Dk Mwinyi: Mazingira mazuri yamewavutia wawekezaji

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema mazingira mazuri na miundombinu bora ndio inamfanya mwekezaji kuwekeza fedha zake, hivyo Serikali itafanya kila linalowezekana kuendelea kuboresha mazingira kukuza uchumi.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 12, 2024 wakati akizindua Hoteli ya The Mora inayomilikiwa na Kampuni ya Tui Group Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika kuhakikisha hilo, amesema ndio maana Serikali inaboresha na kujenga viwanja vipya vya Ndege.

Amesema utalii ndio sekta mama ya uchumi Zanzibar ukichangia asilimia 30 ya pato la Taifa, hivyo wanapopata wawekezaji kama hao wanatakiwa kuwapongeza kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kukuza uchumi.

“Wawekezaji ndio wanakuza uchumi katika nchi, kwa hiyo hatuna budi kuendelea kuwapa ushirikiano na kuboresha mazingira yetu kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” amesema Dk Mwinyi. 

Pia, amesema mwekezaji huyo amewekeza zaidi ya Dola 500 milioni za Marekani, “hawa sio wawekezaji wa mchezo, hawa ni wawekezaji wa kwelikweli tunashukuru kwa kuendelea kutuamini na kuleta uwekezaji wao hapa.”

 Dk Mwinyi amesema, “kwasasa tuna miradi mingi mizuri ya kuboresha na kujenga viwanja vya ndege, haya yote yanalenga kuwafanya watu wakifika katika nchi yetu wasikute mazingira hayaeleweki.”

 Amesema, hivi karibuni wanategemea kuwa na uwanja wa ndege wa kimataifa katika Kisiwa cha Pemba kwa kuwa tayari kuna mkataba ambao umeshasainiwa kujenga uwanja huo.

Amewataka wawekezaji kuangalia fursa za kuwekeza katika kisiwa hicho kwa kuwa awali changamoto ilikuwa ni kukosekana kwa uwanja na barabara.

Amesema kutokana na uwekezaji huo Serikali inafaidika katika maeneo makuu manne ikiwamo ajira na wananchi kuuza bidhaa zao katika mahoteli zao.

 “Wakulima wavuvi wadogo wauze katika hoteli hizi, tungependa bidhaa nyingi zinazopatikana ndani ya nchi wanunue na waagize nje zile ambazo hazipatikani,” amesema Dk Mwinyi.

Pia, kupitia uwekezaji huo nchi inapata kodi na kuendeleza miradi na miundombinu ya shule, maji, barabara na kuboresha huduma za afya.

Pia, eneo lingine la kunufaika ni kutoa huduma za kijamii na ni lazima sio hiari kwa hiyo wanatakiwa kujua matatizo yao wanapotoa msaada watoe katika eneo walilowekeza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uchumi na Uwekezaji (Zipa), Saleh Saad Mohamed amesema uwekezaji katika hoteli hiyo pekee unagharimu Dola 61 milioni za Marekani.

“The Mora itatoa ajira 600, na imeweka mifumo ambayo itasaidia mamlaka za mapato kufuatilia mapato yanayoingia hivyo kujua kila kinachoingizwa,” amesema Mohamed.

Related Posts