Hat trick ya 7 yapigwa Zenji, Uhamiaji ikiizamisha Kipanga

LIGI Kuu ya Zanzibar (ZPL) iliyopo ukingoni imeendelea tena jioni ya leo, ikishuhudiwa hat trick ya saba ikifungwa visiwani humo, wakati Uhamiaji ikiizamisha Kipanga kwa mabao 3-2 katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan A, mjini Unguja, huku Malindi ikitakata mbele ya Mafunzo kwa bao 1-0.

Mchezaji aliyeingia katika orodha ya watupia hat trick kwa msimu huu ni; Yahya Haji Salmin wa Uhamiaji aliyefunga mabao yote matatu yaliyoizima Kipanga na kumfanya afikishe matano hadi sasa katika Ligi hiyo iliyosaliwa na mechi za raundi mbili kabla ya kufikia tamati Juni 17.

Yahya alifunga mabao hayo katika dakika ya kwanza tu, tangu filimbi ilipolia kuashiria kuanza kwa pambano hilo, kisha akaongeza mengine mawili dakika ya 11 na 51, huku mabao ya kufutia machozi ya Kipanga iliyokuwa wenyeji wa mchezo huo yakifungwa na Muhamed Ramadhan Ameir dakika ya 15 na Juma Amir Kombo aliyekwamisha dakika ya 51.

Kabla ya Yahya kufunga hat trick hiyo inayokuwa ya saba kwa msimu huu na iliyoiwezesha Uhamiaji kufikisha pointi 38, wachezaji wengine sita walitangulia kufanya akiwamo Ibrahim Hamad ‘Hilika’ wa Zimamoto aliyefunga dhidi ya Ngome waliyoinyoa kwa mabao 5-0 na Ibrahim Is-haka wa KMKM walipoichapa New City pia kwa 5-0.

Wengine ni kinara wa orodha ya wafungaji wa msimu huu, Suleiman Mwalimu Abdallah wa KVZ, aliyeweka rekodi ya kufunga mabao manne katika mchezo mmoja wakati timu hiyo ya maafande ikiizamisha Maendeleo kwa mabao 7-3.

Suleiman ndiye anaongoza orodha ta wafungaji akiwa na mabao 20 akifuatiwa kwa mbali na Ibrahim Hamad ‘Hilika’ mwenye mabao 15, huku akizikosa mechi kadhaa za timu hiyo ya Zimamoto kutokana na kuwa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambacho kesho Jumanne kitashuka jijini Ndola, Zambia kuvaana na wenyeji Chipolopolo.

Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa ni ya kuwania fainali za Kombe la Dunia za 2026.

Nyota wa JKU, Mudrick Miraji Mawia, ni mkali mwingine aliyefunga hat trick msimu huu wakati timu hiyo ikishinda mabao 7-0 dhidi ya Jamhuri, naye Moh’d Ali Moh’d wa Mlandege alifunga matatu walipoichapa Maendeleo kwa mabao 5-2, huku Mgaza Seleman Ramadhan wa Zimamoto alipiga ya sita wakati akiizamisha Jamhuri kwa mabao 3-0.

Katika mechi nyingine ya Ligi hiyo ya ZPL iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mao A, pia mjini Unguja Malindi iliizamisha Mafunzo kwa bao 1-0, lililowekwa kimiani na Mohammed Abdallah Ali dakika ya 65 na kuwafanya mabingwa hao wa zamani w Tanzania kufikisha pointi 35 baada ya mechi 28.

Mafunzo yenyewe imesaliwa na pointi 44 ikiwa nafasi ya tano baada ya kucheza mechi 28 pia.

Related Posts