MUNICH, UJERUMANI: SIKU zinakwenda kasi sana. Euro 2008 inaonekana kama ni jana tu hapo, lakini kumbe michuano hiyo ilikuwa miaka 16 iliyopita, ambapo mastaa waliotamba uwanjani wakati huo wakiwa wachezaji kwa sasa ni makocha.
Kuwa mchezaji mzuri hakuna maana kwamba utakuwa kocha mzuri, lakini sehemu kubwa ya waliopo kwenye kundi hilo ni wale ambao walikuwa moto uwanjani na kutamba kwenye fainali za Euro 2008 na sasa wanafanya vizuri wakiwa kwenye mabenchi ya ufundi.
Ndoto ya kucheza msimu wote bila ya kupoteza kwenye michuano yote zilikufa baada ya kikosi chake cha Bayer Leverkusen kuchapwa na Atalanta kwenye mchezo wa fainali ya Europa League. Lakini, Alonso, rekodi zake kwenye Bundesliga kwa msimu wa 2023-24, timu yake ilizicheza msimu wote bila ya kupoteza mechi hata moja. Alonso aliichukua Leverkusen miezi 18 iliyopita ikiwa kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini baada ya hapo aliifanya timu hiyo kucheza mechi 51 bila ya kuonja machungu ya kupoteza, huku akiweka rekodi tamu kabisa kwenye Bundesliga.
Alikuwa sehemu ya kikosi cha Italia kwenye Euro 2008. De Rossi ameliweka jina lake kwenye ramani ya makocha mahiri mwaka huu. Alirithi mikoba ya Jose Mourinho alipofutwa kazi huko AS Roma na hakika, kiungo huyo wa zamani ameonyesha kile ambacho anaweza kukifanya na kuonyesha mwanzo mzuri katika maisha yake mapya ya ukocha. Aliichukua AS Roma ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo, lakini aliisaidia na kumaliza nafasi ya sita na kufuzu kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
Kiungo huyo wa zamani wa Hispania aliingia kwenye ukocha huko Qatar miaka kadhaa iliyopita kabla ya kunasa dili la kuinoa Barcelona mwaka 2021. Tangu wakati huo, Xavi alionyesha kwamba ukiweka kando ule umahiri wake wa kukamatia kiungo enzi zake akiwa mchezaji, amekuwa moto pia kwenye ukocha, ambapo aliisaidia Barcelona kushinda ubingwa wa La Liga mwaka jana. Mwaka huu mambo yake hayakuwa mazuri kwenye kikosi hicho cha Nou Camp na baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano yote, Xavi alifunguliwa mlango wa kutokea huko Nou Camp.
Tangu alipotundika daruga zake 2018, Kuyt amepita kwenye klabu nyingi akifanya kazi ya ukocha kabla ya sasa kuripotiwa kuinoa klabu ya Beerschot ya huko Ubelgiji. Amekuwa akifanya vizuri kwenye kazi yake ya ukocha kama ambavyo alikuwa mchezaji, aliyekuwa akiichezea Uholanzi kwenye fainali za Euro. Beerschot alianza kuinoa Desemba mwaka jana na alifanikiwa kushinda ubingwa wa Challenger Pro League, ambao ni ubingwa wa ligi ya pili kwenye soka la Ubelgiji.
Ni kitu kinachoweza kukusangaza kufahamu kwamba Nuno alikuwa bado anakipiga mwaka 2008, lakini ndiyo hivyo, kwa sasa Mreno huyo ni kocha hodari. Nuno alikuwa sehemu ya kikosi cha Ureno kilichofika robo fainali katika michuano hiyo, lakini hakucheza dakika yoyote kwenye fainali hizo. Kutoka hapo hadi sasa 2024, Nuno amekuwa kocha kwenye klabu saba tofauti. Baada ya kutamba kwenye klabu za FC Porto, Wolves, Tottenham na Al-Ittihad, kwa siku za karibuni amekuwa akiinoa Nottingham Forest.
Staa huyo wa kimataifa wa zamani wa Uholanzi ameshakuwa kocha kwenye zaidi ya mechi 100 hadi sasa, lakini kwa siku za karibuni amekuwa hana kazi. Alikuwa bosi wa PSV ya Uholanzi kwa mwaka mmoja, ambapo inaelezwa kwamba alitengeneza msingi imara uliokuja kumsaidia kocha Peter Bosz kunyakua ubingwa wa Eredivisie msimu huu. Kwa uhodari wake alionyesha kwenye kazi ya ukocha ni suala la muda tu kabla ya kumshuhudia Van Nistelrooy akirudi tena mzigoni kwa maana ya kupata timu nyingine ya kuifundisha.
Ajira ya kuinoa Juventus ilidaiwa kuja mapema sana kwa Andrea Pirlo katika kazi yake ya ukocha, lakini baada ya kuachana na vigogo wa Serie A, alikwenda kutengeneza jina lake huko Fatih Karagumruk na sasa Sampdoria. Pirlo, aliyekuwa moto kwenye Euro 2008 akiwa na kikosi cha Azzurri, aliiongoza Sampdoria kucheza mchujo kwenye Serie B msimu huu, lakini kwa bahati mbaya ilichapwa na Palermo kwenye raundi ya awali. Hata hivyo, umahiri wake kwenye kufundisha ni kitu cha muda tu kabla ya kiungo huyo fundi wa mpira hajapata kazi ya juu zaidi.
Kovac alitangaza kustaafu soka muda mfupi baada ya kukamilika kwa fainali za Euro 2008 na kiungo huyo wa zamani wa Croatia amefanya kazi za ukocha kwenye klabu nyingi tangu wakati huo. Alipata umaarufu zaidi kwa wakati wake alipokuwa kocha wa Bayern Munich, lakini pia Niko Kovac alipita kwenye mabenchi ya ufundi ya klabu za AS Monaco, Eintracht Frankfurt na Wolfsburg katika miaka ya karibuni. Kwa kusema ukweli, wakati ambao alifanya vizuri zaidi kwenye kazi yake ya ukocha ni wakati alipokuwa kwenye benchi la ufundi huko Allianz Arena.
Kiungo huyo Mfaransa kazi yake ya kwanza ya ukocha ilikuwa 2016 wakati alipochukua mikoba ya kuinoa timu ya Ligi Kuu Marekani, New York City FC. Baada ya hapo alipita kwenye kikosi cha Nice na Crystal Palace kabla ya kwenda kuwa kocha wa Strasbourg. Alipokuwa Palace kwenye Ligi Kuu England, timu ya Vieira ilikuwa ikicheza soka lenye mvuto kwelikweli na kuzivimbia timu vigogo wa Big Six kwenye ligi hiyo. Matarajio ya wengi ni kumshuhudia tena Vieira kwenye ligi zenye ushindani mkali kama EPL.
Kwa sasa anafahamika zaidi kwenye kazi ya uchambuzi wa mechi za soka. Lakini, fowadi huyo wa zamani wa Ufaransa bado yupo kazini kwenye kazi ya ukocha baada ya kupita kwenye klabu za Monaco na Montreal Impact. Alikuwa kocha msaidizi pia wa Roberto Martinez kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji. Kazi yake ya siku za karibuni ni ukocha wa timu ya taifa ya Ufaransa ya vijana U-23.