Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa kimetoa mwezi mmoja kwa Halmashauri ya jiji la Mbeya kujenga miundombinu ya mfereji katika makaburi ya Isanga yaliyopo Mtaa wa Mkuyuni.
Hatua hiyo imetokana na malalamiko ya wananchi kutokana na miili ya watu waliozikwa kwenye makaburi hayo kufukuliwa na kuelea kwenye maji au kusombwa hadi katika makazi ya watu kila zinaponyesha mvua kubwa.
Aprili 8, 2024, Mwananchi liliripoti kuhusu mvua kubwa zilizonyesha mkoani humo kufukua makaburi na miili ya watu waliozikwa kuonekana na mingine kusombwa na maji hadi kwenye makazi ya watu.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Juni 12, 2024, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mbeya, Christopher Uhagile amesema ni jambo la fedheha kwa jiji kushindwa kuboresha miundombinu hiyo na kusababisha miili ya watu waliozikwa kuonekana hadharani, jambo ambalo si la kawaida.
“Ninatoa siku 30 za kujengwa mifereji na tutafuatilia kuona kama Serikali imetekeleza ujenzi huo ili kujua hatua gani zitachukuliwa na kurejesha amani na utulivu kwa jamii inayoishi jirani na makaburi hayo,” amesema.
Amesema chama kama watekelezaji wa ilani, hawataweza kuvumilia jamii kuendelea kulalamikia suala hilo ambalo limeripotiwa miaka mitatu iliyopita na hakuna hatua zilizochukuliwa.
Awali akizungumza na Mwananchi Digital leo Juni 12, 2024, diwani kata ya Iganzo, Daniel Mwaipopo amesema ametoa taarifa mara kadhaa kwa uongozi wa jiji lakini hakuna majibu ya kuridhisha.
“Hili tatizo linajitokeza mfululizo kwa miaka mitatu sasa na taarifa za maandishi nilishapeleka. Kutokana na changamoto ya mfereji huo zaidi ya miili minane imeibuliwa na maji ya mvua, miwili ndugu walijitokeza, mmoja ulipotelea majini na mitano wananchi wamesaidiana na viongozi wa serikali kuizika maeneo mengine,” amesema.
Amesema kutokana na changamoto hiyo, wananchi mara kadhaa wamejichanga kununua saruji na mchanga kujengea kwenye makaburi ambayo yako hatarini kusombwa na maji.
“Kwa kweli, kama wananchi tumepambana sana kunusuru makaburi lakini kutokana na wingi wa maji tunakwama kwani nguvu yetu ni ndogo kifedha,” amesema.
“Tunaomba Serikali iingilie kati ili wananchi watuelewe kwani viongozi tunapitia vipindi vigumu tunapohojiwa na wananchi na sasa tunaelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025, tutawaeleza nini,” amesema.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema tayari bajeti wametenga kuna mambo ya ndani yakikamilika wataanza ujenzi wa mfereji huo.
Mkazi wa Mtaa wa Mkuyuni, Tumaini Samora amesema wanashindwa kuelewa sababu inayoikwamisha Serikali kujenga mtaro huo ikiwa ni miaka mitatu sasa imepita.
“Huenda kwa kuwa miili hiyo hawaishuhudii ndio maana hawajaweka kipaumbele au mpaka tuandamane ndio wataona kuna umuhimu wa kujenga,” amesema.