Dodoma. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema baadhi ya vifaa vya ujenzi wa minara ya mawasiliano 758 kwenye maeneo ya vijijini, vilivyochelewa kuingia nchini vimeingia, hivyo wananchi wataanza kuona minara hiyo ikijengwa.
Nape amesema hayo leo Jumanne, Juni 11, 2024 wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Kalenga (CCM), Jackson Kiswaga.
Kiswaga amesema katika minara 758 aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hassan na jimbo la Kalenga lilipata minara 10.
“Ni lini wataenda kujenga minara hiyo katika Kata ya Masaka ambayo pia walipewa,”amehoji Kiswaga.
Akijibu swali hilo, Nape amesema ni kweli Rais Samia Suluhu Hassan alitoa minara 758 kwa ajili ya kupelekwa hasa katika maeneo ya vijijini na jimbo la Kalenga lilipata mgao huo.
Amesema changamoto iliyotokea ni minara hii yote 758, haiwezi kujengwa kwa wakati mmoja na kuwa inajengwa kwa awamu, hivyo bila shaka jimbo lake liko katika mchakato huo wa ujenzi.
“Ile iliyokuwa ijengwe na Kampuni ya Vodacom kulikuwa na changamoto waliagiza vifaa vyote kwa wakati mmoja kuwa vilichelewa kidogo kufika na hivi tunavyoongea vifaa vyote vinavyotakiwa viko nchini na ndani ya muda mfupi tutaona hiyo minara ikiinuka na wananchi watapata huduma wanazostahili kupata,” amesema.
Mbunge wa Mtwara Vijijini (CUF), Shamsia Mtanda amehoji ni lini Serikali itapeleka minara ya mawasiliano katika Jimbo la Mtwara Vijijini.
Akijibu swali hilo, Nape amesema inabidi wakajiridhishe iwapo maeneo anayoyataja mbunge kama hayapo katika ujenzi wa minara unaondelea nchini.
Amesema kama hayapo katika miradi watafanya tathimini na kuyaingiza katika mradi unaofuata ili wananchi wa jimbo hilo wapate mawasiliano.
Katika swali la msingi la mbunge wa viti maalumu (CCM), Dk Christine Ishengoma amehoji ni lini kata za Bwakila Juu, Singisa pamoja na Mkulazi Morogoro Vijijini zitapatiwa mawasiliano ya uhakika.
Akijibu swali, Nape amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ilitoa ruzuku kwa watoa huduma za mawasiliano ya simu kwa ajili ya ujenzi wa minara mitatu katika Kata ya Mkulazi katika awamu tofauti.
“Vodacom ilijenga mnara katika Kijiji cha Mkulazi, Halotel kijiji cha Chanyumbu na TTCL kijiji cha Usungura,” amesema.
Aidha, Nape amesema kwa upande wa Kata ya Bwakila Juu UCSAF iliingia makubaliano na TTCL kwa ajili ya kupeleka huduma katika kata husika na utekelezaji unaendelea.
Amesema Kata ya Singisa, Kampuni ya Airtel itajenga minara mitatu kwa ajili ya kuhudumia vijiji vya Nyamigadu ‘A’, Nyamigadu ‘B’, Lumba Juu, Lumba Chini, Ntala, Singisa na Kitengu.
“Serikali kupitia UCSAF itafanya tathimini ya hali ya mawasiliano ya simu katika maeneo husika baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa miradi inayoendelea hivi sasa na kuchukua hatua stahiki endapo kutatokea na maeneo yatakayokuwa hayana mawasiliano,”amesema.