Mwanafunzi asimulia alivyotumia dakika 10 kujiokoa kwa aliyemjeruhi kwa panga

Buchosa. Mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Ilenza iliyoko Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza Agnes Marco (17), amesimulia alivyotumia takribani dakika 10 kupambana na mtu aliyedai alitaka kumbaka wakati akitoka kuchanja kuni porini na wenzake 16 waliokimbia.

 Akisimulia tukio hilo leo Jumanne Juni 11, 2024 kwa simu akiwa Kituo cha Afya Kakobe anakopatiwa matibabu, Agnes amesema uthubutu na kumtanguliza Mungu ndiko kulimpa ujasiri wa kujinusuru asibakwe.

Anasema mtu huyo ambaye hakuweza kumtambua, aliwavamia njiani walipokuwa  wanarudi nyumbani wakiwa wamebeba kuni kichwani wakitokea Pori la Buhindi linalomilikiwa na Serikali.

“Mtu huyo alipoanza kunishambulia, wenzangu niliokuwa nao kila mmoja alikimbia kivyake na akawa amefanikiwa kunikamata mimi,” anasema Agnes.

Kati ya watoto 16 aliokuwa ameambatana nao, anasema yeye ndiye alikuwa mkubwa na mtu alimkamata akawa anamlazimisha warudi porini, lakini aligoma.

“Hapo ndipo alipoanza kunishambulia kwa panga alitaka anidhoofishe ili atimize lengo lake la kunibaka, lakini ilishindikana, wakati huo tayari alikuwa ameshanikata panga kichwani na mkononi,” anasimulia Agnes.

Anasema haikuwa kazi rahisi kupambana naye kwa kuwa alishamjeruhi mkono wa kulia, alitumia wa kushoto kujiokoa.

“Nilimnyang’anya panga kwa kutumia mkono wangu wa kushoto nikataka nimkate na mimi, akakimbia ndiyo nikaanza kupiga kelele huku nakimbia kuomba msaada,” anasema Agnes.

Akizungumzia hali yake, binti huyo anasema anaendelea vizuri licha ya kuuguza majeraha kichwani na mkononi.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Ilenza iliyoko Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, Agnes Marco (17) akiendelea na matibabu akiwa kituo cha afya Kakobe leo Juni 11, 2024.

Agnes ameiomba Serikali iweke kambi Kata ya Ilenza ili kuwabaini watu hao anaodai mara nyingi huwavamia wasichana wakienda kuokota kuni.

Daktaria aeleza hali ya mgonjwa

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kakobe, Venus Lusangija  amesema hali ya Agnes inazidi kuimarika akiendelea na matibabu chini ya uangalizi maalumu kutoka kwa madaktari.

“Hivi sasa anaugaza jeraha ambalo liko kichwani na mkononi, akiendelea hivi alivyo sasa, tunategemea kumruhusu arudi nyumbani na atakuwa akija kwa ajili ya kusafisha vidonda tu,” amesema Dk Lusangija.

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Ilenza wamesema kumekuwa na matukio ya wanawake na watoto wa kike kuvamiwa watokapo kuchanja kuni katika Pori la Buhindi.

“Uvamizi huu upo mara kwa mara, lakini hauripotiwi, tukio la mwanafunzi huyu kuvamiwa ndiyo limeleta mwanga na kutambua kuwa watu wanaofanya vitendo hivyo wapo, jamii inatakiwa kuwabaini ili wachukuliwe hatua,” amesema Martine Edward mkazi wa Ilenza.

Amesema kwa sasa kumekuwa na mtindo wa watu wasiojulikana kufanya vitendo vya kihalifu katani humo, hivyo anaviomba vyombo vya dora vichukue hatua ya kukomesha hali hiyo.

Kata ya Ilenza ni miongoni mwa kata 26 zinazounda Halmashauri ya Buchosa na licha ya kukumbwa na matukio ya uvamizi, viongozi wake wanatajwa kushindwa kuisimamia kutokana na malumbano ya wao kwa wao hali inayodaiwa kutoa mwanya kwa waharifu kutekeleza uovu wao.

Juni 10, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alifanya ziara ya siku moja kwenye Halmashauri ya Sengerema na alitoa maagizo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia haki na kutokomeza vitendo viovu vinavyofanywa na watu wachache na kuhatarisha maisha ya raia wema.

Amesema kama amani haipo, hakuna maendeleo kwa wananchi hivyo watu wanaofanya vitendo vya kiharifu na kudidimiza maendelo ya wananchi wanapaswa kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi.

Related Posts