Mwanza. Watu saba wamejeruhiwa baada ya daladala kuacha njia na kugonga nguzo zilizoko barabarani eneo la Nyakato Sokoni, Jijini Mwanza.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya amesema ajali hiyo imetokea leo Jumatatu Juni 10, 2024 na uchunguzi wa awali unaonyesha daladala hilo liliacha njia kwenda kugonga nguzo zilizokuwa pembeni mwa barabara, baada ya kufeli breki.
“Gari aina ya Tata ikiwa inatoka Kisesa kwenda Usagara leo saa 1:45 asubuhi ikiwa imebeba abiria kwenda katika maeneo mbalimbali wakiwemo wanafunzi, ilipata hitilafu ya mfumo wa breki, hali iliyosababisha gari ikose uelekeo na kugonga nguzo zilizoko barabarani na kusababisha majeruhi na uharibifu wa chombo,” amesema Msuya.
Kaimu Kamanda huyo amesema katika ajali hiyo hakuna kifo na majeruhi wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure na Kituo cha Afya Buzuruga mkoani humo kwa matibabu zaidi.
“Jeshi la Polisi tunaendelea na msako wa dereva wa gari hilo ambaye ametokomea kusikojulikana baada ya ajali kutokea,” amesema Msuya.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure, Bahati Msaki, wamepokea majeruhi 41, wanaume 22 na wanawake 19, huku abiria saba wakiwa wamejeruhi vibaya, akiwemo mtoto wa miezi miwili.
Amesema majeruhi wanne wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na watatu wanaendelea na matibabu hospitalini hapo.
“Majeruhi wengine waliopata michubuko tumepatia huduma ya kwanza na kuwaruhusu kuendelea na shughuli zao,” amesema Dk Msaki.
Akisimulia ajali ilivyotokea, mwanafunzi wa Sekondari ya Pamba jijini humo, Tatu Wambura amesema alipandia kituo cha Igoma na gari lilipokaribia eneo la Nyakato dereva alionekana kujawa hofu.
“Baadhi ya abiria waligundua gari linamshinda dereva wakawa wanapiga kelele asimame washuke, lakini hakusimama mpaka lilipomshinda na kwenda kuligongesha kwenye nguzo zilizokuwa pembeni ya barabara,” amesimulia mwanafunzi huyo.
Anasema baadhi ya abiria waliokuwa wamekaa mbele, akiwamo mwanafunzi wa shule ya msingi, abiria mmoja na dereva wao walirushwa nje kupitia kioo cha mbele na abiria wengine wakakandamizwa na viti.