KIUNGO Axel Witsel, 35, ambaye amerejea tena kutoka kustaafu ili kuichezea Ubelgiji katika michuano ya Euro, amefikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye viunga vya Atletico Madrid.
Mabosi wa Atletico wamevutiwa na kiwango cha Witsel alichoonyesha msimu uliomalizika ambapo alicheza mechi 51 za michuano yote.
NEWCASTLE inapambana kuhakikisha inaipata saini ya beki wa AFC Bournemouth, Lloyd Kelly, 25, katika dirisha hili baada ya kuikosa huduma ya beki wa Fulham na England, Tosin Adarabioyo, 26, aliyefikia makubaliano ya kujiunga na Chelsea.
Lloyd ambaye anamalizika mkataba Juni mwaka huu, msimu uliomalizika alicheza mech 25 za michuano yote.
VIGOGO wa Manchester United wameamua kumuuza staa wao Jadon Sancho kwa Pauni 40 milioni katika hili hata itakapomfukuza Erik ten Hag ambaye Sancho ameeleza kwamba ikiwa ataondoka yeye ndio atarudi.
Sancho ambaye ameonyesha kiwango bora akiwa na Dortmund kwa mkopo katika msimu uliomalizika, mkataba wake unamalizika mwaka 2026.
MANCHESTER United inataka kulipa Pauni 40 milioni kwa ajili ya kuipata saini ya beki wa Everton, Jarrad Branthwaite ambaye timu yake inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni ili kumuuza.
Man United imevutiwa sana na staa huyu kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita ambapo alicheza mechi 41 za michuano yote. Mkataba wake unamalizika 2027.
BAYERN Munich inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuipata saini ya winga wa Stuttgart, Chris Fuhrich katika dirisha hili.
Winga huyu raia wa Ujerumani alionyesha kiwango bora katika msimu uliomalizika kilichovutia vigogo wengi barani Ulaya.
Mkataba wa sasa wa Chris unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, msimu huu amecheza mechi 38 za michuano yote.
BORUSSIA Dortmund imeshaanza mazungumzo na mabosi wa Olympique Lyon kwa ajili ya kuipata saini ya beki wa timu hiyo na Ireland, Jake O’Brien, 23, katika dirisha hili.
Jake ambaye huduma yake pia inahitajika na Everton na AC Milan, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu uliomalizika alicheza mechi 32.
LIVERPOOL imeanza mazungumzo na FC Porto kwa ajili ya kumsajili staa wa timu hiyo raia wa Argentina, Alan Varela, 22, katika dirisha hili.
Benchi la ufundi la Liverpool chini ya Arne Slot limevutiwa na ripoti ya maskauti iliyowasilishwa mezani kwao ikimwelezea kiungo huyu ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.