Moshi. Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, limebariki adhabu ya kifo kwa wauaji watatu, akiwemo Jackson Msuya, aliyemuua mkewe kwa kumchoma visu mwilini na kumkata titi baada ya kugoma kurudiana naye.
Licha ya kumshambulia kwa visu na kumuua mkewe huyo aitwaye Parpetua Tumkaza, mkazi wa Kijiji cha Mhezi wilayani Same, Jackon aliwajeruhi kwa visu mama mkwe wake, Beatrice Japhet na baba mkwe wake, Charles Tumkaza.
Pamoja na jopo hilo la majaji, Dk Ndika, Zaphrine Galeba na Leila Mgonya kubariki adhabu hiyo ya kifo kwa Jackson, pia wamebariki adhabu ya kifo kwa watu wengine wawili— Denis Tarimo na Hamad Temu, waliomua Idd Mkojera kwa risasi.
Tukio hilo lilitokea saa 3:00 usiku, Januari 6, 2017 katika Kijiji cha Kisangesangeni wilaya ya Moshi, baada ya kundi la majambazi kumvamia mfanyabiashara huyo nyumbani kwake akiwa na familia yake wakiangalia televisheni kwa lengo la kupora.
Katika rufaa zote mbili walizozisikiliza, majaji hao walisema hawaoni sababu za kutokubaliana na hukumu za majaji waliosikiliza kesi hizo.
Walisema upande wa mashtaka ulithibitisha mashitaka yao kwa viwango na bila kuacha mashaka.
Majaji hao walisema vigezo muhimu vya kuthibitisha shtaka la mauaji ya kukusudia ambavyo, moja ni kifo kisiwe cha kawaida, mbili washtakiwa wawe ndio waliosababisha kifo na tatu, kuua kwao kulisababishwa na dhamira ovu, vilitimizwa.
Hukumu zote mbili zimetolewa Juni 11, 2024 katika kikao cha mahakama ya Rufani kilichoketi Moshi, na kwa kuwa Mahakama ya Rufani ndio chombo cha juu cha rufaa kwa mashauri ya jinai. Warufani hao watatu wamefika mwisho katika milango ya sheria.
Mauaji ya mke yalivyofanyika
Kulingana na hukumu hizo na uchambuzi wa ushahidi uliofanywa na majaji hao, kulikuwa hakuna ubishi kuwa Msuya na Perpetua walikuwa mume na mke, lakini kulitokea kutokuelewana, mke akarudi kwa wazazi Kijiji cha Mhezi.
Septemba 9,2017, saa 3:00 usiku, hapo Mhezi, familia ya mkewe ikimjumuisha marehemu, baba mzazi, Charles Tumkaza, mama mzazi, Beatrice Japhet, mdogo wa marehemu, Mary Charles, bibi na wajukuu walikuwa wakipata chakula cha usiku.
Wakati wakiendelea kula, Jackson aliwatembelea na kukaribishwa ambapo alijumuika na familia kupata chakula pamoja nao na baada ya kumaliza kula, Jackson akaomba maji ya kunywa ambayo aliletewa na kupewa na baba mkwe wake, mzee Charles.
Baadaye baba mkwe aliondoka na kwenda nyumba ya Jirani na kuiacha nyumba ya familia yake, akiwemo Jackson ambapo baadaye aliomba azungumze na mkewe nje ya nyumba, lakini mama mkwe hakuruhusu kwa kuwa mumewe alikuwa ametoka.
Katika jitihada zake za kujaribu kumshawishi marehemu akubali ombi lake hilo, Jackson aliahidi kumpa mkewe huyo Sh5,000 japo ombi hilo nalo lilikataliwa na hapo ndipo alipochomoa kisu na kumchoma mkewe begani, kifuani na kwenye mapaja.
Perpetua alipiga kelele kuomba msaada, akasimama na kukimbilia alipokuwa mama yake na kumkumbatia, Jackson akamfuata na kuanza kuwashambulia kwa kisu mkewe na mama yake, ambapo mama alijeruhiwa kwenye mbavu, kichwani na begani.
Baba mzazi wa marehemu aliposikia kelele hizo alirudi nyumbani na kuingia ndani kwa lengo la kuwaokoa mkewe na mwanae ambapo alimsukuma Jackson na mkewe na mwanae walifanikiwa kukimbia nje, hapo ndipo Jackson akamgeukia.
Alianza kumshambulia baba mkwe wake kwa visu, akamchoma mara mbili kwenye mbavu, mara tatu kichwani, mara mbili kwenye mapaja na mara moja mgongoni na kutokana na kelele za kuomba msaada zilizokuwa zikipigwa, Jackson akakimbia.
Mwenyekiti wa kitongoji, Nzinyangwa Abraham ndiye alikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio ambapo alijulishwa na Charles, Beatrice na Marry juu ya nini kimetokea na nani amefanya ambapo wote walitoka nje kwa ajili ya kumtafuta marehemu.
Nzinyangwa na Charles walifuatilia michirizi ya damu iliyowaongoza hadi katika migomba ambako marehemu alikuwa amelala chini na walipomuita alikuwa akiitikia kwa sauti ndogo, huku akiendelea kutokwa na damu nyingi maeneo aliyokuwa amejeruhiwa.
Katika hali ya maumivu makali, alimtaja mumewe kuwa ndiye aliyemshambulia baada ya kumkatalia ombi lake la kwenda naye nje kuzungumza, ili waweze kurudiana.
Wazazi wake walipata matibabu ya huduma ya kwanza na baadaye kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Same ambako nako walipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya KCMC walikolazwa, lakini marehemu alipofikishwa hospitalini Same, ilithibitika amefariki.
Muuaji alivyojitahidi kujinasua
Katika utetezi wake, Jackson alikanusha tuhuma hizo za mauaji, lakini pamoja na kukanusha, alikubali baadhi ya ushahidi uliotolewa na mashahidi mmojawapo wa marehemu alikuwa mkewe na walifanikiwa kupata mtoto mmoja.
Ushahidi mwingine aliokubali ni kuwa siku ya tukio, kwenye saa 2:00 usiku aliitembelea familia ya mkewe na baada ya kukaribishwa alipata nao chakula cha jioni na akakubali alipewa maji ya kunywa na baba mkewe na kwamba siku hiyo kulitokea ugomvi.
Alijitetea kuwa siku hiyo akiwa hapo, kulitokea ugomvi baina yake na baba mkwe wake na kwamba kiini cha ugomvi huo ni kitendo cha baba mkwe kumwagia maji kwa maelezo kuwa (baba mkwe) alimwambia hataki kumuona katika nyumba yake.
Jackson alikanusha kwenda na kisu kwenye nyumba ya baba mkwe wake, badala yake akadai kisu hicho kililetwa jikoni na mama mkwe wake kutoka katika moja ya vyumba.
Mahakama Kuu chini ya Hakimu Mkuu mkazi Moshi aliyepewa mamlaka ya nyongeza, Pamela Mazengo aliukataa utetezi wake na kukubaliana na upande wa mashtaka, msimamo ambao umechukuliwa pia na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani.
Wauaji wa mfanyabiashara nao kunyongwa
Katika hukumu ya rufaa iliyokuwa inapinga adhabu ya kifo, jopo la majaji hao liliitupa rufaa hiyo iliyowasilishwa na warufani wawili, Denis Tarimo na Hamad Temu, ambao walihukumiwa kifo kwa kumuua mfanyabiashara wa duka, Idd Mkojera.
Kulingana na ushahidi wa Jamhuri, Januari 6,2016 saa 3:00 usiku huko Kisangesangeni wilaya ya Moshi, marehemu (Mkojera) akiwa na mkewe, Mwajumua Temba na wanafamilia wengine, walikuwa wakipata chakula cga usiku, ghafla wakavamia na majambazi wanne.
Majambazi hao walikuwa wameficha sura zao kwa vinyago na waliwavamia wakiwa wamejihami kwa mapanga na visu na kuanza kumshambuliwa marehemu wakimtaka awape fedha na kuwaweka wanafamilia wengine chini ya ulinzi.
Wakati hilo likiendelea ndani ya nyumba ya kuishi, nje ya nyumba kukasikika mlio wa risasi ambapo majambazi wengine watatu waliingia ndani, lakini hawakuwa wameficha sura na walitambuliwa kuwa ni warufani na mwingine Zebedayo.
Baada ya kuingia bila kutoa onyo lolote, mrufani wa kwanza (Denis Tarimo) alimfyatulia risasi marehemu kutokea nyuma na alianguka na hakuamka tena, akaanza kutokwa na damu nyingi na kufariki dunia papo hapo.
Ingawa warufani waliegemea ushahidi wa kutokuwepo eneo la tukio muda na siku ya tukio, Hakimu Mkuu Mkazi, Pamela Mazengo aliukataa ushahidi wao na kuwatia hatiani kwa kosa la mauaji ya kukusudia na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Hawakuridhika na hukumu hiyo iliyotolewa Agosti 31, 2020 na kukata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania, lakini baada ya majaji kupitia sababu za rufaa pamoja na mwenendo wa kesi hiyo, wameona kesi hiyo ilithibitishwa kwa viwango na bila kuacha mashaka.