Dkt Batilda: Shirikianeni kupanga, kupima na kumilikisha ardhi

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inatelekeza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika halmashauri mbalimbali nchini zikiwemo za Mkoa wa Tanga.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zinazotekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) kushirikana na timu zinazotekeleza mradi huo ili kuhakikisha ardhi yote inapangwa, kupimwa na kumilikishwa kwa wananchi.

Dkt. Batilda ametoa agizo hilo mkoani Tanga wakati anafungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Juni 12, 2024 jijini Tanga.

Akinukuu maneno ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Batilda amesema Baba wa Taifa wakati akifungua mkutano wadau hao amesema “Ili taifa liendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.”

Mkuu wa Mkoa amesisitiza “Kwa mkoa wa Tanga watu wapo, siasa safi ipo, uongozi bora upo na ardhi ipo, tumeelezwa kuna migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali katika mkoa wetu, wajanja sasa hivi ni wengi. Mradi huu umekuja kusaidia kutatua changamoto hizi ili kukuza uchumi na kujiletea maendeleo yetu na taifa.”

Kwa upande wake Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Miliki za Ardhi Dkt. Upendo Matotola amesema mradi huo unatekelezwa nchini na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Januari 21, 2022 ilisaini makubaliano na Benki ya Dunia ya mkopo wa Shilingi bilioni 346 sawa na dola za kimarekani milioni 150 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Dkt. Matotola Mradi amesema mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano ukiwa na vipengele vinne vikilenga kuongeza usalama wa milki za ardhi, kuimarisha mifumo ya taarifa za ardhi, kujenga miundombinu ya ardhi na usimamizi wa mradi.

Mradi huo utatoa fursa katika kijamii kwa kuzingatia makundi maalum na kuleta usawa wa kijinsia na kuwezesha wamiliki wa ardhi kumiliki ardhi zao kisheria hatua inayosaidia kupunguza migogoro ardhi katika maeneo mbalimbali inayohusiana na matumizi ya ardhi hasa ya wakulima na wafugaji pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa shughuli maalumu.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika Mkoa wa Tanga unatekelezwa katika halmashauri miji za Tanga jiji, Korogwe DC na Mheza wakati kwa upande wa vijijini unatekelezwa katika halmashauri za Kilindi, Handeni na Mkinga.

Related Posts