Watanzania wametakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuuhamasisha umma juu ya matumizi ya nishati mbadala ukiwemo Umeme Jua ili kutunza mazingira na kuokoa gharama za maisha.
Akiongea wakati wa maonesho ya kimataifa ya Kili Fair Arusha yenye lengo la kusaidia pia ukuaji wa sekta ya utalii, Meneja wa Masoko na Biashara wa Compact Energies Alfred Msafiri amesema Serikali kwa sasa inasimamia ajenda ya kimataifa ya matumizi ya nishati mbadala ikiwemo kuhamasisha matumizi ya majiko ya kupikia yanayotumia nishati ya gesi katika kutunza mazingira na kuzuia ukataji miti kwa ajili ya kuni.
Amesema katika kuunga mkono jitihada hizo, Compact Energies kupitia banda lake imetumia maonesho hayo kuelimisha umma juu ya matumizi ya nishati mbadala ya umeme jua ambao unapatikana kwa uhakika hapa nchini kwa sababu ya uwepo wa teknolojia ya kisasa ya uzalishaji huo na uwepo wa jua vipindi virefu vya jua kwa ajili ya kuzalisha nishati hiyo.
“Tukiwa kama kampuni ya Kitanzania, tunafurahia mazingira wezeshi ya kufanya kazi na kutoa fursa ya ajira kwa vijana na huduma bora kwa wateja wetu hapa nchini,”
“Tumewekeza katika vifaa vyenye ubora wa hali ya juu vinavyowezesha uzalishaji wa umeme wa uhakika muda wote na kutoa huduma kwa wateja wetu kwa gharama nafuu kabisa popote pale walipo,”, amesema.
“Hii ni katika kuiunga mkono Serikali ambapo kupitia huduma zetu, wateja wetu wanapata umeme jua wa uhakika na kushiriki katika ukuaji uchumi hapa nchini ,” amesema Msafiri wakati wa maonyesho hayo mkoani Arusha.
Wananchi mbalimbali walionyesha kuvutiwa na huduma za umeme jua kwa sababu ya unafuu wake ambapo mteja akifunga hakutani tena na gharama za matumizi.
Meneja wa Masoko na Biashara wa Compact Energies Alfred Msafiri akizungumza mteja wakati alipotembelea Banda la Compact Energies kwenye Maonesho ya Utalii ya Arusha Kili Fair yaliyofanyika jijini Arusha.