Waziri Mkuu Haiti augua ghafla, apelekwa hospitali

Haiti. Waziri Mkuu mpya wa Haiti, Garry Conille, amepelekwa hospitali baada ya kuugua ghafla, huku ikidaiwa kuwa ni shambulio la ugonjwa wa pumu.

 “Baada ya wiki ya shughuli nyingi, Conille aliugua alasiri ya Juni 8, 2024 na akapelekwa hospitali kwa matibabu,” taarifa ya ofisi ya mawasiliano ya waziri mkuu imeeleza.

Chanzo kutoka serikalini kikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, kimeiambia AFP kwamba Waziri Mkuu alipata shambulio la pumu na huenda akasafirishwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi. Hali yake kwa sasa inaendelea vizuri.

Conille (58), aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Baraza la Mpito la Rais la Haiti,   Mei 29, 2024 kisha kuapishwa.

Conille, aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Haiti kwa kipindi kifupi mwaka 2011-2012 na hadi anarudi tena kuwa Waziri Mkuu mwezi Mei, alikuwa Mkurugenzi wa Kikanda wa Shirika la Misaada la Umoja wa Mataifa (UNICEF).

Hata hivyo, wataalamu wanasema kazi iliyo mbele yake ni kubwa, ikiwemo kuondoa mizozo ya kisiasa, kiusalama na kibinadamu inayoichachafya nchi hiyo maskini katika ukanda wa magharibi.

Tangu kuteuliwa kwake amekuwa akifanya vikao mfululizo na wadau na wawakilishi, huku akiwa katika harakati za kuunda baraza la mawaziri.

Ghasia za magenge kwa muda mrefu zimeikumba Haiti, lakini mwishoni mwa Februari makundi yenye silaha yalianzisha mashambulizi yaliyoratibiwa kwenye maeneo ya kimkakati huko Port-au-Prince yakidai yalitaka kumpindua Waziri Mkuu, Ariel Henry.

Henry, ambaye alikuwa akiiongoza nchi hiyo tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mwaka 2021, alikubali kujiuzulu na kukabidhi mamlaka kwa baraza la mpito la wanachama tisa.

Kabla ya kuugua ghafla, Conille alitembelea uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince, kusifu juhudi za vikosi vya usalama vilivyowezesha safari za ndege kuanza tena baada ya kusimamishwa kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na mashambulizi ya magenge.

Ghasia hizo zimeathiri pakubwa usalama wa chakula na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, huku sehemu kubwa ya mji mkuu ukiwa mikononi mwa magenge yanayotuhumiwa kwa unyanyasaji ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji, uporaji na utekaji nyara.

Related Posts