Biashara, Tabora  mechi ya akili leo

HESABU za nani kucheza Ligi Kuu baina ya Tabora United na Biashara United zinaanza leo Jumatano pale wapinzani hao watakapokutana katika mchezo wa kwanza wa play off.

Mchezo huo ambao utapigwa uwanja wa Karume mjini Musoma, Biashara United ndio watakuwa wenyeji dhidi ya wapinzani hao wa mjini Tabora.

Timu hizo zinakutana baada ya wenyeji kushinda hatua ya kwanza Play Off dhidi ya Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 4-0 katika Championship.

Tabora United wao walikunjwa pia kipigo cha jumla ya 4-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo wa hatua ya kwanza Ligi Kuu na sasa inatafuta huruma kupitia mchujo huo wa mwisho.

Tabora United ambayo awali ilijulikana Kitayosce, ndio msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu, ambapo haikuwa na matokeo mazuri walipomaliza nafasi ya 14 kwa pointi 27.

Biashara United ambao waliwahi kucheza Ligi Kuu kwa nyakati tofauti walishuka daraja misimu miwili nyuma, ambapo kwa sasa wanaisaka tena nafasi hiyo baada ya kumaliza Championship nafasi ya nne kwa pointi 59.

Baada ya mchezo wa leo Jumatano, timu hizo zitarudiana tena Jumapili, Juni 16 ambapo mshindi wa jumla atacheza Ligi Kuu msimu ujao, ambapo kama Tabora atakwama atashuka daraja, lakini iwapo Biashara atapoteza atabaki Championship.

Biashara wanashuka uwanjani wakijivunia rekodi ya matokeo mazuri kwenye uwanja wao wa nyumbani, ambapo katika michezo 15 ikiwamo wa play off, wameshinda 14 na sare moja dhidi ya Pamba.

Kocha Mkuu wa Biashara United, Aman Josiah alisema watawaheshimu wapinzani, lakini kiu yao ni kushinda kwa idadi kubwa ya mabao ambayo yatakuwa msaada mechi ya marudiano. Nini maoni yako, tuandikie ujumbe mfupi.

Related Posts