MOJA kati ya stori kubwa ya kichekesho aliyowahi kukutana nayo bondia wa ngumi za kulipwa nchini na bingwa wa mkanda wa mabara wa World Boxing Federation ‘WBF’ katika uzani wa Super Middle ni ile aliyowahi kuandikwa na vyombo vya habari nchini kuwa ‘Kidunda adundwa’. Lakini sasa katika upande mwingine wa kiprotokali katika Serikali ya Tanzania, Kadunda ni mtumishi wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania ‘JWTZ’ akiwa katika cheo cha Sajini Taji ‘Staff sergeant’.
Kidunda ambaye ni kiasili ni mzaramo wa Kisarawe upande wa baba yake mzazi, mzee Salum Kidunda licha ya kuzaliwa mkoani Ruvuma kwa kuwa baba yake aliwahi kuishi huko kikazi kama afisa wa Shirika la Umeme Tanzania ‘Tanesco’ na ndiyo ilipo asili ya mama yake mzazi akitokea katika kabila ya Wangoni.
Tanzania imeanza kumfahamu Kidunda kupitia mchezo wa ngumi za ridhaa kutoka na ushiriki wake katika mashindano mbalimbali ya kimataifa yakiwemo Jumuiya ya Madola mwaka 2010 na mwaka 2012 katika mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto kabla ya mwaka 2014 kushiriki tena Jumuiya ya Madola.
Lakini ikamchukua miaka minne kuingia katika ngumi za kulipwa kwa pambano lake la kwanza kumchapa Karage Suba kwa TKO ya raundi tatu kabla ya mwaka 2020 kumtandika Shaban Kaoneka hadi kutangaza kwamba hazitaki tena ngumi ila Karim Mandonga alivyomrudisha.
Mpaka sasa Kidunda amecheza jumla ya mapambano 11 akiwa ameshinda tisa kati ya hayo saba ni kwa KO na ametoka sare mara mbili huku akiwa hajawahi kupigwa tangu aingie kwenye ngumi za kulipwa.
Katika mahojiano yake maalum na Mwanaspoti, Kifunda ambaye kituo chake cha kazi ni bendikoyi, Lugalo anafafanua kuwa maisha yake ya utoto yalijawaja na mambo ya utemi wa mitaani lakini amesisitiza yeye hakuwa mkorofi zaidi ya kupenda kujilinda mwenyewe.
Bondia huyo anaendelea kufunguka kuwa yeye amekulia Mburahati na wakati huo kama unajishi Mburahati basi lazima uwe mtemi kwa kuwa kulikuwa na mambo mengi ya kupiganapigana hali ambayo ilimfanya afanye mazoezi kutokana na asili yake ya uoga wa kuogopa kupigwa na wenzake.
“Huwezi kuwa mtemi bila ya kufanya mazoezi kwa sababu nilikuwa muoga wa kupigwa hivyo ikawa chachu kwangu ya kuweza kujifundisha mchezo wa ngumi.”
Sasa huo utemi ulikuwa katika njia gani?
Jibu: Unajua katika mazingira ya utoto ilikuwa unaweza kupigwa mtaa wa pili labda halafu unaambiwa ole wako upite mtaani kwetu. Sasa unajua ile michezo ya kitoto ndiyo inapelekea ujifunze kitu cha tofauti ili uweze kujiamini au imetokea umekutana na mtu kwenye mpira halafu ukampiga na yeye ndiyo anakwambia kwamba usikanyage mitaa yao, sasa mimi ndiyo nilikuwa sipendi.
Swali: Wewe umefanya mara ngapi?
Jibu: Utotoni imetokea mara nyingi sana kwa sababu yule Ayubu (mtumishi mwenzake jeshini) nilikuwa namwambia usipite mtaani na huyo ndiyo mtu ambaye nimecheza na kukuwa naye lakini nilikuwa namwambia hivyo.
Swali: Sasa kwa hali hiyo hujawahi kupiga mtu hadi ukapelekwa polisi kweli?
Jibu: Hahahah!, mambo hayo yalishawahi kutokea ila ni mambo ya kitoto lakini sijawahi kuwekwa ndani kwa ugomvi wa kitoto ila nakumbuka nilimpiga mtu kwa kuwa alimkaba baba yangu.
Swali: Ilikuwaje baada ya kumpiga?
Jibu: Kipindi baba anakutana na tatizo hilo tayari nimeshaanza kucheza ngumi za ridhaa katika gym yangu ya Mpitimbi, nakumbuka jamaa alikuwa mtemi sana mtaani. Nakumbuka alikuwa anaitwa Abbasi, wakati baba anapata shida hiyo nilikuwa nimetoka Rwanda kwenye mashindano ya Majiji. Baba akawa amerudi kutoka kazini usiku lakini akiwa anavuja damu kidoleni, kumuuliza akamtaja huyo mtu kwamba amemkaba, basi nakumbuka nilitoka kumtafuta hadi saa nane usiku sikuweza kumpata. Lakini siku ya pili baba yangu wakati anatoka kuchoma sindano ya tetenasi, akamkuta amekaa katika kijiwe chake basi akaja katuambia, nilitoka na kipensi hadi hapo kwenye kijiwe chake. Nilipofika na hasira zangu, watu wakasema waacheni mtu mbili (tupigane wawili), kiukweli yule jamaa nilimpiga sana licha ya utemi wake maana nilimpiga hadi akawa hajiwezi, unajua mtu anayecheza ngumi ukiwa unapigana na mtu ambaye hajui ngumi. Unajua kila nilipokuwa napiga nilikuwa napiga sehemu muhimu hadi ikafika kipindi kuinuka akawa hawezi, alizidiwa hadi watu waliokuwa wakiangalia pale wakawa wanaogopa, jamaa akaenda kulazwa hospitali. Nakumbuka hilo ndiyo tukio la mwanzo na mwisho maana nilikalishwa na familia ikanisema kwa kile ambacho nilichokuwa nimemfanyia yule kibaka tangu wakati huo sitaki tena yale mambo.
Swali: Wewe shule umesoma hadi ngazi gani?
Jibu: Kwanza nataka nikwambie kwamba mimi ni mtaalamu sana hesabu yaani watu niliosoma nao shule ya msingi wanajua kabisa hilo jambo ingawa nilishindwa kuendelea kutokana na maisha kuwa magumu. Unajua ilikuwa ngumu baada ya mzee kustaafu kazi maana alikuwa anafanya Tanesco, Songea na ndiyo maana Watanzania wengi wanasema mimi ni Mngoni ila ukweli mzee wangu ni mzaramo na mama ndiyo alikuwa Mngoni.
Swali: Nani alikupeleka kwenye ngumi za ridhaa?
Jibu: Kwanza ngumi nilikuwa napenda hata nilipoenda Gym nilitumia muda mchache kujifunza na nikawa napiga gym nzima, wenyewe wakagundua kama nina kipaji tena chini kocha Anthony Kanuti marehemu sasa.’
Swali: Ilikuwaje ukaweza kujiunga na jeshi?
Jibu: Naweza kukueleza kwamba kipaji ndiyo kimechangia kwa sababu nilikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga wenzangu ndiyo sababu iliopelekea kupata nafasi kwenye timu ya ngome. Unajua mimi sijacheza kwenye timu nyingi za majeshi kama mabondia wengine, nilicheza kidogo Magereza lakini baadaye ndiyo nikapata ajira JWTZ kupitia timu ya ngome.
Swali: Uliwahi kuwa na ndoto ya kuwa mwanajeshi?
Jibu: Hapana kiukweli sijawahi kabisa kuwa na ndoto hiyo ila tunapokuwa tunakuwa ndiyo kichwa kinaanza kufunguka.
Swali: Kidunda alidundwaje?
Jibu: Nakumbuka ilitokea katika kuwania kufuzu Olimpiki na Afrika Mashariki, tulifanikiwa kwenda kwenye mchujo wa mwisho Morroco, nilikuwa mimi na Mkenya. Sasa kule kuna bondia nilicheza naye akanipiga ndiyo waandishi wakaandika Kidunda adundwa, binafsi haikuniumiza kwa sababu ilikuwa Sehemu ya waandishi kuweka udambwi udambwi wao ili kunogesha walichoandika.
Swali: Kiliwapata nini katika michuano ya Jumuiya ya Madola, Scotland?
Jibu: Nadhani wakati ule chama cha ngumi kilifanya makosa kwa sababu ilikuwa bondia hawezi kupandishwa na kocha ambaye hana vigezo vya IBA na kigezo ni nyota, chama chetu kilisafirisha kocha ambaye hana nyota. Sasa wakati tupo kule, ikabidi nitafute kocha mwenye vigezo ili atusaidie wakati huo nilikuwa nimetoka katika Olimpiki ndiyo tukapata Mkenya kwa sababu kocha wetu hapakuwa na vigezo.
Halafu ndiyo ikatokea kichekesho kwamba mimi Mtanzania ila kocha alikuwa Mkenya na amevaa koti la bendera ya Kenya, watu walijadili sana ila sasa chama chetu kimepiga hatua.
Swali: Kwa nini umechelewa kuingia kwenye ngumi za kulipwa?
Jibu: Naweza kukueleza kubwa sijachelewa ingawa mashindano ya mwisho kwenye ngumi za ridhaa ni Olimpiki lakini baada ya kucheza ndiyo nimekuja huku kwa sababu nipo chini ya wakuu wangu. Sasa naamini kwa muda ambao nipo watu wataweza kuona vile ambayo hawakuviona kutoka kwangu na suala la lini nitaacha ngumi bado lipo kichwani muda ukifika nitaweka wazi kwa sasa mapromota walete kazi.
Swali: Kati ya pambano la Tshimanga Katompa na Asamahle Wellem lipi limekutesa?
Jibu: Binafsi yangu pambano la Katompa yule Mkongo niliteseka sana kwenye ulingo ila siyo huyu Asamhle kutoka Afrika Kusini. Unajua pambano la Asamhle nimepewa ndani ya muda mfupi halafu nilipata majereha ya goti na hili katika kambi yangu kila mmoja anajua ndiyo maana nilishindwa kuonyesha ukali ila namtaka tena halafu nipate miezi miwili ya kujiandaa, watapata majibu yao.
Swali: Unaoendelea kula vyakula gani?
Jibu: Kiukweli katika mambo ya kula mimi siyo mlaji kabisa, ugali wangu hata robo huwa simalizi, napenda sana matunda na juisi na wakati mwingine maziwa peke yake. Licha ya kuwa tunaambiwa mabondia tunakula sana lakini chapati mbili siwezi kumaliza kabisa mwisho wangu moja.
Swali: Wakati gani kwenye ngumi zimekupa pesa nyingi?
Jibu: Katika ngumi za ridhaa hakuna ambacho nimeweza kupata kwa maana ya pesa ingawa tunaweza kupata pesa ikiwa tunaenda nje huwa tunapewa pesa ya kuacha nyumbani.
Lakini katika ngumi za kulipwa naweza kuambia katika mapambano yangu ya mwisho mawili, nililocheza na Erick Mukadi, Mlimani City na ile la Asamhle ndiyo nimeweza kupata fedha nyingi kwa pamoja ambayo sikuwahi kufikiria ningepata.
Nashukuru pesa niliopata nimefungulia duka kubwa la spea za pikipiki mke wangu ambalo anakaa mwenyewe pamoja na mfundi wake yaani hata nikienda naona kabisa hii nguvu yangu.