30 kupita, mlalamikaji alionekana akitoka kwenye gari.

Saa 6:24 usiku, zinaonesha gari hilo lilionekana katika geti la kutokea likiwa eneo la mwanga mkali uliowezesha kulitambua usajili wake. Dereva wa gari hilo alikuwa amevalia kofia aina ya kapelo akitoka kwenye gari hilo kwa ajili ya kulipia ushuru wa maegesho.

Taarifa zinadai, Juni 3 mwaka huu, siku moja tangu alipofanyiwa ukatili huo, binti huyo alikwenda kutoa taarifa katika  kituo cha Polisi-dawati la jinsia na watoto, jijini Mwanza. Alisikilizwa kisha kupelekwa moja ya  hospitali kubwa jijini hapo  kwa uchunguzi.

Katika uchunguzi huo uliofanywa na daktari (jina tunalihifadhi), alibaini mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza aliingiliwa kinyume na maumbile.

Taarifa zinadai Jeshi la Polisi limetuma barua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza ili kupata usajili wa namba za gari hilo aina ya Toyota Crown nyeupe.

Aidha, tararibu za kupeleka simu ya mlalamikaji na vipande vya picha zilizopigwa na kamera za usalama zinaandaliwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye maabara ya uchunguzi wa kisayansi.

Related Posts